Dunia na wapenzi wa soka kiujumla wamepata fursa ya kuona na
kushuhudia vipaji na ufundi mbalimbali unaoonyeshwa au uliowahi kuonyeshwa na
wanasoka mbalimbali ulimwenguni kiasi ambacho baadhi ya majina ya wanasoka
ambao wameamua kutundika daruga la kusakata mchezo huo wa kabumbu ulimwenguni
yakiendelea kukaa vichwani na kutajwa midomoni mwa wapenzi na mashabiki wa soka
ulimwenguni.
Miongoni mwa wachezaji ambao licha ya kuamua kupumzika na
mikikimikiki ya mchezo wa soka bado wamebakia kuwepo katika ubongo wa wapenzi
wa soka ulimwenguni ni kiungo fundi wa ushambuliaji wa vilabu vya Barcelona na
PSV Eindhoven, Phillip John William Cocu ambaye dunia ilimtambua kwa kifupi cha
jina lake Phillip Cocu.
KIPAJI TOKA EINDHOVEN
Phillip Cocu alizaliwa mnamo tarehe 29,Oktoba 1970 katika
kitongoji cha Zevenaar kilichopo katika jii lenye wanazi sugu wa soka la
Eindhoven. Ikumbukwe kwamba jiji la Eindhoven ndipo inapotoka timu iliyoweza
kutikisa nchini Uholanzi na Ulaya kwa ujumla mwishoni mwa miaka ya tisini na
mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili ya PSV Eindhoven.
Kama ilivyo ada kwa watoto wengi wanaozaliwa wakiwa na
vipaji vya soka, Cocu alijiunga na timu ya watoto ya mtaani kwao ya DCS kabla ya baadae kujiunga na timu nyingine
iliyopo katika mtaa huo ya De Graafschap ambayo aliichezea mpaka mwaka 1988
ambapo alijiunga rasmi na soka la kulipwa katika timu ya AZ Alkmaar ambayo
aliichezea kwa muda wa miaka miwili tu ambapo baadaye alijiunga na klabu ya
Vitesse .
Akiwa Vitesse, Cocu alipata majeruhi mwanzoni tu mara baada
ya kujiunga na klabu hiyo jambo lililopelekea kutishia kipaji chake lakini
alifanikiwa kupigana na majeruhi hayo ya goti ambayo na kurudi uwanjani kwa
kishindo na kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
AJIUNGA NA KLABU YA NDOTO ZAKE
Baada ya kuichezea timu ya Vitesse kwa muda wa miaka mitano
katika michezo 137 na kufanikiwa kuifungia timu hiyo jumla ya magoli 25, Cocu
alisajiliwa rasmi na klabu maarufu ya PSV Eindhoven ambayo inatoka katika jiji
alilozaliwa la Eindhoven mnamo mwaka 1995.
Cocu aliuelezea uhamisho huo kuwa ni ukamilisho wa ndoto
zake za muda mrefu za utotoni huku akiishukuru klabu ya Vitesse na mashabiki
wake kwa kumsapoti katika matukio shida na furaha aliyowahi kukutana nayo
ikiwemo majeruhi ya muda mrefu aliyopata pindi alipojiunga na timu hiyo huku
wakimchukulia kama miongoni mwa mashujaa wao klabuni hapo.
APIGA SOKA LA UHAKIKA
PSV, ATUA BARCELONA
Mara baada ya kujiunga na klabu ya PSV Eindhoven, Cocu
alifanikiwa kupata alifanikiwa kujitengenezea namba ya kudumu katika timu hiyo akicheza
katika nafasi ya kiungo mshambuliaji nafasi ambayo alikuwa akiimudu vilivyo na
kufanikiwa kutwaa mataji mawili maarufu nchini humo ya KNVB na lile la ligi kuu
nchini humo lijulikanalo kwa jina la Eredivisie mnamo mwaka 1997.
