Search This Blog

Sunday, March 23, 2014

MBEYA CITY: HAKUNA DHAMBI KUBWA KAMA KUKATA TAMAA, KWA UZURI GANI, MAFANIKIO GANI UNAJIHANGAISHA NA VIDUKU?

 
 
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam

HAKUNA dhambi kubwa kama kukata tamaa katika maisha. Inafahamika kuwa kuna changamoto nyingi zinazoweza kumkabili mtu na mwisho wa siku akajiona hawezi kufanikiwa tena.
Kumbe njia sahihi ni kukubali changamoto iliyopo mbele yako na kutafuta njia ya kukabiliana nayo.
Mafanikio si jambo la siku moja, zipo njia za kupita ili kufanikisha malengo yako.
Msimu huu wa 2013/2014  wa ligi kuu soka Tanzania bara kumekuwepo na ushindani mkubwa kuwania ubingwa.
Nafasi za juu kuna timu moja mpya kabisa ambayo ni Mbeya City. Msimu wa mwaka juzi, Simba sc klabu walikuwa wanachuana vikali na Azam fc kuwania ubingwa, huku Yanga akiwa nyuma yao akijikongoja.
Mwisho wa msimu, Simba waliibuka vidume baada ya kutwaa ndoo na kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika ambako walijitahidi kucheza kwa nguvu zote, lakini walitolewa.
Msimu wa mwaka jana, Simba naye akaa pembeni na kuwapisha Azam fc wakichuano  vikali kuwania ubingwa. Mwisho wa siku, Yanga wakaibuka wanaume na kuiwakilisha Tanzania mwaka huu ligi ya mabingwa barani Afrika.
Yanga hawajaweza kusonga mbele baada ya kukutana na kigongo cha Al Ahly ya Misri katika safari yao.
Japokuwa walitolewa kwa mikwaju ya penati 4-3 machi 9 mwaka huu nchini Misri, Yanga walipambana sana na kuonesha kukomaa zaidi.
Kwa mara nyingine msimu huu  kigogo wa soka la Tanzania, Simba sc hazungumzwi katika mbio za ubingwa.
Watu wanawazungumzia Mbeya City, Yanga na Azam fc waliopo nafasi za juu.
Ukiangalia katika misimu mitatu iliyopita, utagundua Yanga na Simba wamekuwa wakibadilika badilika, mara wana makali ya kutosha mara wanalowa.
Azam fc wanaonekana misimu yote ni washindani na ndio maana wamejaribu kutwaa ubingwa kwa misimu yote tangu wapande ligi kuu 2008/2009.
Wamekuwa wakiishia nafasi ya pili mara kwa mara. Hii inatoa picha kuwa Azam fc wanaanzia pale wanapoishia.
Katika maisha ya kawaida, kama mwaka huu umepata alama B, basi mwaka ujao unatakiwa kuanzia B kuelekea alama A.
Kama utapata alama C na mwaka jana ulipata B, basi ujue hauna mipango mizuri ya kuendeleza mafanikio yako.
Unaweza kushangaa Yanga  hawa hawa walioonesha soka kubwa katika mechi mbili za Al Ahly, mwakani wakawa wepesi kupita maelezo.
Tatizo la timu zetu ni kushindwa kuanzia pale zilipoishia.
Hoja Yangu leo inawahusu Mbeya City. Ni msimu wa kwanza kwao tangu wapande daraja.
Katika timu tatu zilizopanda daraja, wao ndiowameonekana kuwa bora zaidi na kuwashangaza wakongwe wa ligi ya Tanzania bara.
Rhino Rangers ya Tabora na Ashanti United ya Ilala, jijini Dar es salaam zipo katika wakati mgumu na zimeshindwa kuonesha makali yao mpaka sasa.
Leo Mbeya City fc  wanawahenyesha Simba, Yanga, Azam fc, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Coastal Union  ambao wana muda mrefu katika ligi zaidi yao.
