Na Oscar oscar Jr.
0789-784858
Kuna
muda huwa nikimkuta mtoto ameshika rimoti ya Runinga,huwa sipendi kukaa
sebuleni siku hiyo na sababu yangu kubwa ni moja tu.sipendi kuhangaisha
macho yangu.Kila mtoto anavyobonyeza rimoti,ndivyo anavyokamilisha
furaha yake.Dakika moja akiweka chaneli inayoonyesha taarifa ya
habari,sekunde kadhaa zinazofuata,utamuona kaweka chaneli ya katuni na
baadae,atakupeleka kwenye picha la kivita au mieleka.Kadri unavyozidi
kukolea kwenye chaneli moja,ndivyo na yeye anavyoongeza manjonjo kwenye
kuzibadilisha!
Sioni tofauti ya akili hizi za kitoto na
anachofanya kocha wa sasa wa klabu ya Bayern Munich,Pep
Gaudiola.Ndiyo,Pep Gaudiola ana akili za kitoto.Wakati ukifurahia
kumuona Philip Lahm akifanya vema kama beki
wa kulia,yeye anamtumia kama kiungo mkabaji na timu inashinda.wakati
dunia ikimkubali kwa sasa Javi Martinez kama moja ya viungo bora,yeye
anamtumia kama beki wa kati na timu inapata pointi 3.Unadhani Pep
Gaudiola anatofauti gani na mtoto aliyeshika rimoti?
Kuna siku
Pep Gaudiola atampanga golikipa wake Manuel Neuer kama mshambuliaji huku
Mario Mandzukic akianza golini na sintoshangaa kuona mechi hiyo
wanashinda.Unajua kwa nini? Bayern Munich ni timu iliyokamilika kwa
sasa,hawakamatiki.Wanapokuwa wanamiliki mpira,timu yote inashambulia na
pindi wanapopoteza,wote wanarudi kukaba na kuusaka mpira ulipo.Unataka
nini zaidi? Bayern walimuuza kiungo Luiz Gustavo na mshambuliaji wao
Mario Gomes,kuna mtu anajali?
Msimu wa 2008/2009 Pep Gaudiola
alipewa rasmi mikoba ya kuwa kocha mkuu wa klabu ya Barcelona toka kwa
aliyekuwa kocha wa kipindi hicho,Frank Rijkaard na katika msimu wake wa
kwanza,Pep Gaudiola alishinda mataji matatu ambayo ni Kombe
la Mfalme,La Liga na klabu bingwa Ulaya ambapo aliweza kuandika
historia ya kuwa kocha wa kwanza mwenye umri mdogo kuwahi kutwaa kombe
hilo la Ulaya.Na kwa ufupi tu,Gaudiola ni moja ya makocha bora duniani
huku mwaka 2011 akiibuka mshindi wa Balon D'or na kutangazwa kocha bora
wa Dunia.
Baada ya kuachana na klabu ya Barcelona,alijipa muda
wa mwaka mmoja kupumzika huko nchini Marekani.Msimu huu amerejea kwenye
kazi yake na sasa ni kocha wa mabingwa wa ulaya Bayern Munich.Alianza
msimu vibaya huku akipoteza kombe la ufunguzi (German Super Cup)dhidi ya
wapinzani wao klabu ya Borussia Dortmund lakini,baadae alifanikiwa
kuwatuliza watu kwa kunyakuwa kombe la European Super Cup kwenye mchezo
dhidi ya Chelsea na baadae,akatwaa kombe la dunia kwa vilabu kwenye
ardhi ya Afrika kule Morocco.
Mchezaji wa zamani wa timu ya
taifa ya Nigeria na mchambuzi wa soka Sunday Oliseh,kwenye moja ya
makala zake ambayo iliipa jina la "Why Bayern is best"
anasema,moja ya sababu za kuifanya Bayern kuwa timu bora ni pamoja na
kutoruhusu wachezaji wake inaowategemea kuondoka katika klabu hiyo
huku,ikitengeneza mazingira mazuri ya kumshawishi mchezaji yoyote yule
bora duniani kujiunga na wababe hao wa Ulaya.
Kwa nyakati
tofauti,Bastian Schweinstiger,Arjen Roben,Frank Ribery na Philip Lahm
wamewahi kutakiwa na baadhi ya vilabu vikubwa barani Ulaya lakini,Bayern
wameendelea kuwashikilia wachezaji hao kwa kuwapatia kila
wanachokitaka.Pamoja na kikosi hicho kutikisa dunia msimu uliopita,bado
waliingia sokoni na kumnunua kiungo mshambuliaji Mario Gotze kutoka
Borussia Dortmund na Thiago Alcantara kutoka klabu ya Barcelona na kwa
taarifa zilizopo ni kwamba,mshambuliaji Robert Lewandowski kutoka klabu
ya Borussia Dortmund na Julian Draxler kutoka Schalke 04 huenda
watajiunga na wababe hao wa Ulaya mapema msimu ujao.
Takwimu
zinaonyesha kuwa,klabu ya Bayern Munich inawastani wa mashabiki 71,000
ambao
wanahudhuruia kila mechi ya bundesliga ambayo Bayern wanacheza katika
uwanja wao wa nyumbani msimu huu.Kutokana na mashabiki wao kuwaunga
mkono,ndiyo maana jamaa waliamua kuacha kabisa kuitumia jezi yao namba
12 kwa mchezaji yoyote yule huku wakiamini,inavaliwa na utitiri wa
mashabiki wao.
