DADA YAKE AJIFUNGUA
MTOTO BAADA YA KIFO CHA METHOD, AMPA JINA METHOD
Muda mfupi baada ya
Method kufariki, dada yake aitwaye Angelina ambaye alikuwa na ujauzito alipatwa
na uchungu na kujifungua salama mtoto wa kiume aliyekuwa na afya njema.
Kabla hajapewa taarifa
za msiba, Angelina alifuatwa nyumbani kwake na kuelezwa kwamba mdogo wake
amezidiwa hivyo anatakiwa aende kumjulia hali, hali hiyo ilimchanganya kidogo
kwani alifahamu fika kwamba yeye si daktari na iweje afuatwe ili aende kumjulia
hali ndugu yake. Alihisi kuna jambo linaloendelea hapo.
“Baada ya kufika maeneo
ya karibu na nyumbani ndipo nilipoona dalili za kuwepo kwa kitu tofauti, Method
alikuwa maarufu hivyo nikaanza kusikia kwamba amefariki hata kabla hatujafika
nyumbani. Nilishtuka sana na kuangua kilio kikubwa sana.
“Kwa kuwa nilikuwa na
ujauzito ambao muda wake wa kujifungua ulikuwa umepitiliza kwa wiki mbili,
palepale nikaanza kuhisi uchungu na haraka nikawahishwa hospitali tayari kwa
kuanza kufuatwa taratibu za kujifungua,” anasema Angelina.
Anasema alipofikishwa
katika hospitali ya TMJ Mikocheni alipewa kitanda na madaktari wakaanza
kumuhudumia lakini ilipofika saa 6 usiku alijifungua salama mtoto wa kiume.
Anasema alimshukuru Mungu hakupata matatizo makubwa wakati wa kujifungua.
Angelina alijifungua
mtoto huyo baada ya kupata mshtuko wa kifo cha mdogo wake ambaye walikuwa
wameshibana vya kutosha hivyo taarifa za kifo chake zilimshtua kiasi cha
kupoteza fahamu.
Wakati ndugu wengine
wakishughulika taratibu za mazishi ya Method, wengine walichukua jukumu la
kumpeleka Angelina hospitali ambako alipofikishwa tu alijifungua mtoto wa
kiume.
MTOTO APEWA JINA LA
METHOD, AHAIDI KUFUATA NYAYO ZA MJOMBA
Kwa kweli ukimtazama
mtoto aliyezaliwa na Angelina anafanana kwa vitu vingi na marehemu Method
lakini uso na rangi ya weupe ndiyo inayothibitisha mfanano huu.
Saa chache baada ya
kujifungua salama mtoto wa kiume, Angelina aliamua kumpa jina la Method mtoto
huyo ambaye pia anatumia jina lingine la Aniceth.
Mama wa mtoto huyo
anasema, amefanya hivyo kwa kumbukumbu ya marehemu mdogo wake ambaye walikuwa
wameshibana sana. “Sikuwa na jinsi kwani niliamua tu kumpa mwanangu jina hilo
kwani nilifahamu kwamba jina hilo litanifanya nimkumbuke ndugu yangu mara kwa
mara,” anasema Angelina.
Dada huyo anasema
hakupata wakati mgumu kuamua jina la mtoto wake kwani hata baba yake
aliliridhia uamuzi huo kwa kumthamini marehemu shemeji yake.
KAULI YA METHOD MTOTO
Kwa sasa anasoma katika
Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) akisomea cheti cha uhasibu na mambo ya bima,
lakini Method Aniceth Theobald anasema anatamani sana kufikia mafanikio ya
mjomba wake ambaye hakuwahi kumuona akicheza soka enzi zake.
“Nataka kucheza soka
kama mjomba alivyokuwa akifanya, sifa zake nimezisikia tu kutoka kwa kaka zangu
ambao waliwahi kumuona pengine akicheza soka. Najipanga kuleta picha mpya ya
mjomba ambayo sasa haipo,” anasema Method.
Method anamudu kucheza
namba nane, tisa na 10 uwanjani na hali ni tofauti kwani mjomba wake alikuwa
akicheza kiungo namba sita wakati mwingi japokuwa alikuwa akipangwa katika
nafasi nyingine pale inapolazimika.
“Mimi sina nguvu nyingi
kuweza kumudu uwezo wa kuwazuia viungo wengi wenye nguvu ndiyo maana
nikashauriwa kucheza namba ambazo hazihitaji kutumi nguvu nyingi zaidi ya akili
ya soka,” anasema Method mdogo ambaye amefanana sura na marehemu Method.
Kwa sasa Method mdogo
ameegemea zaidi katika kutafuta elimu hivyo anapata muda mdogo wa kucheza soka
katika klabu za mtaani kwano japokuwa anasema anaweza kucheza katika timu
nyingine mara tu atakapomaliza masomo yake.
“Mama mara kwa mara
ananishauri kwamba kama ni mpira nitacheza hapo baadaye lakini sasa nikazane
katika elimu ndiyo maana sina timu kubwa ninayochezea japokuwa kuna kipindi
nilikuwa najiiba na kwenda kufanya mazoezi katika kikosi cha timu ay taifa ya
vijana chini ya miaka 17,” anasema Method mdogo.
MARAFIKI ZAKE
WANASEMAJE?
EDIBILY LUNYAMILA…
Edibily Lunyamila si
jina geni katika soka la Tanzania, aliwahi kuvuma akiwa na kikosi cha Yanga
katika miaka ya 1990, na Method alikuwa mshawishi mkubwa wa Lunyamila
kusajiliwa na Yanga mwaka 1993 akitokea RTC Shinyanga.
