Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
NGWE ya lala salama ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 unatarajia kuanza kushika kasi januari 25 mwakani.
Kwasasa timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo zipo katika maandalizi ya vikosi vyao ili kufanya vizuri zaidi ya mzunguko wa kwanza.
Wataalamu wengi wa soka wanasema mzunguko wa pili kama ilivyo kawaida timu zinajigawa katika makundi matatu.
Kundi la kwanza linajumuisha timu zinazowania ubingwa, wakati kundi la pili ni lile la timu zinazowania nafasi za katikati ambazo si nzuri sana wala mbaya sana, cha msingi katika nafasi hizi, timu zinakuwa katika mikono salama.
Kundi la tatu ndio balaa, hapo kunakuwepo na timu zinazopigana kushuka daraja, hivyo zinashindana kwa nguvu zote kusaka ushindi wa kuwasogeza mbele.
Ukiangalia msimamo wa ligi kuu mpaka sasa wakati tunasubiri mzunguko wa pili, timu za kundi la kwanza unaweza kusema ni Vinara Yanga, Azam fc, Mbeya City, pamoja na Simba sc.
Simaanishi nyingine haziwezi kuingia katika nafasi hizo. Mpira wa miguu ni mchezo wa hadharani, hivyo baadhi ya timu zikiwemo Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, na Ruvu Shooting zinaweza kuingia katika mbio za kuwania ubingwa endapo zitachanga vyema karata zao.
Msimamo uko hivi; Yanga wapo kileleni kwa pointi 28, nafasi ya pili wapo Azam fc na pointi zao 27, nafasi ya tatu wapo Mbeya City wakijikusanyia pointi 27, huku nafasi ya nne ikishikiliwa na simba SC yenye pointi 24. Timu hizi zinakamilisha timu nne za juu `Big Four` wakati mzunguko wa pili unasubiriwa.
Nafasi ya tano inakaliwa na Mtibwa sugar wenye pointi 20, sawa na Kagera Sugar katika nafasi ya sita, lakini Mtibwa wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Nafasi ya saba wapo Ruvu shooting wakiwa na pointi 17, wakati nafasi ya nne inashikiliwa na wagosi wa kaya, Coastal Union kwa pointi 16, nafasi ya tisa wapo JKT Ruvu na pointi zao 15, huku nafasi ya kumi ikishikiliwa na Rhino Rangers ya Tabora yenye pointi 11.
Kibarua kipo nafasi nne za mwisho ambapo JKT Oljoro wameshikilia nafasi ya 11 kwa pointi 10 sawa na Ashanti United nafasi ya 12, tofauti ni wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Nafasi ya 13 wapo Tanzania prisons wakiwa na pointi 9, huku Mgambo JKT waikiburuza mkia kwa pointi 6 tu.
Kwa msimamo huu utagundua kuwa nafasi za juu zinaonekana kung`ang`aniwa na timu za Yanga, Azam fc, Mbeya City pamoja na Simba sc. Lakini Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Ruvu Shooting zinaweza kuingia katika kinyang`anyiro cha ubingwa. Sio hizo tu, hata timu nyingine kama Coastal union, Ruvu Stars zinaweza kupanda juu kutegemeana na matokeo ya timu zilizopo mbele yao.
Mzunguko wa pili utakuwa na ushindani mkubwa sana kwa timu zinazowania ubingwa. Ukiangalia hali zao kiuchumi, morali kubwa, ubora wa wachezaji, mipango yao na makocha waliopo, utagundua kuwa kibarua kitakuwa kizito.
Kwa kifupi tuangalie baadhi ya mabadiliko yaliyopo katika timu nne za juu na maandalizi yao kuelekea mzunguko wa pili.
YANGA SC
Timu hii ipo katika maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu pamoja na michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika mwakani.
Kwa bahati Mbaya kumetokea mabadiliko ya benchi la ufundi ambapo Uongozi wa klabu ya Young Africans SC umempatia taarifa (Notice) ya siku ya thelathini (30) kocha mkuu mholanzi Ernie Brandts juu ya kusitisha mkataba wake kuanzia Disemba 22 mwaka huu.
Kwa maana hiyo, Yanga wanahaha kupata kocha mpya kuelekea mzunguko wa pili. Ukipiga hesabu za muda uliobakia kufikia januari 25 na februari ambapo wataanza kampeni za ligi ya mabingwa barani Afrika, utagundua kuwa kocha mpya atakuwa na kazi nzito kuandaa kikosi, na mbaya zaidi akija na falasafa mpya ya uchezaji.
Lengo sio kuingia kiundani zaidi kuhusu suala hili la kumfukuza kocha ambalo yawezekana ni udhaifu wa viongozi wa Yanga au ni uhalisia wa jinsi kiwango cha timu yao kinavyoshuka siku hadi siku licha ya kusheheni nyota kibao.
Yanga kwasasa wapo chini ya kocha msaidizi, Fredy Felix Minziro na wanajiandaa kwenda kushiriki michuano ya kombe la Mapinduzi inayotarajia kuanza kushika kasi januari mosi mwakani katika uwanja wa Amaan mjini Unguja na Gombani kisiwani Pemba.
Michuano hii itakuwa muhimu sana kwa Yanga, kwani itawapa nafasi ya kupima uwezo wa kikosi chao kabla ya kuanza kutetea ubingwa wake na kushiriki michuano ya kimataifa.
Kuna uongezeka la wachezaji wapya katika kikosi chake, hivyo unaweza kukubaliana na mimi kuwa kutakuwa na mabadiliko ukilinganisha na mzunguko wa kwanza, lakini endapo atapatikana kocha mwenye ubora wa juu.
Ongezeko la Juma Kaseja, Hassan Dilunga na Emmanuel Anord Okwi, yawezekana kutawapatia nguvu kubwa zaidi na kuendelea kufanya vizuri.
Kaseja ana uzoefu mkubwa sana na ligi kuu pamoja na michuano ya kimataifa. Okwi naye ni mchezaji bora kwa wakati wote, lakini Dilunga ni chipukizi na anahitaji muda zaidi wa kujiweka sawa katika soka la ushindani.
Kwa usajili wa Okwi, Yanga inafikisha wachezaji watano wa kimataifa, wengine ni Mbuyu Twite, Didier Kavumbagu, Haruna Niyonzima na Hamis Friday Kiiza. Wachezaji hawa wapo katika kiwango kizuri, ingawa bado wameonekana kutokuwa na makali barabara.
Pia imesheheni wachezaji wazawa wenye kiwango cha juu ambao ni pamoja na Juma Kaseja, David Luhende, Nadir Haroub `Canavaro`, Kelvi Yondan `Vidic`, Athuman Idd `Chuji`, Frank Domayo, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa , kipa Ally Mustapha `Bartez`, Deo Munish `Dida` na wengineo.
Ukiangalia majina ya wachezaji wa Yanga kulinganisha na timu nyingine kama Mbeya City, Ruvu Shooting hata Simba Sc, unaweza kuamini kwa asilimia mia moja kuwa Yanga watashinda mechi zote.
Hakika hakuna ushindani wa majina kabisa, Yanga wanaonekana kuwa na kila aina ya mchezaji, lakini kumbuka mpira wa miguu ni mchezo wa mipango na unachezwa hadharani na ndio maana wakiwa na wachezaji wao bora, walifungwa mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba yenye wachezaji wengi vijana.
Kwa kikosi cha Yanga, anahitajika kocha wa kuunganisha timu ili wacheze kitimu. Kama atapatikana mwalimu mzuri, bila shaka Yanga watafanya vizuri ngwe ya pili nap engine kutetea ubingwa wao. Cha msingi tusubiri muda ufike.
SIMBA SC
Simba wakiwa chini ya kocha Abdallah Kibadeni walianza mzunguko wa kwanza vizuri na kuongoza, japokuwa walikuja kupoteza mwelekeo na kuishia nafasi ya nne.
Waliamua kufanya mabadaliko ya benchi la Ufundi ambapo Kibadeni pamoja na msaidizi wake, Jamhuri Kiwhelo walitimuliwa na mikoba yao kuchukuliwa na Mcroatia Zdravko Logarusic `Loga` akisaidiwa na Seleman Matola `Veron`.
