USHINDI
wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Oljoro na sare ya mabao 3-3 kati ya Azam FC na Mbeya
City, kwa pamoja vimeifanya klabu ya soka ya Yanga kujikita kileleni mwa Ligi
Kuu ya Bara hadi mwakani mzunguko wa pili utakapoanza.
Yanga
ilikuwa ikicheza na Oljoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeweza
kusogea kutoka nafasi ya tatu iliyokuwa inashika awali hadi nafasi ya kwanza
baada ya kufikisha pointi 28, huku sare ya mabao 3-3 ya Azam na Mbeya City
ikizifanya timu hizo kufikisha pointi 27 kila moja. Timu zote zimecheza mechi
13.
Kwenye
Uwanja wa Taifa, Yanga iliuanza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la
kuongoza dakika ya 23 mfungaji akiwa Simon Msuva aliyeunganisha vyema krosi
safi ya Haruna Niyonzima kutoka wingi ya kulia.
Baada
ya kuingia kwa bao hilo, Oljoro walikuja juu lakini kitendo chao cha kucheza
huku wakitumia nguvu nyingi kutaka kusawazisha kiliwasababishia wachezaji wao
kadhaa kuumia kila mara huku Yanga wakiendelea kushambulia kwa kasi.
Mrisho
Ngassa aliipatia Yanga bao la pili dakika ya 30 kwa shuti kali akiwa nje ya
eneo la 18 la Oljoro ambalo kipa Damas Kugesha hakuweza kulizuia na kuamsha
shangwe kwa mashabiki wa Yanga. Awali Kugesha alidhani Ngassa angetoa pasi mara
baada ya kupokea pasi ya Frank Domayo kutoka katikati ya uwanja.
Mabao
hayo ya Yanga yalidumu hadi mwamuzi Simon Mbelwa wa Pwani anapuliza filimbi ya
kuashiria timu hizo ziende kupumzika. Kabla ya timu hizo kwenda mapumziko,
Oljoro ilifanya mabadiliko kwa wachezaji Yusuph Mchogote na Babu Ally na nafasi
zao kuchukuliwa na Deogratius Peter na Hamisi Saleh.
Kipindi
cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko baada ya kumtoa Hamisi Kiiza na
nafasi yake ikachukuliwa na Jerry Tegete na mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa
Yanga kwani dakika ya 53, Tegete aliipatia Yanga bao la tatu baada ya kupokea
pasi nzuri ya Ngassa.
Ndani
ya kipindi cha pili Oljoro ilifanya badiliko moja kwa kumtoa Sanu Mwaseba na
nafasi yake kuchukuliwa na Amir Omar wakati Yanga waliwatoa Frank Domayo na
Haruna Niyonzima na nafasi zao kuchukuliwa na Reliants Lusajo na Said Bahanuzi.
Mabadiliko
hayo yaliongeza uhai kwa timu zote mbili lakini hadi dakika 90 zinamalizika
hakuna timu iliyoweza kupata bao baada ya mabadiliko hayo kufanywa licha ya
Yanga kukosa mabao kadhaa ya wazi huku Oljoro nao wakifika langoni kwa Yanga
mara chache.
No comments:
Post a Comment