MWENYEKITI mpya wa Chama cha netiboli Tanzania (Chaneta), Anna Kibira atakabidhiwa rasmi madaraka Mei 11 tayari kuanza kukitumikia chama hicho.
Kibira aliyechaguliwa hivi karibuni kwenye uchaguzi mkuu akichukua mikoba iliyoachwa na Anna Bayi alisema baada ya makabidhiano hayo amepanga kuandaa mpango mkakati wa kuendeleza mchezo huo kimataifa.
"Mara nitakapokabidhiwa nitakaa na kamati ya utendaji na kuweka mikakati ya kuendeleza yalemazuri yote yalioachwa na wenzetu ikiwamo kuhakikisha timu ya taifa inafuzu kushiriki kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwakani," alisema
Katibu mkuu wa Chaneta aliyemaliza muda wake, Rose Mkissi aliliambia gazeti hili jana kuwa wamechelewa kumkabidhi Kibira na kamati yake ofisi kutokana na michezo ya Mei Mosi iliyomalizika jana.
"Tulitaka kuukabidhi uongozi mpya ofisi mapema tangu tulipomaliza uchaguzi Dodoma ingawa ilishindikana kutokana na michezo ya mei mosi," alisema Mkissi.
Kwa mujibu wa Mkissi makabidhiano hayo yatafanyika jijini Dar es Salaam tayari kwa uongozi huo kuanza kuitumikia Chaneta.
No comments:
Post a Comment