Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
WAKATA Miwa wa Kagera Sugar aprili 5 mwaka huu wanawasubiri kwa hamu kubwa
katika dimba la Kaitaba, wanyonge wa
Coastal Union na Azam fc katika mechi mbili zilizopita, Wekundu wa Msimbazi,
Simba sc.
Simba watasafiri kuwafuata Kagera Sugar katika mechi
hiyo ya mwisho ya ugenini msimu huu, huku wakiwa wapole zaidi kwasababu hawana
chao katika nafasi mbili za juu.
Kocha msaidizi wa Kagera, Murage Kabange ameuambia
mtandao huu kuwa baada ya juzi dhidi ya
Ruvu Shooting ambapo walitoka suluhu ya bila kufungana, kikosi chao kipo katika
hali nzuri na wameanza maandalizi ya mechi ijayo dhidi ya Simba.
“Tunamshukuru Mungu kikosi chetu kimeimarika mechi
hizi za mwisho. Tumesumbuliwa na majeruhi karibu msimu mzima. Mechi zilizobaki
tutahakikisha tunashinda. Ilitakiwa tuanze
na Ruvu Shooting, lakini bahati haikuwa upande wetu”.
“Mchezaji wetu Salum Kanoni alikosa penati. Ilikuwa nafasi nzuri ya kupata bao, kakini
ndio Mpira”. Alisema Kabange.
Kocha huyo alisema mechi ijayo dhidi ya Simba
itakuwa ngumu kwasababu Simba ni timu nzuri japokuwa imekuwa na msimu mbaya.
“Mshambuliaji Amisi Tambwe ni hatari sana. Wapo
wengine ambao wana kiwango kizuri, lakini tunajiandaa kikamilifu ili kupata
ushindi dhidi ya wapinzani wetu”.
“Tunajua
kwasasa hatuwezi kuchukua ubingwa wala nafasi pili. Tunapigania nafasi ya tatu
au ya nne ambayo tulishika mwaka jana. Chini ya hapo si matarajio yetu hata
kidogo”. Alisema Kabange.
Kabange aliongeza kuwa mashabiki wao wamekuwa
wavumilivu na kuwatia moyo zaidi katika mechi zao za nyumbani, hivyo amewataka
kujitokeza zaidi mechi ijayo katika dimba la Kaitaba.
Wakati Kagera Sugar wakiwa katika maandalizi
kabambe, Simba wamekuwa katika hali tete baada ya kufungwa mechi mbili
zilizopita dhidi ya Coastal Union na Azam fc.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Dravko Logarusic
alikaririwa kuwa anashangazwa na matokeo ya timu hiyo, licha ya kucheza vizuri
na kutengeneza nafasi za kufunga.
Loga mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa ligi
imekuwa ngumu kwake kwasababu timu zote zimejiandaa vizuri.
“Huwezi kuingia uwanjani kwa kujiona ni timu kubwa.
Timu ndogo zimekuwa zikioneshs upinzani mkubwa zaidi msimu huu.”.
“Nawashangaa wachezaji wengi wa kiafrika,
wanapocheza na timu kubwa wanaonesha kiwango kikubwa, lakini wakikutana na timu
ndogo wanacheza chini ya kiwango”. Aliwahi kutamka Loga.
Hata hivyo Simba kupitia kwa Afisa habari wake, Asha
Muhaji walisema wao wanakubaliana na matokeo yanayotokea uwanjani na
kilichobaki ni kufanya vizuri mechi zilizosalia ili kulinda heshima yao.
Mechi dhidi ya Kagera itakuwa ngumu kwa Simba
kwasababu hata rekodi zinaonesha kuwa timu hizi zimekuwa mahasimu wakubwa tangu
mwaka 2010.
Katika mechi saba walizokutana, Mnyama aliyekosa
meno kwa sasa ameshinda mechi mbili, wakati Kagera wameshinda mara moja na
kutoka sare mara nne.
Mechi ya mzunguko wa kwanza, timu hizo zilitoka sare
ya bao 1-1 kufuatia Kagera kusawazisha dakika za lala salama kwa mkwaju wa
penati iliyofungwa na Salum Kanon.
Bao hilo lilileta kizazaa kwa mashabiki wa Simba
kwani walilipuka kwa kufanya fujo na kung`oa baadhi ya viti vya uwanja wa Taifa
na kulilazimu jeshi la polisi kutumia mabomu ya machozi kuwaondosha mashabiki hao uwanjani.
Sababu ya fujo hizo ilikuwa ni kutoridhishwa na
maamuzi ya mwamuzi baada ya kuwazawadia penati, `Wanankulukumbi` Kagera Sugar.
Mpaka sasa timu hizo zipo katika nafasi tofauti
kwenye msimamo wa ligi kuu msimu huu.
Simba sc wapo nafasi ya nne kwa pointi 36 baada ya
kushuka dimbani mara 23.
Wakati Kagera Sugar wapo nafasi ya tano kwa pointi
33 baada ya kushuka dimbani mara 22, huku wakiwa na kiporo dhidi ya Yanga
Aprili 9 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment