Inawezekana akawa anafanya hivyo kutetea nafasi yake ndani ya Azam FC kwa kuwa yeye ni meneja wa timu hiyo, lakini kama mnakumbuka ni Patrick huyu huyu aliyekuwa mstari wa mbele kupigania mapinduzi ya kweli kwenye soka la Tanzania.
Patrick alikuwa hodari kutoa mada na ushauri katika vyombo vya habari kuanzia redio, televisheni na hata magazeti mbalimbali hapa nchini zenye lengo la kutetea maslahi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Huyu alifanya kazi kubwa sana katika mitandao ya kijamii hasa facebook hadi akaanzisha ukurasa wa LIGI KUU TANZANIA kwenye mtandao huo wa kijamii wa facebook, lengo kubwa likiwa ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa soka kujadili mustakabali wa kulikomboa soka letu.
Jambo la kushangaza, leo amebadilika anapambania maslahi ya kibarua chake, tulitegemea Patrick atuonyeshe mkataba uliosainiwa kati ya Azam na TFF au Kamati ya Ligi kuwaruhusu kuonyesha LIVE michezo yao ya nyumbani badala yake anaweka nguvu kubwa katika kukanusha kile tulichokiandika awali.
Anaenda mbali zaidi kwa kukiri kwamba, Azam imekuwa ikilipa Sh. 1 milioni kwa timu inazocheza nazo ili mechi zao zionyeshwe live kutoka Chamazi.
Je, Patrick anashindwaje kuweka wazi makubaliano ya kuonyesha mechi hizo live ambayo yamebarikiwa na TFF na Kamati ya Ligi?
Je, zile harakati zake za kutaka kuleta maendeleo katika soka la Tanzania sasa zimeishia wapi? Na anadhani kuipa Sh. 1 milioni timu ambayo haina chanzo kingine cha mapato ndiyo kuisaidia huku timu yake ikipata ‘ mileage ’ kubwa na kutengeneza faida kubwa kuliko timu pinzani.
Kama utagundua, mechi kadhaa za Azam FC zimekuwa zikionyeshwa ‘live’ kwenye Uwanja wa Chamazi kwa kile tunachodhani ni bila kuzingatia baadhi ya mambo muhimu ikiwemo timu pinzani kulipwa haki za matangazo hayo inavyopaswa.
MECHI ZINAONYESHWA TFF HAIJUI
Baada ya mjadala kuanzishwa na mtandao huu, jana katika kipindi cha Sports Round Up cha redio Clouds FM, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi aliweka wazi jinsi haki za matangazo ya live zinavyotakiwa kuwa hata kama timu itahitaji kufanya hivyo.
Karia anasema, TFF ndiyo yenye haki zote za kuonyesha mechi live na ndicho chombo kinachoweza kuruhusu hali hiyo. TFF huwasiliana na kamati ya ligi sambamba na klabu husika ili kukubaliana juu ya maslahi ya kuonyesha mechi live.
Bosi huyo wa kamati ya ligi, anasema yeye hafahamu lolote juu ya mechi hizo kuonyeshwa live kwa kuwa alikuwa safarini na akaelekeza TFF kuulizwa kwa ufafanuzi zaidi.
Mkurugenzi wa masoko wa TFF, Jimmy Kabwe alipotafutwa na kipindi hicho, alisema hana taarifa zozote za baadhi ya michezo ya ligi kuu ya VODACOM inayoihusu AZAM FC kuonyeshwa LIVE na akaagiza waulizwe Azam Fc wenyewe au kamati ya ligi.
MASWALI TATA
Kama mwenyekiti wa kamati ya ligi ndugu Wallace Karia hajui chochote kinachohusiana na baadhi ya michezo ya Azam kuonyeshwa LIVE, Mkurugenzi wa masoko wa TFF Ndugu Jimmy Kabwe naye hana taarifa hii ina maana kwamba, mechi hizo zilionyeshwa kwa kujichukulia haki zote bila kufuata taratibu zinazopaswa?
Swali, kina nani wanahusika kwenye hili dili la kuzionyesha LIVE baadhi ya mechi zinazoihusu Azam Fc ?
SI VYEMA KUTUMIA UDHAIFU
Mechi nyingi za timu ambazo hazina wapenzi wengi kiukweli huwa hazipati watazamaji wengi, mara nyingi hupata mgao wa fedha za kiingilio cha milangoni kisichozidi Sh. 100,000. Sasa Azam inapotaka kuonyesha mechi live, kisha ikailipa klabu hiyo Sh. 1 milioni inaweza kuwa kweli inaisaidia klabu hiyo, lakini mantiki yote ya haki za live inafutika.
‘Coverage’ ambayo Azam itaipata kupitia mechi hiyo, haiendani na thamani ya fedha inayotoa kwa klabu pinzani zinazokubali kuonyeshwa live.