Unaanzaje kuwabeza Mbeya City kwa kasi yao nzuri?. Mwanamichezo yeyote lazima akubali wanachofanya vijana hawa wa Juma  Mwambusi.
Jana nilishuhudia Mbeya City wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mabao hayo mawili yalifungwa na Sady Kipanga aliyekuwa mwiba mkali kwa kocha Fredy Minziro wa JKT Ruvu.
Haikuwa mechi yenye mvuto kwa mashabiki wa soka wenye mioyo miepesi. Lakini kwa watu wanaofahamu soka, walikuwa makini kujua nini kitatokeo.
Wakati Mbeya City wakicheza Chamazi, macho na masikio ya Watanzania wengi yalikuwa huko Tabora ambako Yanga walikuwa wanacheza na wenyeji wa uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Rhino Rangers.
Ilikuwa mechi muhimu kwa Yanga ikizingatiwa walikuwa hawajapata matokeo ya ushindi tangu watolewe ligi ya mabingwa.
Yanga walifanikiwa kushindwa mabao 3-0 ambapo bao la kwanza lilifungwa na Jerysonn Tegete, la pili,  beki wa Rhino alijifunga akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na Saimon Msuvu, huku msumari wa mwisho ukitiwa kambani na Hussein Javu.
Nia ya kwenda Chamazi ilikuwa ni kuonana na makocha wa Mbeya City na wachezaji wao.
Lengo lilikuwa ni kujiridhisha kama kweli wapo katika morali na malengo ya kutafuta ubingwa msimu huu.
Nilipofika uwanjani, `breki` ya kwanza ilikuwa ni kuzungumza na kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi ili kujua baadhi ya mambo niliyokuwa nahitaji.
Swali kubwa lilikuwa kama kweli wamedhamiria kuchukua ubingwa msimu huu.
Majibu ya mwalimu yalikuwa rahisi tu. “Bado hatujakata tamaa hata kidogo. Tunaendelea kupambana mpaka mwisho tujue nini kitatokea. Yanga, Azam fc wapo mbele yetu na sisi tunawafuata kwa karibu. Tunaamini inawezekana wao wakafanya vibaya na sisi tukafanya vizuri na kuwapindua juu”.
“Kila mechi kwetu imekuwa muhimu sana. Tunawaambia wachezaji wetu na wanajua wazi kuwa tunatakiwa kujituma zaidi. Umewaona katika mchezo huu, bado wana morali kubwa na wanahitaji kuleta historia”.
“Yanga walikuwa na mechi nyingi mkononi, lakini wameshindwa kupata ushindi katika mechi mbili, Unadhani ni kwanini”. Mungu anajua juhudi zetu. Lengo nikutowafanya wakae mbali na sisi. Huu mwaka wetu na lazima tuwaoneshe kuwa tumedhamiria”.
“Hatuna masihara hata kidogo. Kukata tamaa sio kawaida yetu. Tangu tukiwa ligi daraja la kwanza malengo yetu huwa ni ushindi. Tumekuja ligi kuu kwa mtazamo huo”.
Pia kocha huyo aligusia namna wanavyowadhibiti vijana wao katika masualaya nidhamu.
“Kamwe sisi hatuwezi kumthamini mchezaji kwa madai kuwa amekuwa na kiwango kikubwa. Tunawadharau tu kuonesha kuwa bado hawajafika wanapotaka”.
“Kuna wakati mambo ya ndani ya klabu yanakuwa magumu. Lakini huwa wanatambua kuwa ipo siku watafika. Tunakaa nao na kuwashauri zaidi”.
“Ndio maana huwezi kuona vijana wetu wanajipamba kwa kunyoa `Viduku`,, Tunawauliza kwa uzuri gani walionao waonekana tofauti na wengine?. Kwa pesa gani waliyonayo wajipambe?”.