Akiwa hapo, Cocu alifanikiwa kucheza jumla ya mechi 95 huku
akifanikiwa kuifungia timu hiyo jumla ya magoli 31 katika mechi hizo
alizocheza.
Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata kabumbu, vilabu
mbalimbali barani Ulaya vilianza kuinyemelea saini yake lakini ilikuwa ni klabu
ya Bercelona iliyofanikiwa kuinasa saini yake mnamo mwaka 1998.
ATESA BARCELONA ,
APEWA UNAHODHA
Cocu katika misimu yote aliyoichezea klabu hiyo ya Hispania
inayotokea katika kitongoji cha Catalan, alifanikiwa kuteka nyoyo za wapenzi na
mashabiki wa timu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza soka jambo
ambalo lilipelekea Mdachi huyo kupewa unahodha klabuni hapo, huku akifanikiwa
kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la nchi hiyo maarufu kama La Liga, huku
Barcelona ikifanikiwa kucheza katika nusu fainali mbili za mashindano makubwa
na maarufu ya vilabu barani Ulaya yajulikanayo kama Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia akiwa Barcelona, Cocu alifanikiwa kuweka rekodi ya kuwa
mchezaji wa kwanza wa kigeni kuweza kuichezea mechi nyingi timu ya Barcelona,
ambapo aliichezea timu hiyo jumla ya mechi 205 huku akifunga jumla ya magoli 31
AAMUA KURUDI NYUMBANI
Baada ya miaka sita
ya mafanikio ndani ya Barcelona, Phillip Cocu aliamua kurudi katika klabu aliyoipenda
ya PSV Eindhoven ambako aliweza kuisaidia timu hiyo kushinda jumla ya mataji
matatu ya ligi kuu nchini humo huku pia akiisaidia timu hiyo kufika nusu
fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, huku ikiwa ni nusu fainali yake ya
tatu katika mashindano hayo.
Inasemekana, Cocu aliamua kurudi zake nyumbani Uholanzi ikiwa
ni kama njia ya kumpisha nyota wa Kihispania aliyekua anachipikia klabuni hapo
ambaye baadae ametokea kuwa staa na nahodha wa tim hiyo, na huyu si mwingine
bali ni Xavi Hernandez.
AMALIZIA SOKA
UARABUNI,ANG’ARA TIMU YA TAIFA
Mara baada ya awamu ya pili ya mafanikio ndani ya klabu ya
PSV,Cocu aliamua kutimkia zake Uarabuni ambako alikwenda kumalizia soka lake
katika klabu ya Al Jazira.
Kutokana na soka lake la uhakika alilolionyesha katika timu
mbalimbali, Cocu alifanikiwa kujiwekea nafasi ya kudumu katika timu ya Taifa ya
Uholanzi ambayo aliichezea jumla ya mechi 101 na kuifungia jumla ya magoli 10.
Miongoni mwa matukio ya kusisimua ya Phillip Cocu akiwa na
timu ya Taifa ya Uholanzi, ni kuifungia timu hiyo magoli mawili katika Fainali
za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Ufaransa mwaka 1998 lakini baadae akaja
kukosa penati muhimu dhidi ya Brazil katika mchezo wa nusu fainali ambapo
Uholanzi iliondolewa kwa mikwaju ya penati na miamba hiyo ya soka ulimwenguni.
AGEUKIA UKOCHA
Mara baada ya kuamua kutundika daluga la kucheza soka, kama
ilivyo kawaida ya wanasoka wengi waliostaafu kucheza soka, Cocu aliamua
kujikita katika ukocha wa mchezo huo wenye mashabiki wengi ulimwenguni ambapo
hivi sasa anainoa klabu anyoihusudu ya PSV Eindhoven ambayo ameiwezesha kufika
katika hatuanya mtoano ambayo walitolew na timu ya AC Milan hivi karibuni, huku
wakipata nafasi ya kushiriki katika mashindano ya Europa League.
Imeandaliwa:
CHARLES ABEL-SAUT
0713 923276
Email: charlesabel46@yahoo.com
No comments:
Post a Comment