KIUNGO wa zamani
wa Yanga anayechezea Rhino Rangers ya Tabora, Nurdin Bakari amesema kosa kubwa
walilofanya katika mchezo wa jana na kufungwa mabao 3-0 na Yanga ni wachezaji
wenzake kushindwa kuwakaba vyema wachezaji wa Yanga.
Nurdin amesema hata
ukitazama mabao ya Yanga yalifungwa kutokana na uzembe wa mabeki wa timu yake
kushindwa kuwakaba viungo na washambuliaji wa Yanga ambao kuna wakati walicheza
wanavyotaka.
“Tumefungwa
kutokana na poor marking (umakini mdogo wa kukaba), muda mwingi Yanga walikuwa
wakicheza wanavyotaka na kupenya ngome yetu kirahisi. Lakini hili ni jambo la
kawaida kwa timu hizi zinazokuwa zimepanda daraja kwa mara ya kwanza, nadhani
baadaye mambo yanaweza kuwa mazuri na tutafanya vizuri zaidi,” alisema Nurdin.
Bao la kwanza la
Yanga lilifungwa na Hamisi Kiiza dakika ya 12 akiunganisha vyema krosi ya Simon
Msuva kutoka wingi ya kulia. Kiiza alifunga bao hilo akiwa katikati ya mabeki
wa Rhino ambao ni Julius Masonga na Laslaus Mbogo ambaye amewahi kuichezea Yanga
pia.
Bao la pili la
Yanga lilifungwa na Frank Domayo dakika ya 72 akimalizia pasi nzuri ya Mrisho
Ngassa akiwa ndani ya eneo la hatari la Rhino lakini mabeki hawakuweza kumkaba kiufasaha
na kuweza kufunga kirahisi.
Yanga ilipata
bao la tatu kupitia kwa Kiiza ambaye alimalizia vyema pasi ya Ngassa ambaye aliichambua
safu ya ulinzi ya Rhino kutoka wingi ya kulia na kumpasia Kiiza aliyefunga kirahisi.
Nurdin alienda
mbali kwa kusema kuwa, kitu kingine kilichosababisha kipigo kwao ni kutokana
kuwa na wachezaji wengi ambao hawana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya Bara.
“Wachezaji wengi
katika kikosi chetu hawana uzoefu wa kucheza ligi kuu, nadhani hilo nalo
lilikuwa tatizo kwetu kuweza kuifunga na kuizuia Yanga kufunga nadhani tukikaa
muda mrefu tunaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema Nurdin.
No comments:
Post a Comment