Na Oscar Oscar Jr
Wamempiga Spurs kwenye EPL nje na ndani kwa uwiano wa mabao 11-1.Arsenal alikula 6-3, Norwich city 7-0, Man U
4-1. Manuel Pellegrini ameufanya uwanja wa ETIHAD kuwa kama uwanja wa TENNIS!
Shukrani za dhati zimuendee Injinia Manuel Pellegrini kwa kuleta nidhamu nje na ndani ya uwanja. Utawala wa Roberto Manchini ulikuwa na mafanikio sana kwenye Media kuliko uwanjani ingawa lazima nimpe heshima yake kwa kuwapa taji la EPL ambalo walilisubiri kwa zaidi ya miaka 40 na asante pia kwa taji la FA.
Tulizoea kusikia leo Roberto Manchini amezichapa na Mario Baloteli mazoezini, kesho amekamatana mashati na Carlos Tevez n.k stori za aina hii kwenye utawala wa Pellegrini ni "past tense". Benchi alilompiga Joe Hart baada ya kipa huyo kucheza "Kikaseja" lilikuwa ni somo tosha na kwa sasa, Hart amerejea kwenye kiwango bora kabisa.
Fernandinho na Yaya Toure tayari wamefunga mabao 15 ya EPL wakitokea sehemu ya kiungo. Kun Aguero, Negredo na Dzeko wameshatumbukia kwenye nyavu za Epl mara 43. Man city sio kwamba wanafunga tu magoli, Pellegrini amewafanya waburudishe pia. Nitakosea kama nitaacha kummwagia sifa Jose Mourinho na Chelsea kwa kumuadabisha Pellegrini aliyeshindikana ndani ya Etihad.
Samir Nasri chini ya Pellegrini anaonyesha alikuwa anarudi kwenye kiwango chake bora kabisa lakini majeruhi yameendelea kumuweka nje. Alvaro Negredo na Dzecko wanapasia kamba kila inapoitwa weekend lakini kumkosa Aguero ni pengo kubwa kwenye kikosi cha Pellegrini. Aguero hafungi tu, anakaba, anatengeneza nafasi na hatuliii sehemu moja kama sanamu la Posta na hii ndo tofauti kubwa ya Kun na wengine.
Eneo pekee ambalo sipendi kuona Man city ikipatwa na tatizo, ni kiungo anapocheza Yaya Toure "Fahari ya Afrika" na Fernandinho. Yaya Toure tayari amefunga goli 12 za EPL na kupika mengine 4, ni Boss wa mipira iliyokufa pale Etihad. Fernandinho pamoja na kuwa anagoli 3 tu, jamaa ndo anayefanya gari litembee.
Najua kama kuna Javi Garcia, James Milner na Jack Rodwell lakini, sio mbadala halisi wa Yaya na Fernandinho. Kukosekana kwa Fernandinho kwenye mechi yao na Chelsea, hili limejidhihirisha.
Kipigo toka kwa Sunderland na kile cha Cardiff ambavyo pengine sio rahisi kudhani kama Man city anaweza kupoteza ingawa mpira wa miguu hauna mwenyewe, viliwadhoofisha sana. Pellegini bado hapati matokeo mazuri anapocheza nje ya Etihad lakini ukweli utabaki pale pale, Man city ya Pellegrini inafanya vizuri uwanjani kuliko ya Roberto Manchini ambayo kutwa ilikuwa kwenye vyombo vya habari kwa stori za nje ya uwanja.
All in All, Man city chini ya Pellegrini endapo watachukuwa mataji yote manne FA, UCL, CAPITAL ONE CUP na lile la EPL binafsi siwezi kushangaa, wanakikosi kikubwa na chenye ubora na uzoefu ingawa kwenye UCL ni lazima niwaheshimu Bavarians, Madrid, Barcelona na Man united kama timu bora Ulaya.
Kila la kheri Pellegrini.
No comments:
Post a Comment