Hata hivyo, Sh. 1 milioni au hata Sh. 2 milioni inayoelezwa kuisaidia timu kutatua matatizo yake si mali kitu kuendana na gharama halisi za timu hizo.
Kiasi hiki cha fedha ni kidogo mno na haki ya timu ya kuonyeshwa live, ndiyo maana Yanga ilikataa kulipwa Sh. 10 milioni ili mechi yake na Azam ionyeshwe live.
STAR TV INALIPWA NA AZAM
Azam kwa kuzingatia kwamba inahitaji zaidi kutangaza bidhaa zake kupitia timu yake ya soka, imelazimika kuwa inailipa StarTV kiasi cha fedha kisichopungua Sh. 5 milioni ili mechi yake moja iweze kurushwa live na kituo hicho.
STAR TV kama chombo cha kutoa huduma hawana lawama katika hili,
“Azam huwa wanatulipa ili tuweze kuonyesha mechi zao moja kwa moja. Kwa kweli mambo yanakwenda vizuri maana kwao inawasaidia kwa kujitangaza zaidi na sisi tunaingiza fedha kupitia matangazo hayo kuwa yamelipiwa na wao siyo sisi kuwalipa wao,” kilisema chanzo chetu kutoka StarTV.
Kwa kauli hii, ina maana StarTV haifanyi mazungumzo na klabu inayocheza Chamazi na Azam bali jukumu hilo linabaki kwa Azam wenyewe na klabu husika. Hapa kuna tatizo kwani, Azam haina haki ya 100% ya kurusha live mechi zake zinazochezwa Chamazi hata kama itakuwa mwenyeji.
AZAM FC IFUATE TARATIBU…
Meneja wa Azam Fc Patrick Kahemele alipohojiwa na mwandishi wa blog hii, alisema kila mchezo wao unapokaribia hufanya mawasiliano na StarTV kisha kuwalipa kiasi cha fedha kisichopungua Sh. 5 milioni na mechi zao kuonyeshwa live.
“Sisi tunazungumza na StarsTV kisha tunawalipa gharama za kuonyesha mechi live, ambazo huwa kuanzia Sh. 5 milioni, bada ya hapo mechi inachezwa,” alisema Kahemele.
Japokuwa Azam imekiri kukubaliana na klabu husika, lakini sidhani kama ni sahihi kwasababu hakuna kitu hicho kinapaswa kufanywa na klabu zote halafu Azam ikawa imenunua haki za matangazo ya luninga japokuwa itakuwa ngumu kufanya hivyo kwa kuwa haina kituo cha luninga kwasasa.
YANGA ILIVYOKATAA MTEGO WA AZAM
Jumamosi Februari 23, 2013, Yanga ilicheza na Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Azam ilitaka mchezo huo uonyeshwe live na kulipa Yanga Sh. 10 milioni, lakini Yanga walikataa.
Katika mchezo huo ulioisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Haruna Niyonzima, mashabiki zaidi ya 36,000 waliingia uwanjani na kuingiza kiasi cha Sh. 250 milioni.
Yanga walikuwa wajanja zaidi kwa kuiona thamani yao na kukataa kiasi kidogo cha Sh. 10 milioni ambacho walitaka kulipwa ili mechi yao irushwe live.
VIONGOZI HAWAJUHI HAKI ZA KLABU ZAO
Mara kadhaa unaweza kwenda uwanjani na kukuta mambo yanatendeka kinyume na matakwa au kanuni zinavyotaka. Mfano halisi ni hili la matangazo ya live.
Klabu inaweza kufika uwanjani na kukuta mechi inaonyeshwa live na wasiwe na wasiwasi wowote bila kujua kama wanapoteza haki yao ya kimsingi siku hiyo. Nayo ni kulipwa kwa kitendo cha wao kuonekana moja kwa moja.
Kote duniani na hata hapa bara, mechi yoyote ya live ni lazima timu zote mbili zilipwe haki zao tena kwa makubaliano maalum. Hapo kila timu itaangalia thamani yake na kukubaliana na fedha wanayotaka kulipwa.
Kwa Ligi Kuu ya Kenya, timu zote hupata kiasi kisichopungua Sh. 150 milioni (kwa thamani ya fedha ya Tanzania) kutokana na kituo cha Supersport kuonyesha mechi zao live. Hicho ni kiasi kikubwa katika kuiendesha klabu na kuweza kushindana kikamilifu.
Kumbuka hata wakati ule GTV ilipokuja nchini na kuingia mkataba wa kuonyesha live baadhi ya mechi za ligi kuu, kila klabu iliambulia kiasi cha fedha kwa kitendo chao cha kuonekana live.
