Search This Blog

Friday, August 23, 2013

MAKALA: ·MSIMU WA 16 LIGI KUU YA VODACOM, MABINGWA WATATU


·MSIMU WA 16 LIGI KUU, MABINGWA WATATU
. Simba, Yanga ni vinara
. Mtibwa, Azam hesabu ndogo
NA BARAKA MBOLEMBOLE

 Msimu wa 16 wa ligi kuu ya Vodacom, Tanzania Bara, ( VPL), unataraji kuanza kutimua vumbi lake wikiendi ijayo, mara baada ya kushuhudiwa kwa klabu za Yanga SC na Azam FC, zikikata utepe kwa mchezo wa Ngao ya Jamii, siku ya Jumamosi iliyopita. Mabingwa watetezi ni Yanga, na timu nyingine zilizomaliza katika nafasi tano za juu msimu uliopita ni Azam, Simba SC, Kagera Sugar, na Mtibwa Sugar.
 
Misimu 15 iliyopita timu za Dar es Salaam zimekuwa zikitawala ligi hiyo, ni Mtibwa Sugar pekee ya kutoka Mkoani, Morogoro ambayo imeweza kuvunja utawala wa Yanga na Simba. Mtibwa ilitwaa ubingwa mfululizo katika miaka ya 1999 na 2000, miaka miwili baada ya kuanza kwa mfumo wa ligi kuu kutoka ligi daraja la kwanza, mwaka 1997, wakati ambao kwa mara ya kwanza, soka la Tanzania lilipopata udhamini wa kwanza wa ligi kuu baada ya kampuni ya bia nchini kupitia kinywaji chake cha Safari Lager walipojitosa kusaidia mpira wa Tanzania.
Katika misimu minne iliyopita, timu ya Azam imekuwa mfano wa kuigwa na timu nyingine nchini, hawajafikia mafanikio makubwa, lakini miaka mitano iliyopita wakati ikianzishwa na kutumia udhaifu wa mfumo wa mpira wetu nchini, ikaanza kucheza ligi kuu. Msimu wake wa kwanza, 2008/09 haikufanya vizuri na ikanusurika kushuka daraja, lakini walijihimarisha taratibu na kumaliza katika nafasi ya tatu mara mbili mfululizo, na wameweza kumaliza katika nafasi ya pili mara mbili mfululizo, huku mara ya mwisho wakifanya hivyo, Mei, mwaka huu.
Pamoja na uzoefu ambao umekuwa ukitajwa kama sababu ya timu fulani kutwaa mataji, hesabu pia zinahitajika katika mfululizo wa ligi yoyote ile. Katika misimu kumi iliyopita ya ligi kuu England ni makocha watatu tu ambao wamefanikiwa kutwaa taji hilo, Jose Mourinho, Sir Alex Ferguson, Roberto Mancini na Carlo Ancelotti. Ukitazama mafanikio yao katika EPL, makocha hao ni wana-hisabati wazuri. Walikuwa wakitazama kwanza timu shindani katika ubingwa na kupiga hesabu za pointi ambazo kama watazikusanya watakuwa mabingwa. Pointi 85-90 zinatosha kuwa bingwa wa England, hasa ukichanganya na zile ambazo unakuwa umezipata kutoka kwa mshindani mwenzako wa ubingwa. Jose, alikuwa akitafuta pointi walau nne kwa Manchestester United ili atwae taji. Alipofanikiwa aliweza kupata ubingwa, na hata Carlo pia alikuwa akifanya hivyo. Fergie pia alikuwa akitwaa taji kwa mtindo wa hesabu za kukusanya walau pointi 82 katika michezo 38 ya ligi kuu, huku akihakikisha hafungwi na mpinzani wake namba moja katika kuwania ubingwa. Simba na Yanga zimekuwa zikichukua ubingwa baada ya kukusanya pointi zisizodizi 59, hawaendi kihesabu zaidi ya kutazama zenyewe, faida kwao ni kwamba timu nyingine zimekuwa zikilala. Zinacheza ligi bila hesabu, zinasubiri mechi nne dhidi ya Simba na Yanga na kuonesha ubora wao basi. 
  Azam, wangeweza kuwa mabingwa mwaka jana ( 2012) kama wangeifunga Mtibwa Sugar, pale Chamanzi Complex, bahati mbaya mechi ikavunjika wakiwa sare ya bao 1-1 na iliporudiwa wakapoteza kwa mabao 2-1. Kila mpenda soka alikuwa ameelekeza akili yake katika mchezo ule, kwa kuwa Azam wangeshinda walikuwa wakiongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili mbele ya Simba, na sare tu katika mchezo wa mwisho dhidi ya JKT Ruvu ingewapa ubingwa wa kwanza wa ligi kuu nchini. Matokeo yake, timu ya Simba ikatwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi moja mbele ya Azam. Msimu uliopita, Simba haikuwa imara, Yanga walikuwa wakijipanga upya baada ya kufanya vibaya katika msimu wa 2011 / 12, na Azam walijipanga upya na kuongeza wachezaji wazoefu kama, Gaudensi Mwaikimba, Brian Omony, Hamphrey Mieno na wengineo  lakini tatizo lilelile likawaumiza tena, kukosa ushindi katika michezo ya kuamua bingwa. Nafikiri tangu miaka ile ambayo walimtimua kipa Mrundi, Vladimir Niyonkuru  hadi sasa Azam wangekuwa mabingwa mara tatu mfululizo wa ligi kuu, hesabu zao na uzoefu wao ni mdogo kuliko Simba na Yanga ila wanaweza kuwapita wakongwe hao wa soka nchini kama wataamua kujifunza kutokana na makosa yaliyopita.
ULALAMISHI USIO NA MAANA HAUTAKIWI
Sitafurahi kusikia timu za Simba na Yanga zikilalamikia kuhusu ubovu wa  viwanja, hiyo ndiyo hali halisi tuliyonayo kwa kipindi chote tangu zama za ‘ Mwalimu’, isitoshe viwanja ambavyo wamekuwa wakivitumia kwa muda mwingi wa msimu kujifua kwa ligi hiyo ni vibovu zaidi
 WACHEZAJI WAJITAMUE  SASA
Kinachotakiwa kutoka kwa wachezaji msimu huu ni kiwango kikubwa zaidi ya ilivyokuwa katika misimu yao iliyopita. Wanatakiwa wajitambue kuwa bado wana viwango vya kawaida, wajitume na watambure kuwa Watanzania wanawategemea kuwawakilisha katika timu za Taifa. Wachezaji vijana wanatakiwa kuitimua vyema nafasi waliyopata kwana hata Mfame wa kandana duniani, Pele alianza soka katika umri wa misaka 16 na akafunga mabao sita katika fainali za kombe la dunia akiwa na umri wa miaka 17. Nidhamu ni jambo linalotakiwa kuonekana kutoka kwao japo hili pia linahitajika kutoka kwa mdau wa soka nchini. Wachezaji wazoefu ni lazima watambue kuwa wakati mwingine ni lazima waingie katika majaribu ya kupoteza nafasi zao katika vikosi vyao, changamoto kama hizo ndizo ambazo humkuza mchezaji kuanzia katika utimamu wa mwili na akili vitu ambavyo ni muhimu katika soka. Chuki kati ya wachezaji wa timu moja si kitu kizuri na uadui haupo katika soka. Wakongwe wajitambue kuwa wao ni makocha wa ziada katika timu zao na wakubali matokeo pale kocha anapoamua kufanya mabadiliko, kuzungumza hovyo mambo ya timu ni tabia mbaya, haitakiwi kwa kuwa wapo watu ambao wanaweza kufanya kazi hiyo kwa usahihi.
 KUKUBALI MATOKEO UWANJANI

