Kikosi cha Young Africans kilichoanza dhidi ya Mgambo Shooting
Young Africans mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara leo wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa timu ya Mgambo Shooting kutoka mkoani Tanga kwa mabao 3-0, mchezo uliofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Ikiwa na kumbukumbu ya ushindi katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Rhino Rangers kwa mabao 3-0, kikosi cha Young Africans kiliingia uwanjani kwa lengo la kuendeleza wimbi la ushindi na ndivyo hali ilivyokuwa
Hamis Kiiza, Saimon Msuva na Mrisho Ngasa walikosa mabao ya wazi dakika 15 za kipindi cha kwanza kufuatia kutokua makini katika umaliziaji na kujikuta mipira yao ikitoka pembeni mwa lango la Mgambo Shooting na mingine ikiokolewa na golikipa wa Mgambo Shooting Tonny Kavishe.
Mbuyu Twite aliipatia Young Africans bao la kwanza Young Africans dakika ya 31 ya mchezo kwa shuti kali la mita 25 kwa mpira wa adhabu alioupiga na kujaa moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kwa washabiki wa Yanga.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Young Africans 1 - 0 Mgambo Shooting.
Kipindi cha pili kilianza kwa Young Africans kufanya mabadiliko ambapo aliingia nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' kuchukua nafasi ya Rajab Zahir mabadiliko ambayo yaliongeza uwezo wa kumiliki mchezo na kulinda vyema lango lao.
Dakika ya 50 ya mchezo, Hamis Kiiza 'Diego' aliipatia Young Africans bao la pili kwa mkwaju wa penati kufuatia mlinda mlango wa Mgambo Shooting Tony Kavishe kumuangusha Didier Kavumbagu ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru ipigwe penati ambayo Kiiza hakufanya makosa.
Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao tatu la mchezo dakika ya 67 ya mchezo baada ya mpira uliorushwa na mlinzi Mbuyu Twite kumkuta Kavumbagu ambaye aliwazidi maarifa walinzi wa Mgambo Shooting na kuukwamisha mpira wavuni.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3 - 0 Mgambo Shooting.
Msimu uliopita katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom uliofanyika kati ya timu hizi Young Africans pia iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, mabao yaliyofungwa na Didier Kavumbagu, Jerson Tegete na Nadir Haroub 'Cannavaro'
Young Africans: 1.Dida, 2.Twite 3.Oscar, 4.Rajab/Cannavaro 5.Yondani, 6.Chuji, 7.Msuva/Lusajo 8.Domayo, 9.Kavumbagu, 10.Ngassa, 11.Kiiza
No comments:
Post a Comment