TIMU ya wasichana ya Tanzania
imekabidhiwa zawadi ya Sh milioni 16 baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya
vijana walio chini ya umri wa miaka 17 ya Kimataifa ya Airtel Rising Stars iliyofanyika
Septemba mwaka jana nchini Nigeria.
Timu hiyo ilitwaa taji hilo baada ya
kuifunga Kenya bao 1-0 lililofungwa na Donisia Daniel katika fainali hiyo.
Akipokea fedha hizo jana (Februari 10,
2014) Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Msanifu
Kondo alisema wanaishukuru Kampuni ya Airtel kwa kutimiza ahadi yao ya zawadi
ya fedha hizo na tayari wamezikabidhi kwa makocha na wachezaji wa timu hiyo.
Alisema kila mchezaji amepewa Sh
850,000 wakati kocha mkuu wa timu hiyo Rogasian Kaijage amepewa Sh milioni moja
na laki mbili na kocha msaidizi amepewa Sh milioni moja.
“Tunawashukuru Airtel kwa kutoa
fedha hizo za zawadi kwa timu hii na sisi tumewakabidhi wahusika,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa
Airtel Tanzania Jane Matinde alisema wao kama wadhamini wa mashindano hayo
wametimiza ahadi yao kwa kukabidhi fedha hizo kwa mabingwa hao.
“Kwa niaba ya Airtel Tanzania
tunaipongeza timu ya wasichana ya Tanzania kwa kutwaa ubingwa huo, lakini pia
tumetekeleza ahadi yetu ya kukabidhi zawadi, kama mnavyofahamu kampuni yetu
imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia mambo ya kijamii lakini pia michezo
ikiwemo soka kupitia michuano ya vijana ya Airtel Rising Stars kwa kushiriki na
klabu ya Manchester United,” alisema.
No comments:
Post a Comment