Juma Kaseja akiwa na kocha Ernst Brandts,Kocha msaidizi Felix Minziri na daktari wa timu Dr Nassor Matuzya
KIPA mpya wa Yanga, Juma
Kaseja leo asubuhi ametinga katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwa mara
ya kwanza kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama huku kipa mwingine wa timu hiyo
akishindwa kufika mazoezini hapo.
Kaseja amesajiliwa na Yanga
kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Simba kabla ya kuanza kwa
msimu huu na klabu hiyo kukataa kumuongeze mkataba mwingine.
Kipa huyo alifika
mazoezini hapo lakini akashindwa kufanya mazoezi kwa kuwa ni majeruhi wa ‘enka’
hivyo alisalimiana na Kocha Ernie Brandts na maafisa wengine wa klabu hiyo kisha
akatimua zake.
Mazoezi binafsi
yamharibia kuanza Yanga
Kaseja aliuambia
mtandao huu kwamba, kwa sasa yeye ni majeruhi wa enka hivyo hataweza kuichezea
Yanga lakini atafanya hivyo baada ya siku mbili kutoka sasa.
“Wakati timu haijaanza
mazoezi nilikuwa nafanya mazoezi binafsi hivyo sasa huko ndipo nilipoumia enka
na kama unavyoona mguu wangu umevimba hapa naenda kumuona daktari ili anipe
huduma zaidi,” alisema Kaseja.
Daktari wa Yanga,
Nassor Matuzya aliuambia mtandao huu kwamba, Kaseja alimpa taarifa za ugonjwa
wake na anadhani anaweza kurejea uwanjani kabla ya wikiendi hii.
Katika hali isiyokuwa
ya kawaida, kipa mwingine wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’ hakutokea katika
mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika jana.
Meneja wa Yanga, Hafidh
Saleh alisema hana taarifa za kutokuwepo kwa Barthez mazoezini hapo japokuwa
kila mchezaji anafahamu taarifa za kuanza kwa mazoezi hayo.
“Hapa kila mchezaji
aliambiwa kwamba leo tunaanza mazoezi sasa hao wengine ambao hawapo hapa sijuhi
wana matatizo gani, kwani sina taarifa zao zaidi ya Yule kipa chipukizi Yusuf
Abdul anayesumbuliwa na bega,” alisema Hafidh.
13 tu waanza mazoezi
Katika mazoezi hayo ya
Yanga, ni wachezaji 13 tu waliohudhuria huku wengine wakitarajiwa kufanya hivyo
kesho.
Wachezaji waliohudhuria
mazoezi hayo ni Nizar Khalfan, Said Bahanuzi, Hussein Javu, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Jerry Tegete, Oscar Joshua, Bakari Masoud, Ibrahim Job, Simon
Msuva, Hamis Thabit Rajab Zahir, Abdallah Mguhi, na Reliants Lusajo.
No comments:
Post a Comment