Mbali na kubadili benchi la ufundi, pia wameongeza nguvu katika dirisha dogo ambapo wamewasajili, Ivo Mapunda, Yaw Berko, Donald Mosoti, Awadh Juma Issa, Ali Badru pamoja na kumrejesha Uhuru Seleman Mwambungu aliyekuwa akicheza kwa mkopo Coastal Union ya Tanga.
Mapunda, Awadh, Mosoti, Uhuru, walicheza mechi ya nani mtani Jembe ambapo waliunganisha nguvu zao na wachezaji wengine wakiwemo, Gerrard Jonas Mkude, Ramadhan Singano `Messi`, Said Ndemla, Betram Mwombeki, Hamis Tambwe, Joseph Owino Gella na wengine.
Katika mechi hiyo, Simba ilicheza vizuri na kuonekana kuimarika. Na sasa inajiwinda na mashindano ya mapinduzi yanayotarajia kuanza kushika kasi januari mosi.
Endapo Simba watatulia na kocha wao na kuongeza nguvu zaidi ya mechi ya Nani Mtani Jembe, basi hapana shaka watarudi mchezoni na kuendelea kutafuta ubingwa wa ligi kuu, ikizingatiwa wanazidiwa pointi nne tu na Yanga waliopo kileleni.
AZAM FC
Klabu hii imeachana na kocha wake , Mwingereza Sterwart John Hall na kuanza maisha mapya na kocha raia wa Cameroon, Joseph Marius Omog.
Wanakwenda Zanzibar kutetea ubingwa wao wa kombe la Mapinduzi. Pia watatumia michuano hiyo kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu bara pamoja na michuano ya kombe la shirikisho mwakani.
Katika dirisha dogo la usajili, Azam fc wamemuongeza mshambuliaji mmoja kutoka Ivory Coast, Mouhamed Kone.
Bila shaka baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, benchi la ufundi lilijiridhisha na uwezo wa wachezaji wake kikosini.
Klabu hii yenye makazi yake Mbande, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, imekuwa ikishindana kwa misimu mitatu mfululizo.
Msimu wa 2011/2012 walikuwa wanashindana na Simba katika mbio za ubingwa na kujikuta wakiambulia nafasi ya pili. Msimu wa 2012/2013, Simba wakajitoa, kibarua kikabaki kwa Azam fc na Yanga na wakaishia nafasi ya pili.
Msimu huu wapo katika mbio za ubingwa, Simba wapo nyuma yao, wanapambana na Yanga pamoja na Mbeya City.
Ukiangalia mfululizo wa kufanya vizuri kwa Azam, japokuwa hawajafanikiwa kutwaa ubingwa, utajiridhisha kuwa wamekuwa wapambanaji wa kweli na bila shaka wataendelea na kasi yao chini ya kocha mpya, Omog.
Yanapotokea mabadiliko ya kocha, kuna mambo mawili; Moja, timu inaweza kuongeza kiwango na pili inaweza kupoteana endapo wachezaji watashindwa kuenda sambamba na falsafa ya mwalimu.
Kwasasa ni mapema kuwatabiria lolote, tunaamini wanatambua nini cha kufanya na ndio maana wapo katika maandalizi kabambe.
Mzunguko wa pili, Azam fc wanaweza kuendana na kasi ya ushindani.
MBEYA CITY
Hii ni timu ngeni ligi kuu. Msimu huu ni wa kwanza kushiriki michuano hii mikubwa, lakini wameonesha ukomavu mkubwa na kuleta changamoto kali mzunguko wa kwanza.
Hakuna timu yoyote iliyoweza kupata pointi tatu mbele ya Mbeya City chini ya kocha wake Mzalendo, Juma Mwambusi akisaidiwa na Maka Mwalwisyi.
Waliungana kwa dhati na mashabiki wao waliokuwa wanawafuata popote pale wanapoenda. Wachezaji walikuwa na morali kubwa na kuucheza mpira kwa kasi kubwa, umakini na malengo ya ushindi.
Walifanikiwa kushinda nyumbani na ugenini na hivyo kuamsha ari kwa wapenzi wengi wa soka hususani jijini Mbeya.
Kwasasa wapo katika maandalizi ya mzunguko wa pili na bahati nzuri wamepata nafasi ya kucheza mapinduzi Cup kwa mara ya kwanza.
Hii itawajenga zaidi kwani watakutana na mazingira tofauti na bara. Watacheza na timu za Zanzibar pamoja na timu za Kenya na Uganda.