Imezoeleka kuona Simba na Yanga zikitwaa mataji, na pale ilipotokea timu ya Mtibwa na kutwaa mataji mfululizo timu hiyo ilipigwa vita sana na matokeo yake ligi ikapunzu msisimko, umefika wakati wa kukubali matokeo ya mchezo wa soka japo wakati mwingine huwa yanaumiza sana. Kuanzia kwa mashhabiki hadi kwa wachezaji wa timu kubwa kama Simba, Yanga na Mtibwa kuwa wanakubali matokeo kwa kuwa soka lina matokeo ya aina tatu tofauti, kushinda, kufungwa, ama sare. Timu kubwa zinatakiwa kutambua kuwa zinakwenda kuanza msoimu kushindana na timu nyingine na si kushinda zenyewe kwa zenyewe ili kuwa bingwa
KATIKA HILI, viongozi waache  kununua mechi kwa wachezaji na marefa. Na marefa hawatakiwi kutoa maamuzi kwa uoga wa jina la timu ama mchezaji Fulani, wachezaji nyota wanatakiwa kulindwa mchezoni na walinzi wao ni waamuzi lakini isipitilize na kuwakera wengi  huku sababu kubwa ikiwa na maslai binafsi.
WANAHABARI
Kundi hili ndilo hufikisha taarifa zote muhimu za soka kwa mashabiki, ukweli kila kitu kinachofanyika katika mchezo huu kuna nguvu kubwa ya wana habari. Lakini huwa wanatia shubiri pale wanapotoa sifa kubwa kwa mchezaji ambaye hatakiwi kupewa sifa hizo. Ni tatizo ambalo linatakiwa kupunguzwa kama si kumsalizwa kabisa.
NB; Kwa vile siku hizi kuna Kamati ya ligi, naona tunapiga hatua na tunakwenda vizuri kidogo kuliko kule tulikotoka hivyo kamati inatakiwa kutotoa upendeleo usio na lazima kwa baadhi ya timu ili tupate ligi kuu iliyo bora.

No comments:

Post a Comment