MSIMAMO WA MTANDAO HUU
Tunaipongeza Azam kwa kutaka kuonyesha live mechi zake zote inazocheza kwenye Uwanja wa Chamazi, lakini ni muhimu kwao kufuata taratibu na kuacha kudili na watu binafsi wenye kutaka kujinufaisha wao.
Kama kuna mkataba umesainiwa kwa kufuata taratibu baina ya taasisi husika kwa ajili ya kuonyesha live michezo ya ligi kuu ya VODACOM basi uwekwe wazi kwa wadau.
Viongozi wa klabu zote za ligi kuu kuacha kuona kila kitu ni kawaida kutokea kwani kuna wakati wanapoteza haki zao za msingi na kujikuta wakiendelea kulia na ukata wakati mianya ya fedha wanaiacha bila kujielewa.
Tunaiomba kamati ya ligi kufanya kazi kikamilifu kwa kuzingatia haki na kanuni za mambo yote yahusuyo ligi hiyo. Pia ifanye kazi kwa kwenda viwanjani na kusimamia mambo yote ya msingi kama haya ya baadhi ya mechi kuonyeshwa live.
Tunasisitiza habari hii haiusiani na jambo lolote kwa mtu binafsi, bali ni harakati za kutaka kuonyesha mpira wetu unasonga mbele na isifikiriwe tofauti.
Tuna imani hiki tulichokiandika kitafanyiwa kazi na kila upande uweze kupata haki zake stahiki.
Clouds Television wangekuwa wanarusha matangazo hayo live " ungeandika" uliyoyaandika?
ReplyDeleteViongozi hawa wa soka ndio watambue thamani zao? bado sana shafii, na usiombe watokee kwenye hizo tv wanaenda onyesha wake zao nyumbani, nafikiri hata hizo milioni moja wanazotoa, zinachukuliwa na viongozi kadhaa. Na kama wanatoa basi wanwapendelea tu wao hata bure poa tu, si wanaonekana bwana. Siku moja nikiwa ofisini nikaletewa barua kuteuliwa kuwa meneja wa timu fulani ligi kuu, nilipowauliza majukumu yangu ni yapi, maana kit manager yupo na mimi siwezi fanya shughuli hizo, wakaniambia utazijua tu humo humo, nikawaambia hawajijui wanakurupuka tu. wakajipange ndio waje sana sana wakawa wanakuja siku za mechi kutaka hela za maandalizi ya mechi, ukienda uwanjani utawakuta wamejezana milangoni, wanakagua tiketi mwisho mgawo wa 100,000. tutafika kweli?
ReplyDeleteShaffih sasa na wewe umeanza unafiki katika soka..mimi nilikua nakuamini sana sasa naona unaelekea pabaya...kwani hizo timu zinazocheza na Azam hazijui kama zinazulumiwa????Mbona yanga wao walikataa???basi na vilabu vingine wakatae...Tatizo kubwa vilabu vyetu havina pesa hata hiyo milioni moja wanayopata ni kubwa mno kuliko kuambulia zero
ReplyDeleteHawa viongozi wa TFF nao bure kabisa.Yaani mechi watanzania wote tunaziona wao wanasema hawajui chochote?! Hapa watu wanataka kukwepa majukumu yao kama kawaida siku zote. Unajua huwezi kuwalaumu tu Azam, kama wanaotakiwa kusimamia utaratibu hawajui na hawataki kuonyesha hawajui, kwa nini Azam wasijiweke utaratibu wao, hasa ukizingatia kuwa kuna makubaliano na upande wa pili (kama wenyewe walivyojieleza?) Kama kila mmoja hatataka kutekeleza majukumu yake ni vigumu sana kufika tunapotakiwa kuwa..
ReplyDeleteBongo duluma kila idara ukiwa huna kitu na hujitambui utadhulumiwa mpaka unakufa hao wote wanaodhulimiwa ni kutokana na udhaifu wao laiti kama wangesema hatutki m1 tupeni m3 wangepewa tu ila kutoajiamini kwao na kuona watakosa kabisa na ile misemo yao ya kizamani " bora kuwa nacho kuliko kukosa kabisa" ndio huwaponza.
ReplyDeletemawazo mazuri sana shafih, ila waswas wangu ni juu ya nia yako ya kuandika hayo yote maana nyinyi watu wa CLOUDS MEDIA GROUP huwa mnaangalia maslahi yenu sehemu ambayo hamna maslai mtapiga fitna mpaka jambo lishindwe, BADILIKENI, HATUENDI HIVYO.
ReplyDeletejamani milioni moja ya haki ya kuonyeshwa kwenye tv na elfu 90 za mgao wa gate collection lipi bora shaffih?, nashauri timu endeleeni kukubaliana na azam ngalau mujihakikishie hiyo milioni moja big azam.
ReplyDelete