WAKATI ligi kuu soka Tanzania bara inaelekea
ukingoni, huku Azam fc wakipigiwa upatu wa kutwaa taji lao la kwanza tangu
wapande msimu wa 2008/2009, timu za
majeshi zimekumbwa na balaa la kufanya vibaya na kuwashangaza wengi.
Kati ya timu sita (6) za majeshi, maafande wa Ruvu
Shooting pekee ndio wapo katika mikono
salama ya kubakia ligi kuu msimu huu wakifuatiwa kwa mbali na JKT Ruvu.
Ruvu Shooting chini ya kocha Mkenya, Tom Alex Olaba, wapo
nafasi ya 6 baada ya kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 32, wakati
JKT Ruvu ya kocha Fredy Minziro ndio
timu ya jeshi inayofuatia kwa kufanya vizuri.
JKT Ruvu imecheza mechi 23 na kukusanya mzigo wa pointi
28 katika nafasi ya 9 ya msimamo wa ligi kuu.
Timu nyingine nne ambazo ni maafande wa jeshi la
Magereza, Tanzania Prisons, maafande wa
Jeshi la kujenga Taifa wa Mgambo JKT, JKT Oljoro na wanajeshi wa Jeshi la
wananchi, (JWTZ), Rhino Rangers zipo katika mstari mwekundu wa kushuka daraja.
Katika timu zote za jeshi, Rhino Rangers ndio imetia
fora kufanya vibaya baada ya kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 13
mkiani.
Kwa ugumu wa mechi tatu zilizosalia kwa klabu ya Rhino,
ambapo mbili itakuwa nyumbani dhidi ya
Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting, huku moja akisafiri hadi jijini Mbeya kuumana na
Tanzania Prisons, inaonesha wazi kuwa wameipa mkono wa `baibai` ligi kuu
Tanzania bara.
Dhahiri kabisa, wapenzi wa soka mkoani Tabora mwakani wataukosa
uhondo wa mechi za ligi kuu baada ya kuonjeshwa msimu huu.
Timu nyingine ambayo ipo katika hatari zaidi ya
kushuka daraja ni JKT Oljoro ambayo ipo nafasi ya 13 baada ya kushuka dimbani
mara 23 na kujikusanyia pointi 15 tu.
Oljoro wamebakiza mechi tatu za nyumbani dhidi ya
Prisons, Yanga na Mtibwa Sugar.
Mechi hizo zitakuwa ngumu zaidi kutokana na
mazingira ya timu zote, hasa Yanga na Prisons.
Mtibwa hawana cha kupoteza msimu huu kwasababu
hawawezi kutafuta nafasi tatu za juu wala kushuka daraja, hivyo mchezo
hautakuwa na nguvu sana.
Lakini kimbembe ni mechi dhidi ya Yanga ambao ni
washindani wa Azam fc katika mbio za ubingwa mwaka huu.
Mechi dhidi ya Prisons itakuwa ngumu kutokana na
mazingira ya Wajelajela ambao watakuwa wakisaka pointi tatu ili kukwepa mkasi
wa kushuka daraja.
Kwa upande wa Mgambo JKT angalau wamefufua matumaini
ya kubakika ligi kuu baada ya kuwafunga Yanga mabao 2-1 wikiendi iliyopita katika
dimba la CCM Mkwakwani, jijini Tanga.
Sasa Mgambo wapo nafasi ya 11 baada ya kushuka
dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 22, huku juu yake wakiwemo Prisons wenye
pointi 22 kwa kucheza mechi 23, lakini wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga
na kufungwa.
Kwa nafasi waliyopo Mgambo , kama watatumia vizuri
wembe wake uliowanyoa Yanga SC, katika
mechi tatu walizobakiza dhidi ya Coastal Union, Kagera Sugar (zote Mkwakwani)
na Mbeya City uwanja wa sokoine, wanaweza kubakia ligi kuu.
Haitakuwa rahisi kwa Mgambo kushinda Mbeya kwasababu
Mbeya City wanawania nafasi mbili za juu.
Coastal Union na Mtibwa Sugar hawana uwezo wa kutwaa
ubingwa wala kushuka nafasi, hivyo `Presha` ya mechi hizo mbili haitakuwa kubwa
sana.
Kuna timu nyingi za majeshi katika michuano ya ligi
kuu, lakini kupata mafanikio imekuwa ngumu kwao.
Katika mahojiano maalumu na mtandao huu , aliyekuwa
kocha msaidizi wa JKT Oljoro na kutimuliwa
pamoja na bosi wake Mbwana Makata, Mwalimu Riziki Shawa amebainisha baadhi
ya siri za timu za majeshi kufanya vibaya;
Riziki alisema aina ya wachezaji wanaotumiwa na timu
za mejeshi, wengi wao ni wabovu, huku
upatikanaji wa wanandinga hao ikiwa mbovu zaidi.
