Search This Blog

Monday, August 26, 2013

MAKALA: MSIMU WAANZA KWA KISHINDO, MALALAMIKO NA DOSARI


Na Baraka Mbolembole

Msimu mpya wa ligi kuu Tanzania Bara, Vodacom Primier League ulianza wikiendi iliyopita kwa viwanja saba tofauti nchini kuzipokea timu 14 za ligi hiyo. Msimu wa 2013/ 14 umeanza na mabao ya kutosha, huku mechi ya Yanga na Ashanti United ikizalisha magoli sita kati ya mabao 19 yaliyofungwa katika viwanja sita kati ya saba siku ya ufunguzi. Mechi kati ya timu inayocheza kwa mara ya kwanza ligi kuu, Mbeya City katika uwanja wa Sokoine, Mbeya haikutoa bao lolote, wakati kikosi hicho cha kocha Juma Mwambusi kilipolazimishwa suluhu tasa na timu ya Kagera Sugar.

Wakati, City wakipata pointi moja ya kuanzia msimu, timu nyingine inayocheza ligi kuu kwa mara ya kwanza, Rhino Rangers iliweza kusawazisha mara mbili, magoli ya kiungo, Jonas Mkude wa timu ya Simba na kulazimishwa sare ya mabao 2-2, katika pambano hilo lilokuwa na msisimko mkubwa katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, Rangers ilionesha kuwa wapo tayari kupambana na si kuwa wasindikizaji katika ligi hiyo, mabao mawili waliyopata katika mchezo wao wa kwanza wa kihistoria, tena mbele ya Simba ni dalili njema, walikaribia kuwafunga mabingwa hao mara 18 wa kihistoria lakini hawakuwa na bahati ya kupata mkwaju wa penati, na hata walipofunga bao lilikataliwa na mwamuzi.

Lakini wanatakiwa kusahau yote hayo kabla ya kuwakabili, Azam FC, siku ya Jumatano katika uwanja huo huo.

Mchezo kati ya timu za Ruvu Shooting na Tanzania Prisons ulimalizika kwa kikosi cha kocha, Charles Boniface Mkwasa kushinda kwa mabao 3-0, katika uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Mkoani Pwani. Shooting katika kipindi cha miezi 18 iliyopita imekuwa ikijihimarisha na kufanya vizuri huku wakitegema asilimia kubwa ya wachezaji chipukizi, inacheza mpira wa kushambulia hata dhidi ya timu kubwa, na wameweza kuanza msimu kwa kishindo, ni mechi ya tatu iliyozalisha mabao mengi ( matatu), na watakuwa ugenini siku ya Jumatano kucheza na City katika uwanja wa Sokoine, Mbeya. 


 

Mechi kati ya Mtibwa Sugar na Azam FC ilikuwa kali na yenye ushindani wa hali ya juu, mechi hiyo ndiyo iliyotoa bao la kwanza la msimu ambalo lilifungwa na mchezaji, Luizio. Msemaji wa Mtibwa, Thobias Kifaru aliamua kutupa lawama zake zote kwa waamuzi wa mchezo huo kwa kuwa walinyimwa penati ( kwa mujibu wa msemaji huyo). Sare ya bao 1-1, imeziweka timu hizo katika nafasi iliyo sawa katika msimamo, na siku ya jumatao Mtibwa wataendelea kubaki katika uwanja wao wa Manungu kuwakaribisha, Kagera Sugar na Azam FcC itasafiri hadi mjini Tabora kucheza na Rangers.


  Timu ya Coastal Union ya Tanga ilianza vizuri msimu huu kwa kupata ushindi ugenini mbele ya majirani zao timu ya JKT Oljoro ya Arusha, kiwango chao kilikuwa ni kizuri , na ushindi wa mabao 2-0 unawafanya wajiamini zaidi kabla ya kuwakabili mabingwa watete, Yanga siku ya jumatano hii katika uwanja wa Taifa.



Mshambuliaji, Shaaban Kondo wa timu ya JKT Ruvu alifungsa mara mbili na kuisaidia timu yake kuanza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Mgambo JKT ya Tanga, katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga. JKT Ruvu ambayo ilinusurika kushuka daraja msimu uliopita iliweza kujiweka sawa na wameonesha mwanzo mzuri kwao.



NB; Ligi imeanza kwa kishindo huku washambuliaji, Jerry Tegete wa Yanga, Kondo wa JKT Ruvu na kiungo Jonas Mkude wote wakifunga mabao mawili. Ni dalili kuwa walinzi wanatakiwa kukaza buti zao zaidi ili kuzuia washambuliaji wasiendelee kutamba, wakati huo huo washambuliaji kwa upande wao wakihakikisha wanamaliza matatizo yao ya ufungaji ambayo yamekuwa yakionekana mara kwa mara.



UCHEZESHAJI; Waamuzi wa michezo ya Tabora, Manungu, walianza kutia dosari ya uchezeshaji na kutupiwa lawama kuwa walikuwa na upendeleo kwa baadhi ya timu. Haitapendeza kuona mwanzo tu wa ligi hali ya kukosa uhaminifu kwa waamuzi ikijitokeza na kuzivuruga timu.



DOSARI; Wachezaji kukosa vibali vya utambulisho wao ni kosa kubwa la kwanza kufanyika tena limetokea siku ya kwanza ya msimu, huu ni uzembe ambao hautakiwi kujirudia kama tunataka ligi bora zaidi ya ilivyokuwa mwanzoni ni lazima wahusika wote wawe bize na kutekeleza majukumu yao kwa wakati.



MALALAMIKO YA VIWANJA; Awali shirikisho la soka nchini lilitaka kuvufungia viwanja vya Ally Hassan Mwinyi, Kaitaba, Bukoba na ule wa Sokoine, Mbeya kutokana na hali ya ‘ pitch’ kutokuwa nzuri, na mara baada ya kumsalizika kwa mchezo wa Simba na Rangers, Simba walianza kutoa malalamiko ya uwanja. Je, malalamiko kama haya yanatakiwa kupewa nafasi na kuchukuliwa kama sababu kubwa ya timu kuboronga?. Mimi kwa upande wangu nafikiri vilabu vinatakiwa kutambua kuwa vinatumia viwanja vibovu zaidi kufanyia mazoezi kuliko vile wanavyokuwa wanalalamikia ,

No comments:

Post a Comment