Search This Blog

Tuesday, February 11, 2014

WATANZANIA HATUJACHELEWA KUFAHAMU NAMNA MAJUKUMU YA MABEKI WA PEMBENI YALIVYOBADILIKA......


Siku za karibuni nimekuwa nikifuatilia mechi za ligi kuu ya Vodacom hapa nchini, miongoni mwa maeneo ambayo baada ya kufuatilia kwa muda mrefu sasa nimegundua yanahitaji sana maboresho ni sehemu ya mabeki wa pembeni.

Kutokana na mabadiliko makubwa ya namna ya uchezaji siku hizi, imepelekea pia majukumu ya wachezaji kiwanjani kubadilika kutokana na mahitaji ya kisasa tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzoni. Juzi nilikuwepo kwenye uwanja wa Chamazi kuwashuhudia wawakilishi wetu Azam FC kwenye kombe la shirikisho walipokuwa wanacheza na timu ya Feroviarrio kutoka kule Beira nchini Msumbiji.
Pamoja na Azam kupata ushindi wa bao 1-0 niligundua mabeki wa pembeni Malika Ndeule na Erasto Nyoni kama wangecheza kama ambavyo mahitaji ya mchezo wa kileo yanavyowataka wabeki wa pembeni kucheza basi Azam wangeweza walau kupata ushindi zaidi ya walioupata ama kwenye mechi ya marudiano wakirekebisha hayo mapungufu basi watakuwa na nafasi ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo.


Katika kuelezea jukumu la beki wa aidha upande wa kushoto au kulia, kazi yao kubwa ni kulinda goli lao kwenye pembe za uwanja, wakiwazuia wachezaji wa timu pinzani kuingiza mipira ndani ya eneo lao penati na kuleta madhara.

 Jukumu lao la pili, pia wanatakiwa kusaidia timu wakati wa kushambulia. 

Mwanzoni, mabeki wa pembeni walikuwa wagumu na kuaminika sana, jukumu kubwa na la pekee lilikuwa kusimamia ulinzi zaidi, lakini siku hizi timu nyingi zimekuwa na mabeki wa pembeni ambao wamekuwa wasaidizi wazuri wa mashambulizi ya timu zao kutokea pembeni.  

Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita majukumu ya mabeki wa pembeni yamebadilika. Hivi sasa, timu nyingi bado zinacheza na mabeki wazuri wa pembeni ambao wanaweza kuzuia vizuri pamoja na kushambulia, mfumo wa siku hizi mabeki wa kati wanajipanga kucheza pembeni kuhakikisha wanakuwa na mstari mzuri wa ulinzi. Lakini hii staili haipo kwa timu ambazo zina uwezo mdogo wa kumiliki mpira, ambazo muda mwingi wa mchezo zinakuwa zinazuia mashambulizi, hivyo zinakuwa hazihitaji mabeki wao wa pembeni kwenda mbele kushambulia - staili hii inaweza kuonekana sio nzuri hasa kwa sababu inaacha mstari wa ulinzi hasa kati kati kuwa wazi wakati timu inapopoteza mpira.

Jukumu la beki wa pembeni wa kisasa kwa ujumla kwenye timu inayocheza soka la kushambulia na kwa timu inayocheza soka kwa kumiliki zaidi mpira, ni kujenga mashambulizi kuanzia nyuima.

Jukumu la beki wa pembeni limebadilika hasa wakati timu zilipoamua kucheza kwa kumiliki zaidi mpira, hasa katika ligi kama ya Hispania ambapo timu zinajaza viungo kati kujaribu kuimiliki zaidi mechi.  
Mabeki wa pembeni ndio wanategemewa zaidi kuipeleka timu mbele kwa sababu mara nyingi ndio wachezaji wanaokuwa na nafasi kubwa uwanjani kwa sababu katikati mwa uwanja kunakuwa kumejaa wachezaji wengi. Kwa timu kuweza kufaidika na mfumo huu, mabeki wa pembeni inabidi wawe fiti vya kutosha ili waweze kushambulia kutokea pembeni na kuwahi kurudi wakati timu yao inashambuliwa. 
 Matokeo ya mfumo huu timu nyingi zimeacha kuweka umuhimu wa kutumia mawinga asilia. Kwa timu ambazo hazichezi na mawinga asilia, mabeki wa pembeni ndio hutumika kama mawinga na mabeki kwa wakati mmoja. 
 AC Milan wamekuwa maarufu kwa miaka kadhaa sasa kwa kucheza bila mawinga asilia na wakiwa na mabeki wanaoshambulia. Kasi na nguvu ndio vitu muhimu kwa mabeki wa pembeni wa kisasa kwa sababu watakuwa wanakimbia eneo kubwa ikiwa watakuwa wanaifanya vizuri kazi yao.

Kutokana na sifa hizi anazotakiwa kuwa nazo beki wa pembeni wa kisasa, ndio maana sio jambo la kushangaza kuona kuna wachezaji wachache wanaoweza kucheza kwenye nafasi hizo ukifananisha na sehemu nyingine dimbani. 
Mabeki wengi wa pembeni wa kisasa waliwahi kuwa wachezaji wa kushambulia ambao walirudishwa nyuma kucheza kama mabeki wa pembeni. Mfano mzuri ni wachezaji kama Ashley Cole, Patrice Evra, Daniel Alves na Zambrotta.  Jukumu la beki wa pembeni limekuwa kubwa kiasi kwamba katika michezo mikubwa na muhimu, timu nyingi zimekuwa zikijaribu kuzuia kipekee mbio za mabeki wa pembeni, huku timu nyingine zikitoa uhuru wa kushambulia kwa mabeki wao. Kwa mfano, barani ulaya  Manchester United inapendelea kucheza na mawinga wazuiaji kama vile Antonio Valencia na hata Park alitumika hivyo hivyo, hii ilikuwa kuweza kurudi na kusaidia kuzuia mashambulizi ya wachezaji wa pembeni wa timu pinzani. 
Daniel Alves ni mfano wa beki wa pembeni ambaye timu inajipanga kwa mtindo wa kipekee ili kuweka mfumo unaomfaa yeye na uchezaji wake. Ni mzuri sana katika kushambulia, na kasi na nguvu - akiongeza mashambulizi ya Barca kutokea upande wa kulia, hivyo mara nyingi Barcelona kucheza wachezaji watatu mbele (hasa upande wa kulia) ili kwenda sawa na aina ya uchezaji wake.  Hii haiwapi shida Barcelona kwa sababu muda mwingi wa mchezo wanakuwa na mpira wao; hii inamfanya Alves kuwa na faida sana kwenye mashambulizi ya timu. 
Hii staili ya uchezaji timu nyingi bado hazijaimudu na ni vigumu kuweza kuitumia katika siku za hivi karibuni, lakini kutokana na kuongezeka kwa umuhimu wa mabeki wa pembeni leo hii, jukumu hili la mabeki wa pembeni litazidi kuendelea kuboreka na litakuwa jambo la kawaida kiasi kwamba timu zitakuwa zikipanga mbinu za kuzuia mashambulizi ya mabeki wa pembeni zaidi ili kuweza kudhibiti mchango wao katika timu zao kuliko ilivyo hivi sasa. 

No comments:

Post a Comment