Haya yalikuwa majibu ya kocha Maka Mwalwisyi. Ukiyapima kwa undani kuna mambo makubwa matatu aliyosema.
Moja; kutokata tamaa. Nilisema mwanzo kuwa kukata tamaa ni dhambi kubwa. Mbeya City hawajaonekana kukata tamaa hata kidogo. Wanapambana hadi mwisho wa safari. Kama itatokeo kushindwa kufanikiwa, bila shaka watarudi na kujipanga upya. Kama watafanikiwa basi watakuwa wametimiza ndoto zao msimu huu.
Kujiamini kwao kunaonesha wanajitambua na wamepanga malengo yao. Hii ni nzuri, nimeipenda sana.
Pili; wanazungumza sana na wachezaji wao kuwajenga kinidhamu na kuwafanya wajione wana deni kubwa kwa klabu na katika maisha yao.
Wachezaji wa Mbeya City wanaonekana wazi kuwa na nidhamu kubwa uwanjani na kwenye mazoezi. Nadhani ni matundo ya makocha wao.
Tatu; wachezaji wao wamefundishwa maisha kuwa yanahitaji subira. Ndio maana wanavumilia kila matatizo klabuni kwao. Hawazungumzii shida zao hata siku moja. Huwezi kuwasikia wakisema wamecheleweshewa mishahara wala posho. Haimaanishi wanalipwa vizuri, la hasha! Bali wanajitambua tu kuwa Mbeya City ni kama njia ya kusonga mbele.
Mawazo yao yako vizuri sana. Hawana muda wa kujiona wanaweza. Huwezi kisikia kutofautiana na makocha wao. Hakika kwa hili wameweza kufanikiwa.
Kwa mtazamo rahisi, Mbeya City wamekomaa kimawazo na kiakili. Wachezaji na makocha wanaishi kama baba na wanae.
Wanaheshimu mawazo ya Maka Mwalwisyi na Juma Mwambusi wenye dhamana ya kuwajenge  katika maisha yao ya  kisoka.
Kwa mtazamo huu wa kuwa na matumaini au malengo makubwa kwa Mbeya City ni jambo jema la kuigwa.
Itakuwa furaha siku moja kuona timu kama Mbeya City zinakuwa nyingi zaidi ili kubadili ligi yetu ambayo kwa miaka mingi imetawaliwa na Simba, Yanga.
Hata kama Mbeya City hawatashinda taji msimu huu, bado wanahitaji pongezi kubwa zaidi.
Ukiwaona uwanjani wanacheza na Yanga, Azam fc au Simba huwezi kutofautisha nani ana wachezaji ghali na wa kimataifa.
Hawana watu kama Amisi Tambwe, Donald Mosoto, Joseph Owino, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza, Emmanuel Okwi , Kipre Tchetche, Brian Umony na wengineo, lakini wanapokutana uwanjani na `mastaa` hawa huwa kunakuwa na shughuli pevu.
Huwezi kuwatofautisha kwa haraka. Ni hatua nzuri kimpira na wanastahili pongezi.
Najua ni ngumu kwa baadhi ya watu kuwakubali kwa kile wanachokifanya, lakini ukweli unabaki palepale kuwa Mbeya City wana mtazamo mpya na endelevu.
Kikubwa kwao ni kuanzia pale watakapoishia msimu huu. Itakuwa mbaya zaidi kama watageuka kuwa `mboga` msimu ujao.
Hakika watadhihirisha yale maneno ya watu wengi kipindi wanakuja kuwa ni `nguvu ya soda”.
Mbeya City hongereni sana kwa mtazamo wenu, najua wapo watu wengi nyuma yenu wakiwaunga mkono. Fadhila kubwa kwao ni kuucheza mpira tu.
Pia wapo wapinzani wenu, kama mtalewa sifa na kujiona mmefika, basi mtawapa watu cha kuzungumza.

No comments:

Post a Comment