Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Young Africans leo imekamata kiti cha uongozi baada ya kuendeleza wimbi la ushindi mfululizo kwa kuichapa timu ya Maafande wa jeshi la Kujenga Taifa nchini JKT Ruvu kutoka mkoani Pwani kwa mabao 4- 0 mchezo uliofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kikosi cha mholanzi Ernie Brandts kiliingia uwanjani kwa lengo la kuhakikisha kinapata pointi 3 muhimu , jambo ambalo vijana wake walilitekeleza na kuwapa furaha washabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Yanga waliokwepo uwanjani kushuhudia mchezo huo.
Mshambuliaji Mrisho Ngassa aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 3 ya mchezo kwa shuti kali baada ya kuwatoka walinzi wa JKT Ruvu na kumtazama amekaa vipi mlinda mlango wa JKT Ruvu na kuukwamisha mpira wavuni.
Dakika ya 12 ya mchezo, Mrisho Ngassa tena aliwainua vitini mashabiki wa timu ya Young Africans baada ya kumalizia mpira ulipogwa na Saimon Msuva kabla ya kuwababatiza walinzi wa JKT Ruvu na kumkuta mfungaji ambaye aliukwamisha mpira wavuni kwa kichwa.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, JKT Ruvu 0 - 2 Young Africans .
Kipindi cha pili cha mchezo kilianza kwa kasi na Young Africans kupata bao la tatu la mchezo dakika ya 47 kupitia kwa Oscar Joshua ambaye alikutana na mpira uliokolewa walinzi wa JKT na kumkuta mfungaji ambaye alifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na klabu ya Yanga miaka mitatu iliyopita.
Mabadiliko yaliyofanya na kocha mholanzi Ernie Brandts kuwaingiza Reliants Lusajo, Ibrahim Job na Jerson Tegete yaliongeza kasi na uwezo wa kumiliki mchezo kwani waliweza kucheza vizuri na kulilinda lango lao lisipatwe na madhara yoyote.
Dakika ya 89 Jerson Tegete aliipatia Yanga bao la nne la mwisho katika mchezo huo kufuatia migongeo ya Saimon Msuva na Ngassa kabla ya kumkuta Tegete akiwa peke yake na kuukwamisha mpira wavuni.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, JKT Ruvu 0 - 4 Young Africans
Young Africans: 1.Dida, 2.Twite/Job, 3.Oscar, 4.Cannavaro 5.Yondani/Lusajio, 6.Chuji 7.Msuva 8.Domayo, 9.Kavumbagu/Tegete, 10.Ngassa, 11.Kiiza
source: http://www.youngafricans.co.tz
Weka mbali na watoto,hii hatariiii
ReplyDelete