Search This Blog

Monday, March 18, 2013

TFF WAIPONGEZA AZAM KUENDELEA KUIWAKILISHA VIZURI TANZANIA KIMATAIFA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaipongeza klabu ya Azam kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata timu yake katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

Mechi hiyo dhidi ya Barrack Young Controllers II ilichezwa jana jijini Monrovia, na timu hizo zitarudiana wikiendi ya Aprili 6 au 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo unaiweka Azam chini ya kocha wake Stewart John Hall katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya mechi ya marudiano. Bila shaka ushindi wa timu ya Azam pamoja na mambo mengine umechangiwa na klabu hiyo kujipanga vizuri.

Hata hivyo ushindi huo bado ni changamoto kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa Azam kuhakikisha unajipanga vizuri kwa mechi ya marudiano kwa vile mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu; kushinda, kutoka sare au kufungwa.

Msafara wa timu ya Azam unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo unatarajiwa kurejea nchini kesho alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.

No comments:

Post a Comment