KLABU ya Simba inapenda kutoa taarifa hizi mbili muhimu kwa umma siku ya leo.
KUAHIRISHWA KWA MECHI YA RUVU SHOOTING
UONGOZI wa Simba umekubaliana na hatua ya serikali kuzuia kuchezwa kwa
mchezo uliopangwa kuchezwa leo wa Ligi Kuu ya Tanzania baina ya Wekundu
wa Msimbazi na Ruvu Shooting Stars.
Hata hivyo, uongozi wa Simba
haujafurahishwa na namna uzuiaji huo ulivyofanyika. Taarifa imetolewa
leo kwenye siku ya mechi yenyewe wakati maandalizi yote yakiwa
yamefanyika na hivyo kusababisha matatizo katika sehemu kubwa tatu.
Mosi, uongozi wa Simba umeingia gharama kubwa ya kuweka timu kambini na
kujiandaa na mechi. Pili, benchi la ufundi na wachezaji walikuwa tayari
wamejiandaa na mechi kimwili na kiakili na kuahirishwa huku kwa mechi
kumesaidia tu kuvuruga programu. Tatu, wapenzi na washabiki wa Simba
wamepata usumbufu wa kwenda uwanjani na kukuta hakuna mechi.
Uongozi
wa Simba unapenda kutumia nafasi hii, katika namna ya kipekee kabisa,
kuwaomba radhi wapenzi na wanachama wake ambao walifika Uwanja wa Taifa
kutazama mechi ambayo haikuwapo.
Washabiki ndiyo wanaoifanya Simba
na mchezo wa mpira wa miguu nchini uwe na umaarufu ulionao na bila wao
ligi yetu inaweza kupoteza nguvu na ushindani ilionao.
Simba SC
inapenda kuwe na utaratibu unaojulikana wa kuahirisha mechi wa walau saa
48 kabla ya siku ya mechi. Hii itasaidia pande zote zinazohusika. Kama
mechi imeshindikana kwa sababu za nje ya uwezo wa kibinadamau (Force de
Majeure) kama vile mafuriko, tetemeko la ardhi na vimbunga, mechi
inaweza kuahirishwa ghafla lakini si kwa mechi ambayo uwepo wake
ulifahamika miezi kadhaa nyuma.
Tunashauri pia kwamba siku za mechi
ambapo Ligi Kuu inachezwa (match days), inatakiwa kuwa zinafahamika na
isiwe kila siku mechi zinachezwa. Simba ilikuwa na mechi wikiendi
iliyopita na Ruvu ilikuwa na mechi Mbeya zaidi ya wiki moja iliyopita na
hivyo mechi hii ingeweza kuchezwa hata jana (Jumatano) ambayo ni siku
ya kawaida kwa mechi kuchezwa badala ya leo Alhamisi.
Ni matumaini
yetu kwamba kuahirishwa kwa mechi hii kutakuwa fundisho kubwa katika
upangaji wa ratiba na uahirishaji wa mechi ambao una faida kwa pande
zote husika.
Poppe arejea Simba
MWENYEKITI wa Simba, Mhe, Ismail
Aden Rage, amemshukuru aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
klabu, Zacharia Hans Poppe, kwa kukubali kurejea kushikilia nyadhifa
zake zote.
Poppe alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake za uongozi ndani
ya Simba Machi 7 mwaka huu, kutokana na hali ya migogoro iliyokuwapo
wakati huo.
Hata hivyo, Rage alikataa kujiuzulu huko kwa Poppe na akasema atamshawishi abadili maamuzi kwa manufaa ya Simba.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwaarifu wana Simba popote walipo kwamba
Poppe amerejea na yuko tayari kuitumikia Simba kama Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba,” alisema Rage.
Kwa upande wake, Poppe alisema amerejea Simba kutokana na utulivu
ulioanza kujitokeza klabuni na kwamba nia yake ni kuhakikisha klabu
inafanya usajili mzuri na wa kiwango kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi
Kuu.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
No comments:
Post a Comment