Amlima alivyo sasa |
Leo tunaendelea na simulizi ya mshambuliaji wa
zamani wa Yanga na Taifa Stars, Idfonce Amlima ambaye aliweza kusaini na
kuchukua fedha katika klabu tatu za Simba, Yanga na Majimaji, lakini akaruka
adhabu ya kufungiwa kisha akaenda Mtwara kuichezea Bandari ya huko.
Unaweza ukashangaa lakini ndiyo ukweli wenyewe,
Amlima wakati aking’ara na Bandari Mtwara hasa katika ufungaji wa mabao, mwaka
1992 klabu za Simba, Yanga na Majimaji ziliona uwezo wake na kumuwania
kumsajili.
Kwa kuwa Amlima alikuwa anahitaji sana fedha,
alifanya makubaliano ya usajili na klabu
zote hizo tatu, ambapo Simba na Yanga zote kwa pamoja zilikubali kisha
zikamlipa Sh. 1,000,000 (Milioni Moja),ili zimsajili.
“Majimaji niliwaonea huruma kwa ni timu ya kutoka
kwetu kusini (Songea), hivyo nikakubaliana nao wanipe Sh. 600,000 (Laki Sita)
ili nijiunge nao, nikazichukua hizo fedha, halafu nikakaa kimya,” anasema
Amlima.
Amlima anasema alichukua fedha hizo na kuanza
kuzitumia lakini ndani ya kichwa chake alijua wazi kwamba hana mpango wa
kuchezea hata timu moja katika msimu unaofuata.
“Nakumbuka nilipochukua fedha ya Simba, moja kwa
moja nikaenda Kariakoo na kununua bati 60 ambazo hadi leo zinazuia nyumba yangu
isiingize maji ndani na hizo nyingine za Yanga na Majimaji nikajihimarisha
katika mambo mengine,” anasema Amlima.
Amlima anasema, msimu wa ligi ilipoanza, aliichezea
Bandari Mtwara na kuziacha Simba, Yanga na Majimaji katika mataa na hata Chama
cha Soka Tanzania (FAT), kilimuhidhinisha kucheza Bandari.
“Hata Simba, Yanga na Majimaji zilipolalamika kuhusu
jambo hilo, FAT haikuwasikiliza na mimi nikachezea Bandari kama kawaida,”
anasema Amlima.
JINSI ALIVYOCHUKUA FEDHA ZA SIMBA
Nyumba anayoishi Amlima |
“Kusema kweli Simba ndiyo walikuwa watu wa kwanza
kutaka kunisajili, kama unakumbuka huo ni wakati ambao Simba ilikuwa na
wachezaji nyota kama George Masatu na Hussein Masha ambao nao walikuwa na
mpango wa kujiunga na Yanga chini ya mfadhili wa Yanga, Abas Gulamali (sasa
marehemu).
Nakumbuka habari kubwa wakati huo ilikuwa ni
wachezaji hao kujiunga na Yanga huku aliyekuwa mfadhili wa Simba Azim Dewji
naye akipambana kuhakikisha wachezaji hao hawaondoki katika kikosi chake.
Kiongozi mmoja wa Simba alinifuata na kuniambia hazma yao ya kutaka kunisajili,
name nikakubaliana naye kwa sababu nilikuwa na shida fedha,” anasema Amalima.
Amlima anasema alilazimika kuzichukua fedha hizo ili
aweze kutatua matatizo yake na alipewa Sh. Milioni Moja na moja kwa moja alikwenda
kununua bati alizoezekea nyumba yake kama inavyoonekana katika picha. Nasema
muda mfupi tu baada ya kuchukua fedha hizo alikwenda moja kwa moja kununua bati
ambazo kesho yake asubuhi alizipandisha katika basi hadi Mtwara mjini ilipo
nyumba yake, huku akisubiri muda wa kuichezea Simba.
MASATU, MASHA WAMFANYA ACHUKUE FEDHA YANGA
Amlima anasema wakati akijipanga namna ya kuichezea
Simba msimu unaofuata, Gulamali na watu wake walimfuata ili ajiunge na Yanga
kitu kilichomshangaza katika kichwa chake japokuwa alikuwa na uwezo mkubwa
uwanjani.
“Hakikuwa kitu chepesi kuamini kwamba Simba na Yanga
zinanihitaji kuzichezea kwa wakati mmoja, hapo kengele ililia katika kichwa
changu na kuona kuna kitu kinachoendelea nyuma ya pazia.
