Search This Blog

Wednesday, February 19, 2014

MAKALA: SIMBA WAICHEZESHE TIMU YAO KWA MAHITAJI YA TAMBWE....

Na Baraka Mbolembole

Simba SC, imeshindwa kupata matokeo ya ushindi katika michezo mitatu ya hivi karibuni. sitazungumzia matokeo hayo, bali kwa muda sasa nimekuwa nikiamini kuwa timu hiyo inakosa mambo muhimu kikosini.
 Inawezekana kocha, Logarusic na msaadizi wake, Suleiman Matola wakawa pia wameyaona makosa mengi, ila kosa ambalo linawanyima matokeo kwa sasa, ni timu hiyo kucheza bila kuwa na utambuzi wa yupi mchezaji hatari zaidi katika timu yao.
 Je, mpira ukiwa katikati ya uwanja wacheze kwa kumpatia nani ambaye atapiga pasi sahihi ya mwisho, na pasi hiyo atampigia mchezaji gani. Je, makocha hawatoi maelekezo kwa wachezaji
wao muhimu? Ama labda wachezaji wanasahau majukumu yao muhimu
wanapokuwa uwanjani?.


Kwa timu ya Simba, naweza kusema kuwa endapo timu itakuwa inacheza kwa mtindo wa kumzunguka mshambuliaji wao, Amis Tambwe bila shaka yoyote wanaweza kufunga mabao yasiyopungua mawili katika kila mechi. Tambwe ni mshambuliaji wa hatari anapokuwa ndani ya mita 18.


KUMZUNGUKA KWA MAANA GANI...?.
Ni kucheza huku wakijua kuwa wanaye mchezaji ambaye akipata nafasi mbili, anafunga moja, ama zote kabisa. Simba walikuwa na tatizo la kukosa mshambuliaji-mfungaji kwa misimu kadhaa iliyopita, ila mabao 15 katika michezo 17 ambayo mshambuliaji huyo raia wa Burundi amekwishacheza hadi sasa katika msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu ni kigezo tosha kuwa timu hiyo kwa sasa ina
mfungaji wa kutisha. 
Tambwe ni mpigaji mzuri wa mipira ya kichwa, hivyo kama Simba wataamua kucheza kwa mtindo wa krosi wanaweza kufunga mabao ya kutosha, kwa kuwa walinzi wengi nchini si wazuri kwa
kuondosha na kuicheza mipira ya krosi, au kona. 
Wakati fulani, timu hiyo ilipokuwa na Emmanuel Gabriel, ambaye alikuwa mtaalamu wa kupiga
vichwa, kiungo wa pembeni wa timu hiyo, Steven Mapunda alijua namna ya kumchezesha, ' Emma', Said Sued, Ramadhani Ramadhani, katika sehemu za ulinzi wa pembeni, na hata baadae, Nurdin Bakari na Soud Abdallah, walikuwa wakipanda mbele na kupiga krosi kwa mtu maalumu tu, Emma.

Wakati, Tambwe akionekana mzuri katika mipira ya vichwa, mchezaji huyo pia ni mzuri katika kujipanga wakati timu ikicheza mpira wa pasi. Ni mmaliziaji mzuri na mwenye umakini mkubwa hivyo Simba wanaweza kujipanga na kutazama ni nani hasa katika kikosi chao anaweza kumchezesha mfungaji huyo na kumpatia mipira sahihi. Je, Simba wanaye kiungo mwenye uwezo wa kupiga pasi za kupenyeza? 
Wanaye Henrry Joseph ambaye katikla mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City alicheza katika nafasi ya ulinzi wa kushoto. Joseph anaweza kutoa mchango mkubwa kwa Simba kama ataendelea kupandisha kiwango chake katika michezo iliyosalia. Ni mchezaji ambaye ana uwezo mkubwa wa kutuliza akili yake na kutoa pasi, katika mchezo dhidi ya City alionekana kupiga pasi zenye macho ili nyingi zilikosa nguvu na kutofika kwa walengwa, hiyo ni dalili kuwa mchezaji huyo hayupo fiti vya kutosha.


Said Ndemla alipiga pasi mbili za hatari kwa muda wote aliokuwepo mchezoni na pasi moja ilizaa bao la kusawazisha. Kama, Joseph atapandisha kiwango chake na kurudishwa katika nafasi ya kiungo wa kati sambamba na Jonas Mkude, Simba itaweza kunufaika zaidi na Tambwe kwa kuwa ni mchezaji asiyetaka masihara. Ni mviziaji mzuri, na mtumiaji mzuri wa nafasi anazotengenezewa.


KUJITUMAKatika siku ambazo nilishuhudia kujituma kwa wachezaji wa kigeni, ni siku ya mchezo wa City na Simba. Wachezaji, Yaw Berko, Donald Mosoti, Joseph Owino na Tambwe walicheza kwa viwango vya juu katika mchezo huo. Walijituma vya kutosha na walijaribu kutulia hata pale wachezaji wenzao walipochanganywa na bao la kuongoza la City. Walijituma sana na walionesha kuwa hitaji lao lilikuwa ni ushindi tu. Wapo pia wachezaji wa ndani waliocheza kwa moyo wa kujituma, ila wachezaji kama Ramadhani Singano, na Harouna Chanongo walionekana kupagawa na matokeo yake wakajikuta wakicheza kwa viwango vya kawaida kwa kuwa walipaniki mara baada ya mwamuzi kutoa mkwaju wa penati kwa City.

Kama, Singano atakuwa akicheza huku akituliza kichwa chake zaidi anaweza kuibuka mtengenezaji bora wa mabao ya Simba kwa kuwa amekuwa na uwezo mkubwa wa kuwalazimisha walinzi wa timu pinzani kurudi nyuma. Akituliza akili na kutazama mtu wa kumpasia Simba itafunga sana kwa kuwa Tambwe ni mchezaji anayeweza kuwapoteza ' maboya' walinzi wa timu pinzani. Simba icheze kwa kutambua mahitaji ya Amis Tambwe, wachezaji wacheze wakitambua kuwa wanaye mchezaji wa hatari katika timu yao. Wakubali kucheza kwa kumtegemea Tambwe huku wachezaji wengine wakijitahidi kufunga mabao muhimu ikiwa mchezajio huyo atabanwa. Soka linachezwa kwa kuheshimiana bwana, ni lazima wachezaji wajitambue na kutambua majukumu yao uwanjani.
0714 08 43 08

2 comments:

  1. Siku nyingine brother, uwage unatoa pia makala zinazoihusu YANGA, AZAM, MTIBWA n.k

    ReplyDelete
  2. Hah hah Baraka nimeipenda sentensi yako kuwa Hata Pale Mwamuzi alipotoa Penalti kwa City!!!!!! Halafu unategemea tukuamini katika uchambuzi wako? Acha mapenzi Yasiyo na Tija Bro!

    ReplyDelete