KIRAKA wa Tanzania, Shomari Kapombe ametambulishwa juzi Ahamisi
kwenye mazoezi ya klabu ya AS Cannes ya Ufaransa, lakini Kocha Mfaransa
aliyetimuliwa Simba, Patrick Liewig amesema timu hiyo haina hadhi ya
Kapombe.
Hata hivyo, Simba imemjibu Liewig kuwa asiwe na wasiwasi kwani tayari Kapombe anatakiwa na timu ya daraja la pili ya Ufaransa.
Liewig aliiambia Mwanaspoti kwa simu kutoka jijini
Paris, Ufaransa jana Ijumaa kwamba klabu hiyo ya daraja la nne ni ya
hadhi ya chini sana kulinganisha na ubora wa Kapombe ambaye alipaswa
kuchezea madaraja ya juu hivyo Simba imempeleka sehemu anakokwenda
kupoteza muda wake.
Liewig alisema; “Naijua Cannes ni timu ndogo sana,
inashiriki daraja la nne ni ya chini sana kulinganisha na ubora wa
Kapombe niliyemfundisha hapo Simba. Yeye hadhi yake ni daraja la kwanza
au la pili, na zipo klabu nyingi tu ambazo angeweza kupata nafasi.”
“Simba na huyo wakala wanampotezea Kapombe muda
wake, wachezaji wakubwa wa Tanzania wanapaswa kukaa chini na kujipanga.
Klabu zikae na watu wa maana zifanye mambo kwa kufuata weledi, mimi
najuana na watu wengi sana kuanzia makocha na viongozi ambao naweza
kuwaunganishia wachezaji wa Tanzania na wakacheza soka daraja la kwanza.
“Mchezaji mwenyewe ajipange anifuate aonyeshe nia
ya kweli mimi nitashirikiana na viongozi nitamsaidia, lakini huko
alikokwenda Kapombe sijapaafiki,” alisisitiza kocha huyo ambaye bado
hajapata dili mpya.
Katika klabu hiyo, Kapombe atajumuika na ‘Waswahili’ wanne kutoka Burundi, Uganda, Senegal na Togo.
Kapombe atakuwa katika klabu hiyo na iwapo atauzwa ndio Simba itapata mgawo wake.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Usajili wa Simba,
Zacharia Hanspoppe aliliambia Mwanaspoti jana Ijumaa kuwa hawana
wasiwasi na suala hilo kwani tayari Kapombe ameivutia timu ya daraja la
pili.
“Sisi tunajiamini na mambo tunayoyafanya, hapo
nazungumza na wewe nilikuwa napata mawasiliano kutoka Ufaransa kuwa kuna
timu ya daraja la pili inamhitaji Kapombe. Hao AS Cannes wakimuuza
Kapombe sisi tunapata asilimia 40,” alisema Hanspoppe.
SOURCE: MWANASPOTI
SOURCE: MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment