Search This Blog

Monday, March 24, 2014

MASHABIKI SIMBA WATULIZWA JAZIBA, LOGA KUSUKA KIKOSI KAZI KUWAVAA AZAM , KAGERA SUGAR, ASHANTI, YANGA MECHI ZILIZOSALIA!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


KIPIGO cha bao 1-0 walichopokea Simba sc kutoka kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga  jana  uwanja wa Taifa  katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara kimezidi kuwavuruga  na kuwafanya wawe wanyonge  ngwe hii ya lala salama.
Wagosi wa Kaya wakiwa katika morali ya ushindi , waliandika bao la ushindi dakika ya 45 kipindi cha kwanza kupitia kwa mlinzi wake wa pembeni, Hamadi Juma kufuatia mabeki wa Simba kujikoroga.
Matokeo hayo yamepokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa klabu hiyo ambao wanaona kama ligi kuu inawaonea msimu huu.
Hata hivyo Uongozi wa Simba sc kupitia kwa Afisa habari wake, Asha Muhaji umewataka mashabiki na wanachama wao kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu kwao.
“Matokeo ya jana hatukuyatarajia hata kidogo. Tumeshitushwa mno na kipigo hicho. Lakini hayo ndio mambo ya uwanjani. Mpira umechezwa vizuri na tumepoteza. Hatuna budi kuukubali ukweli japo unauma”. Alisema Asha.
Afisa habari huyo aliongeza kuwa kutokana na matokeo wanayozidi kuyapata, yanawapa watu cha kusema, lakini soka huwa lina tabia ya kupanda na kushuka.
“Siku za nyuma mashabiki wetu walikuwa wanatoka na furaha uwanjani. Kwa sasa mambo yamebadilika. Huo ndio Mpira, ukiupenda lazima uwe  na moyo wa kukubaliana na kile kinachotokeo”. Alisema Asha.
Asha alisisitiza kuwa bado wamebakiwa na mechi nne, hivyo mashabiki waendelee kuiunga mkono klabu yao ili iweze kufanya vizuri.
“Mashabiki waliamini benchi la ufundi. Makocha wataangalia wapi tumekosea ili kujipanga upya. Cha msingi tuwe wamoja katika mechi zote”. Alisema Asha.
Baada ya kipigo cha jana, Simba wanaendelea kusalia nafasi ya nne wakiwa na pointi zao 36, huku juu yake wakiwepo Mbeya City katika nafasi ya tatu wajikusanyia pointi 42.
Mbeya City wameonekana kudhamiria kuwa miongoni mwa timu tatu za juu, huku Mnyama Simba akihenyeka nyuma yao.
Wikiendi iliyopita walishinda mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Dar es salaam.
Sady Kipanga ndiye alikuwa shujaa wa mechi hiyo na kuwafanya mashabiki wa Mbeya City kuendelea kuwa na furaha msimu wao wa kwanza katika michuano ya ligi kuu.
Simba Sc wanaonekana kupoteza matumaini kupata nafasi tatu za juu.
Hata katika mchezo wa jana, baadhi ya dakika wachezaji walionekana kutokuwa mchezoni, huku wakishindwa kutumia vyema nafasi walizopata.
Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Croatia, Dravko Logarusic anatakiwa kufanya kazi ya ziada kurudisha morali ya wachezaji wake wanaonekana kukata tamaa.
Kipigo cha jana kimewavuruga zaidi Simba, lakini Loga bado alisema wana matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zilizosalia.
“Ligi ni ngumu msimu huu. Huwezi kuingia uwanjani ukadhani utashinda kirahisi. Timu ndogo zimekuwa zikicheza vizuri na kuzipiga timu kubwa. Kikubwa sisi tutakaa chini na kutafakari wapi kuna tatizo na kulifanyia kazi”. Alisema Loga.
Simba baada ya mechi ya jana amebakiwa na mechi tatu za ugenini na moja ya nyumbani.
Atakutana na Kagera Sugar ugenini mjini, Bukoba. Pia atakuwa mgeni wa Azam na Yanga ingawa  mechi zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine ni dhidi ya Ashanti United katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Mechi dhidi ya Azam fc na Yanga itakuwa ngumu zaidi kwa Simba kwasababu timu hizi zinahitaji matokeo kwa nguvu zote katika harakati zao za kuwania ubingwa.
Pia Kagera Sugar wanapocheza Kaitaba si rahisi kuwafunga, hivyo Loga lazima aandae majeshi yake vizuri.
Mechi na Ashanti United haitakuwa nyepesi pia kwasababu wauza mitumba hao wa Ilala wapo katika harakati za kukwepa kushuka daraja.
Benchi la ufundi la Simba lazima litulize akili kwasababu mechi zilizosalia kwao ni ngumu.

No comments:

Post a Comment