“Wachezaji ambao ni raia, siku zote wanacheza kwa kujituma. Lakini timu
za majeshi zina sheria zake. Wachezaji wengi wanatoka jeshini bila kujali ubora
wao. Pia wanajeshi wanapata mishahara kwa kazi yao, hivyo wanaridhika na kucheza
mpira bila Malengo”.
“Hata kiutaalum, wachezaji wa jeshi wanatumia nguvu
zaidi badala ya maarifa. Kuwafundisha ni kazi kubwa na wanapokutana na
wachezaji wa kawaida waliojengwa katika mfumo wa soka, wanashindwa kabisa
kucheza vizuri”. Alisema Riziki.
Kocha huyo alitaja sababu nyingine kuwa ni undugu; ambapo baadhi ya wachezaji wanasajiliwa na
wakubwa wa jeshi kwa kujuana bila kuangalia viwango vyao.
“Kuna wachezaji wanaonekana wachezaji, lakini si wachezaji. Utakuta bosi wako
analazimisha mchezaji fulani asajiliwe. Kocha unajua kabisa hana uwezo, inabidi
ukubali ili kulinda kibarua chako”.
“Mimi naweka
bayana, kama wanataka kufanikiwa lazima waheshimu benchi la ufundi. Kumwingilia
kocha katika kazi yake ni kuleta matatizo. Katibu mkuu anataka kuwa kocha,
unaacha kazi kubwa kama hiyo na kutaka
kuwa kocha wakati hana taaluma”. Alifafanua Riziki.
Riziki aliendelea kumwaga siri za timu za jeshi na
kusema sababu nyingine ni kukataliwa kwa mapendekezo ya makocha.
“Kocha unapendekeza wachezaji, lakini wanakataa. Sisi makocha, ligi inapoendelea tunaona wachezaji wa
kuwasajili, unapopeleka majina, wao
wanakataa. Utakuta siku zinaenda na hujapata wachezaji. Unapoanza kambi
wachezaji wanajituma, lakini unakuwa umechelewa”.
“Kuna wakati unaweza kuletewa wachezaji ishirini wa
jeshi, katikati orodha hiyo unakuta wazuri ni kumi tu. Na wewe umepewa nafasi
ya kutafuta wachezaji watano, sasa unawezaje kufanya mambo kwa wakati wakati
wanakataa baadhi ya mapendekezo”. Aliongeza Riziki.
Pia alitaja sababu nyingine kuwa ni utovu wa nidhamu
kwa baadhi ya wachezaji wengi wa jeshi.
“Ukiwapa mapumziko ya miezi miwili, utakuta
wanafanya mambo ya ajabu akiwemo ulevi na kujihusisha na mambo ya ngono.
Wanapoteza nguvu nyingi na wakirudi wanakuwa wabovu kupita maelezo”.
Alibainisha Riziki.
Akizungumzia kufukuzwa kwa makocha katika timu za
majeshi, Riziki alisema viongozi wengi
wa juu jeshini hawajui mpira na wanadhani unachezwa tu bila kanuni na kujali
wachezaji kimaslahi.
“Unapokuwa mwalimu unakuwa na msimamo wako. Sasa
jeshini mambo mengi ni amri, unapopinga tu waliyoamua unakuwa huna chako”.
“Kuna makundi mawili ya wachezaji, wapo wanajeshi na
raia. Ifikapo mwisho wa mwezi, wachezaji wa jeshi wanalipwa mishahara yao na
raia wanayumbishwa. Sisi walimu tunajua umuhimu wa kumlipa posho na mshahara
mchezaji. Lakini ukihoji unaonekana mbaya”.
“Utakuta mchezaji anapata mshahara tarehe 15 ya
mwezi mwingine, ukizingatia ana familia nyumbani. Muda mwingi anakuwa na
mawazo, lakini unapohoji unaonekana jeuri. Sasa kuna mpira gani hapo?”. Alihoji
Riziki.
Pia kocha huyo aligusia suala la ripoti ya benchi la
ufundi baada ya msimu kuisha ambapo alisema makocha wanaandaa ripoti yao na
kueleza wazi kuwa wachezaji kadhaa wameshuka kiwango, lakini kwakuwa viongozi
wa juu ndio waliofanya mpango wa kuwasajili kwa undugu, wanalazimika kuwalinda.
“Unawapa ripoti wanaikalia. Wanaanza kuwaza kutafuta
mwalimu mwingine kwasababu wakikubali mapendekezo yenu, wachezaji wao
wataondolewa”
Kocha huyo
alimalizia kwa kuwaasa viongozi wa jeshi, maofisi wa jeshi kuwaacha makocha
wafanye kazi yao kama wanataka kufanikiwa.
Lakini kama
wataendelea kwa mfumo huo na kukumbatia madhaifu haya, watabakia kuwa wa kupanda
na kushuka daraja.
No comments:
Post a Comment