Kuiongoza timu ambayo imetoka kutwaa mataji
makubwa matatu kwenye msimu uliopita chini ya kocha bora wa dunia kwa
sasa,Juup Heynches,sio kazi ndogo.Heynches alifanikiwa kutwaa kombe la
Ligi,Bundesliga na lile la klabu bingwa Ulaya msimu uliopita lakini,Pep
Gaudiola anaendelea kuithibitishia dunia kwamba alikuwa mtu sahihi wa
kuchukuwa mikoba ya kuinoa timu hiyo ya Ujerumani huku akiwa hajapoteza
mchezo wowote wa Bundesliga msimu huu.
Mkongwe wa Bayern
Munich,Ruud Gullit amesema "Hata kama wewe ni adui namba moja wa klabu
ya Bayern ni wazi kwamba kwa sasa utakubali kwamba hawakamatiki" wakiwa
chini ya kocha Gaudiola,wanawastani wa asilimia 68 katika
kumiliki mpira huku wakiwa wanafunga magoli mengi sana.kabla ya kucheza
na arsenal mechi za ligi ya mabingwa Ulaya,walikutana na klabu za Vfl
Wolfsburg,Schalke 04 na Hannover 96 kwenye muendelezo wa michezo ya
bundesliga na katika michezo hiyo mitatu,Bayern wameshinda yote huku
wakifunga magoli 15 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 2 tu.
Baada
ya mechi yao na Vfl Wolfsburg kumalizika kwa Bayern kuibuka na ushindi
wa bao 6-1,Pep Gaudiola alionyesha kutoridhika na kiwango
kilichoonyeshwa na timu yake.Sikumuelewa alikuwa anamaana gani
lakini,baadae nikagundua kuwa,huyu jamaa aliwahi kumfanya Sir Alex
Ferguson atetemeke vidole kwenye fainali ya klabu bingwa pale kwenye
dimba la Wembley,nadhani kwa sasa,anatamani kuona makocha wenzie
wakiomba kwenda "kuchimba dawa" kabla ya dakika 90 za mchezo kumalizika
ndiyo roho yake itaridhika!
Pep Gaudiola ndiye aliyeshika rimoti
kwa sasa,kuna muda anatuonyesha picha za kivita na kuna muda,anatuwekea
picha za katuni tuangalie.Unadhani nitasema nini sasa? Sehemu pekee
inayoonekana ina mapungufu kwa mchezaji mmoja mmoja,ni beki ya kati
anapocheza Jerome Boateng na Dante,lakini unawezaje kuwafikia hawa jamaa
wakati mbele yao kuna "wanajeshi" Bastian Schweinstiger na Javi
Martinez? inabidi tu ukubali kuangalia chaneli anayokuchagulia Pep
Gaudiola maana ukileta ubishi,anaweza kumuanzisha Thiago Alcantara na
Toni Kroos,ikawa ni balaa lingine!
Kwa mara ya kwanza Bayern
wameweza kukusanya alama 68 katika mechi 24 tu za bundesliga,na kuna
uwezekano kabla ya kuumaliza mwezi machi,watoto wa Gaudiola wakawa
washatangazwa mabingwa wapya wa Bundesliga.Bado unaswali kwa Pep
Gaudiola? kwa namna anavyowatesa wapinzani,kuna siku mchezaji ataomba
ruhusa kwa mwamuzi ili "akachimbe dawa" kabla ya muda wa mapumziko!
ukirejea
mechi zake mbili dhidi ya Arsenal za klabu bingwa Ulaya,utagundua
kuwa,yeye ndiye alikuwa ameshika rimoti huku kocha wa Arsenal,Arsene
wenger akiwa kwenye kochi akitazama chaneli anazowekewa na Pep
Gaudiola.Kwani hili linaubishi? hapana,kila kitu kinajieleza uwanjani.
kwenye
mechi ya Emirates,Gaudiola alianza kwa kuweka chaneli ya katuni na
arsenal wakapata penati,walipokosa tu,akaweka picha la kivita na mpaka
dakika 90 zinamalizika,Arsenal 0-2 Bayern.Mechi ya pili pale Allianz
Arena,Gaudiola alifungulia picha la "wanamitindo" burudani kwa kwenda
mbele na mwisho wa siku,bayern walipiga pasi 791 huku arsenal
wakifikisha pasi 497 na mchezo ulimalizika kwa kufungana bao 1-1 bila
kutuonyesha picha la kivita!
Pep Gaudiola alifanikiwa kushinda
mataji 14 ndani ya miaka minne alipokuwa anaiongoza Barcelona kwa aina
hii hii ya kuwabadilishia wenzie picha za kutazama.Kadri anavyozidi
kukaa na timu,ndivyo inavyozidi kuwa tishio na ndivyo anavyozidi
kubadilisha chaneli kama mtoto.Rais wa Bayern Munich amefungwa wiki hii
miaka mitatu na nusu jela na pengine hali hii inaweza kuiathiri
Bayern lakini,bado ninauhakika kwamba rimoti ya runinga iko mikononi
mwa kocha Pep Gaudiola.
No comments:
Post a Comment