Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya pili kesho (Agosti 24 mwaka
huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani huku macho na masikio ya washabiki
wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Yanga na Coastal Union.
Mechi
hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni
kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
Mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro ndiye atakayepuliza filimbi wakati
Kamishna atakuwa Omari Walii kutoka Arusha.
Mtibwa
Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko
Turiani mkoani Morogoro wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora
utakuwa mwenyeji wa pambano kati ya wenyeji Rhino Rangers na Azam.
Vumbi
lingine litatimka kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani
Pwani wakati maafande wa JKT Ruvu watakapokwaruzana na wenzao wa
Tanzania Prisons kutoka Mbeya. Mbeya City na Ruvu Shooting zitacheza
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jiji
la Tanga litakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ashanti
United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Oljoro JKT itakuwa
mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri
Abeid jijini Arusha.
RATIBA COPA U15 KUPANGWA ALHAMISI
Ratiba
ya michuano ya U15 Copa Coca-Cola ngazi ya kanda mwaka huu itapangwa
keshokutwa (Agosti 29 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Michuano
hiyo ya kanda itaanza Septemba Mosi mwaka huu wakati mikoa inakumbushwa
kuwa inatakiwa iwe imewasilisha usajili wa wachezaji wao kufikia Agosti
28 mwaka huu kupitia email ya TFF ambayo ni tanfootball@tff.or.tz na nakala kwa madadi_salum@ yahoo.com
Pia
mikoa inakumbushwa kutowajumuisha wanafunzi wa darasa la saba katika
timu zao katika ngazi ya kanda na fainali itakayochezwa Dar es Salaam
kuanzia Septemba 7 mwaka huu kwa vile watakuwa katika mitihani ya
kumaliza elimu ya msingi. Timu zinatakiwa kufika vituoni Agosti 30 mwaka
huu.
Kanda
hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma,
Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,
Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.
Zanzibar
itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja
wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara,
Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.
Kanda
ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma
wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.
Mwanza
itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za
Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro
itaingiza timu mbili.
No comments:
Post a Comment