Muda mfupi baada ya
kutua Yanga, Lunyamila alipewa nyumba ya kuishi maeneo ya Magomeni lakini baada
ya kukaa kwa muda mfupi marehemu Method alimshawishi wakawa wanakaa wote Mwenge
katika eneo ambalo leo hii linajulikana kama Bamaga.
Lunyamila anasema
marehemu hakuwa mtu anayependa makuu, bali alikuwa kijana mwenye msimamo muda
wote wa maisha yake ndani na nje ya uwanja.
“Maisha yetu yalikuwa
ya amani na kila mmoja wetu alimfurahia mwenzake, hakika tulikuwa tukiishi kama
ndugu na mara nyingi Method alikuwa mfano mzuri kwangu kwani alikuwa mwalimu wa
maisha kila mara, hakuwa mjivuni wala asiyependa maendeleo ya mwenzake,”
anasema Lunyamila.
Lunyamila anakumbuka
zaidi namna Method alivyokuwa mhamasishaji mkubwa katika fainali za Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati wakati wanacheza huko Kampala mwaka 1993 kwenye
Uwanja wa Nakivubo ambapo walifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuifunga SC
Villa mabao 2-1.
Winga huyo wa zamani wa
Yanga anasema siku ambayo Method anafariki yeye alikuwa katika kambi ya Taifa
Stars iliyokuwa ikijiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi
ya Sudan.
Siku ambayo Method
anaagwa ili akazikwe ndiyo siku ambayo Taifa Stars ilikuwa inacheza na
Lunyamila ilibidi aombe kwa kocha na wachezaji wenzake kwamba asicheze mechi
hiyo kutokana na kuwa katika majonzi ya msiba wa rafiki yake kipenzi.
“Hata hivyo wachezaji
wenzangu pamoja na kocha walinifariji na kuniambia huku wakiniomba kwamba
nicheze mechi hiyo muhimu ili tuweze kuwa nafasi nzuri ya kuhakikisha tunacheza
Kombe la Afrika, nami nikakubaliana nao baada ya majadiliano ya muda mrefu,”
anasema Lunyamila.
Kwa mujibu wa Lunyamila,
Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku mfungaji wa mabao hayo akiwa
Madaraka Selemani.
Method Mdogo akiwa na mama yake Angelina....
STEVEN NEMES…
Huyu alikuwa kipa wa
Yanga wakati timu hiyo inatwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati ngazi ya
klabu, Steven Nemes anakumbuka jinsi Method alivyokuwa akiwahamasisha katika
mechi za michuano hiyo hadi kuchukua ubingwa.
“Kila tulipokuwa
tukiingia vyumba vya kubadilishia nguo huku tukiwa nyuma kwa mabao, Method
alikuwa akitumia muda mwingi katika kuwahamasisha wachezaji wenzake juu ya kupambana
na kuhakikisha wanarudisha bao au mabao na kushinda mchezo ikiwezekana,”
anasema Nemes.
Nemes anasema binafsi
ataendelea kumkumbuka Method kama rafiki yake wa karibu wa siku zote na mtu
ambaye aliishi naye klabuni bila matatizo yoyote yale.
MUHIMU;
MAREHEMU METHOD MOGELLA
HANA UNDUGU NA ZAMOYONI MOGELLA
Wengi wanaweza kudhani
wawili hawa yaani, Method Mogella na Zamoyoni Mogella walikuwa ndugu wa damu
kutokana na kufanana kwa majina yao, si kweli wawili hawa hawakuwa na undugu
wowote zaidi ya kufanana kwa majina yao tu.
Dada yake Method,
Angelina anasema; “Zamoyoni ni mtu ambaye ni kabila moja na sisi lakini hatuna
undugu wowote ule na wote hawa wamekutana katika mambo ya mpira tu.”
KWA NINI METHOD MOGELLA
NA SIYO METHOD MARTIN KUNAMBI?
Angelina anasema kwamba,
jina halisi la mdogo wake ni Method Martin Kunambi lakini katika kabila lao la
Waluguru mtu anaweza kuchagua jina lingine kutokana na hali halisi aliyonayo,
hivyo Method alipewa jina la Mogella ambalo maana yake ni mweupe. Jina lingine
linalofanana na hilo ni Mzeru.
Kwa upande wa wanawake
weupe wanaozaliwa katika kabila hilo mara nyingi huitwa Ng’oga ikimaanisha
asiyeogopa maji.
NAAM, HAYO NDIYO MAMBO
YA MAREHEMU METHOD MOGELLA.
Shaffih, huyu kijana ni mtoto wa ALEX KUNAMBI, tena walizaliwa mapacha kama sikosei, Picha yake na urefu wake unashabuhiana kwa karibu sana na marehemu baba yake. Alex alikuwa mtu wa watu, mcheshi na mpenda mpira pia, alifikwa na umauti baada ya kuugua kichwa ghafla na wakamkimbiza hospitali ya chuo kikuu cha Dr es Salaam lakini Mungu akamchukua, pale mtaani UNBUNGO MSEWE mtaa wote ulizizima baada ya kupata habari ya kifo cha ALEX KUNAMBI, watu walilia sana maana alikuwa rafiki wa kila mtu awe mkubwa awe mdogo, awe tajiri awe maskini, wote kwake ilikuwa sawa na ukizingatia alikuwa anatoka kwenye familia yenye uwezo haswa, pia alikuwa anapenda sa kucheza mpira hivyo ningemshauri Method afuate misingi ya marehemu baba yake. Nimeguswa sana na hii article na hakika imenifanya nimkumbuke kaka yetu ALEX KUNAMBI. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
ReplyDeleteWilfred