“Kweli baadaye nikabaini kwamba Yanga walitaka
kunisajili ili ionekane nami nimesaini mara mbili kama ilivyokuwa kwa akina
Masatu halafu katika makubaliano yao wabadilishane wachezaji ambapo labda mimi
niende Simba na mmoja kati ya Masatu au Masha acheze Yanga, mapango ambao
baadaye haikufanikiwa kwani Dewji na Gulamali walikubaliana wenyewe na
wachezaji hao wakacheza Simba kasoro mimi,” anasema Amlima.
MAJIMAJI WALIJILETA WENYEWE
“Siku tukiwa katika kambi ya timu ya taifa, rafiki
yangu mmoja aliyekuwa anacheza Majimaji aliniomba nimsindikize Kisutu (jijini
Dar es Salaam) kwa mmoja kati ya mabosi wa Majimaji ili akachukue fedha, sasa
tulipofika akanitambulisha kwa bosi wake.
“Yule bosi baada ya kusikia kwamba mimi ni Amlima
akaanza kunisifia na kuniomba nijiunge nao, sasa hapo nikaona mbona mambo
yanaenda kwa kasi mno na mimi bado naipenda Bandari ya Mtwara ambapo kulikuwa
na ajira ya kudumu?
Sikulaza damu nikawauliza Majimaji wana kiasi gani
cha fedha, nao wanakinijibu wana Sh. Laki Sita, sikulaza damu nikawaambia
leteni maana niliona hawana uwezo wa kutoa fedha nyingi halafu pia ni ndugu
zangu wa Kusini,” anasema Amlima.
KOSA LILILOFANYWA NA SIMBA, YANGA NA MAJIMAJI
“Timu zote hizo zilinipa fedha bila kunisainisha
sehemu yoyote kwa kuamini kwamba wachezaji wote hawawezi kutambua mambo ya
kisheria na wala hawana ujanja wa kukataa walichofanya bila maandishi, kama
unavyoona leo hii.
“Sasa mimi wote hao tulikubaliana mdomoni tu na zile
fomu au mkataba wa kukubaliana hatukuwa tumesaini ambao ungeweza kupelekwa Fat
maana wakati ule kulikuwa na karatasi moja tu inayotambuliwa na Fat na ukisaini
hiyo unakuwa hauna ujanja mwingine tena.
Kwa hiyo kwa kuwa nilifahamu hali hiyo halafu
niliona kama usajili wangu ulikuwa wa kulipizana kisasi nikaona bora nirudi
zangu Bandari kuendelea na kazi yangu kwani kule hakukuwa na mambo ya kusaini
maana nilikuwa na ajira yangu,” anasema Amlima.
Kweli msimu uliofuata niliendelea kuitumikia Bandari
na ingawa baadhi ya watu hawakunielewa na hata hizo klabu zenyewe hazikuweza
kunisumbua sana japokuwa nilikuwa napata usumbufu wa aina yake,” anasema
Amlima.
Amlima anasema klabu zote hazikuwa na kielelezo
ambacho wangeweza kumtia hatiani kwa kuchukua fedha kwao ili aweze kupewa
adhabu na Fat ambayo kwa wakati huo ilikuwa makini sana na mambo ya usajili wa
wachezaji.
APITIA TANDALE KURUDI YANGA BURE
Baada ya kucheza sokakwa muda mrefu akiwa na Bandari
na klabu mbalimbali za Oman, Amlima aliamishia makazi yake kwa muda jijini Dar
es Salaam na makazi yake yalikuwa katika wilaya ya Kinondoni hasa Mwanyamala na
Kinondoni.
“Wakati nipo Mwanyamala nikawa nafanya mazoezi
katika uwanja wa shule ya msingi Mwananyamala B, ambapo klabu ya National ya
Tandale iliniomba niwasaidie katika michuano ya Masafi pamoja na Kombe la
Kinesi, huko nilicheza vizuri na Yanga wakanifuata huo ulikuwa mwaka 1994.
“Wakati nataka kusajiliwa Yanga, viongozi
wakanikumbushia fedha zao nilizozichukua, name sikuwa na jinsi nikaamua kusaini
fomu zao na kucheza soka kwa moyo wangu wote hadi nikapata mafanikio ndani ya
timu hiyo japokuwa kuna mambo mengi nilikutana nayo ambayo mengine mazuri na
mengine ya kusikitisha na yanayonifanya nikatishe mapema safari yangu ya soka,”
anasema kwa masikitiko Amlima.
USIKOSE SEHEMU YA TATU YA MAKALA HII ILI UWEZE KUJUA
AMLIMA ALIKUMBANA NA MAMBO GANI YANGA.
No comments:
Post a Comment