Itakuwa nafasi nzuri kwao kujipima uwezo wao kuelekea mzunguko wa pili ligi kuu bara.
Cha kufurahisha hakuna mabadiliko ya kikosi chao, lakini wamemuongeza mchezaji mmoja tu ambaye ni Saad Kipanga.
Ni ngumu kusema Mbeya City wataendeleza makali yao, lakini inawezekana kutegemeana na maandalizi yao, motisha kwa wachezaji na mipango ya ndani na nje ya uwanja.
Lakini bado nawatabiria kufanya vizuri kutokana na kusheheni wachezaji wenye kasi kama Deus Kaseke, Mwagane Yeya, Paul Nonga, Peter Richard, Jeremiah John, Alex Seth na wengine wengi.
Ni suala la kusubiri muda ufike ili tuone maujanja yao. Pia mapinduzi itaonesha wazi kama wana mwelekeo japokuwa itakuwa sehemu ya kujaribu kikosi chao.
Kukutana na timu za Tusker, AFC Leopard, KCC na URA itakuwa changamoto nzuri sana achilia mbali Simba, Yanga na Azam ambazo tayari wameshakutana nazo ligi kuu.
Baada ya kuangalia timu nne za juu, kwa nafasi za katikati huwa hazina ushindani sana kwani timu hzi huwa zinakuwa na uhakika wa kubakika ligi kuu kwa msimu unaofuata.
Timu nyingine kama ilivyo kwa timu za juu, zimefanya usajili katika dirisha dogo kama ifuatavyo;
ASHANTI UNITED
Ndiyo inayoongoza kwa wachezaji 15 ambao ni Kassim Kilungo, Mohamed Banka, Bright Obinna, Victor Costa, Juma Mpongo, Juma Jabu, Ally Kondo, Shafii Rajab, Mohamed Faki, Abubakar Mtiro, Patrick Mhagama, Ally Kabunda, Hassan Kabuda, Idd Ally na Rahim Abdallah.
RUVU SHOOTING; Ally Khan na Jumanne Khamis,
RHINO RANGERS; David Siame, John Kauzeni, Salum Mamlo, Jingo Seleman, Darlington Enyinna, Rajab Twaha, Godfrey Mobi na Mussa Digubike.
TANZANIA PRISONS; Dennis Liwanda, Godfrey Pastory, Henry Mwalugala, Jamal Salum na Brayton Mponzi.
OLJORO JKT; Jacob Masawe, Mansour Ali, Juma Mohamed, Amour Mohamed, Mohamed Ali, Mussa Nahoda, Benedict Ngasa, Seleman Makame, Shija Mkina, Ali Omar na Shaweji
MGAMBO SHOOTING; Suleiman Khatib, Bolly Ajali, Amri Sambinga na Issa Ali.
JKT RUVU; Chacha Marwa, Sino Augustino, Idd Mbaga na Cecil Luambano.
Coastal Union, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar hazijafanya usajili kutokana na kuviamini vikosi vyao.
Timu zote zimeshaanza mipango ya mazoezi, kinachosubiriwa ni muda muafaka kufika.
Kulingana na usajili wa timu hizi, labda tunaweza kupata kitu kipya kutoka kwao, lakini timu zinazoshika nafasi za mwishoni zitakuwa na kibarua kizito zaidi.
Mgambo Jkt, Tanzania Prisons, Ashanti United na JKT Oljoro zinatakiwa kujipanga zaidi ili kuepuka mkasi wa kushuka daraja.
Baadhi ya timu za mkiani, zimeanza harakari za kujinasua na mtego wa kuporomoka daraja, hivyo kwa kuanzia, zimebadili makocha wao.
Prisons imepata kocha mpya David Mwamwaja, Ashanti United, Abdallah Kibadeni, na JKT Oljoro imnasa Hemed Morroco.
Mabadiliko haya yamelenga kuzinusuru timu hizi na tayari zote zimeshaanza mazoezi na kambi kujiwinda na mzunguko wa pili ambao utakuwa wa mapambano ya kufa na kupona.
Tusubiri kuona matunda ya mabadiliko haya, na inawezekana zikaja na sura mpya au zikazidi kwenda shimoni.
No comments:
Post a Comment