Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imezuia usajili wa wachezaji 37 wa klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kutokana na usajili wao kuwa na kasoro.
Klabu
husika zimetakiwa kurekebisha kasoro hizo kabla ya kuanza kuwatumia
wachezaji hao kwenye mechi za VPL ambazo zinaanza leo (Agosti 24 mwaka
huu) katika viwanja mbalimbali nchini.
Klabu
ya Simba inatakiwa kumfanyia uhamisho Betram Arcadi Mwombeki kutoka
Pamba SC wakati wachezaji Gilbert John Kaze na Amisi Tambwe bado
hawajapata ITC kutoka Burundi na hawana vibali vya kufanya kazi nchini.
Mchezaji Joseph Owino tayari ITC imepatikana lakini hana kibali cha
kufanya kazi nchini. Pia kipa Abel right Dhaila hana kibali cha kufanya
kazi nchini.
Vilevile
Simba inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji wawili iliyowasajili
katika kikosi chake cha U20. Wachezaji hao ni Twaha Shekue Ibrahim
kutoka Coastal Union 20 na Adeyun Saleh Seif (Oljoro JKT U20).
Nayo
Yanga inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Rajabu Zahir Mohamed kutoka
Mtibwa Sugar U20 wakati Hussein Omari Javu bado ana mkataba wa mwaka
mmoja na Mtibwa Sugar huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa
mchezaji mwenyewe, Mtibwa Sugar au Yanga kama mkataba huo ulivunjwa au
umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.
JKT
Ruvu Stars inatakiwa kuwafanyia uhamisho (transfer) wachezaji Salum
Machaku Salum aliyekuwa Polisi Morogoro na Emmanuel Leonard Swita (Toto
Africans). Mgambo Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji
Mohamed Hussein Neto (Toto Africans), Kulwa Said Manzi (Polisi Morogoro)
na Mohamed Ally Samata (African Lyon).
Pia
Salum Aziz Gilla anaonekana bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Coastal
Union huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji
mwenyewe, Coastal Union au Mgambo Shooting kama ulivunjwa au umenunulia
na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.
Tanzania
Prisons inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji James Mjinja Magafu
kutoka Toto Africans na Six Ally Mwasekaga (Majimaji). Nayo Coastal
Union inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Kenneth Abeid Masumbuko
kutoka Polisi Morogoro.
Kagera
Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Suleiman Kibuta Rajab
(Toto Africans), Godfrey Innocent Wambura (Abajalo), Eric Mulera Muliro
(Toto Africans), Adam Juma Kingwande (African Lyon) na Peter Gideon
Mutabuzi (Toto Africans).
Pia
Kagera Sugar imepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya
mchezaji Kitagenda Hamis Bukenya, lakini bado hana kibali cha kufanyia
kazi nchini (work permit).
Kwa
upande wa Ruvu Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Abdul
Juma Seif (African Lyon), Lambele Jerome Reuben (Ashanti United), Juma
Seif Dion (African Lyon) na Cosmas Ader Lewis (African Lyon).
Oljoro
JKT inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Tizzo Charles Chomba kutoka
Polisi Morogoro, lakini imekataliwa kumsajili mchezaji Damas Mussa
Kugesha wa Mlale JKT kwa kigezo kuwa ni askari na amehamishiwa Arusha
kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi. Kama Oljoro JKT inamtaka mchezaji huyo
ni lazima ifuate taratibu za usajili kwa kumfanyia uhamisho kutoka Mlale
JKT.
Nayo
Mtibwa Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Shomari
Sharrif (Polisi Morogoro), Salim Hassan Mbonde (Oljoro JKT U20) na
Hassan Salum Mbande iliyemsajili kwenye kikosi chake cha U20 akitokea
Oljoro JKT U20.
Ashanti
United haiwezi kumtumia Said Maulid Kalikula aliyekuwa akicheza Angola
kwa vile hajapata ITC. Nayo Rhino Rangers inatakiwa kuwafanyia uhamisho
wachezaji Ally Ahmad Mwanyiro (Mwadui FC), Laban David Kambole (Toto
Africans) na Musa Boaz Chibwabwa (Villa Squad).
Wachezaji
waliosajiliwa kutoka nje ambao ITC zimefika na pia wana vibali vya
kufanya kazi nchini ni Crispine Odula Wadenya kutoka Bandari ya Kenya na
Yayo Wasajja Fred Lutimba kutoka URA ya Uganda waliojiunga na timu ya
Coastal Union. Pia Mtanzania Hamis Thabit Nyige aliyejiunga na Yanga
kutoka Ureno naye tayari na ITC.
Kwa
mujibu wa kanuni, wachezaji wote wa ridhaa (wa madaraja ya chini
ikiwemo Daraja la Kwanza) wanatakiwa kufanyiwa uhamisho (transfer) kwa
klabu husika kujaza fomu za uhamisho na kulipia ada Chama cha Mpira wa
Miguu cha Wilaya, Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa na TFF.
Pia
TFF inakumbusha kuwa wachezaji wanaotajwa kuwa wamesajiliwa kama
wachezaji huru (free agent) ni lazima waoneshwe kama huko walipokuwa
mikataba imekwisha au la.
No comments:
Post a Comment