Na Baraka Mpenja
Maafande wa jeshi la magereza,
Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya wamejigamba kuwatandika wana lamba lamba,
klabu ya Azam fc katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara utaopigwa kesho kutwa
(Machi 27) uwanja wa Azam Complex, Mbande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza leo hii, Katibu mkuu wa
Prisons Sadick Jumbe amesema maandalizi yanakwenda vizuri na kocha mkuu Jumanne
Chale anamalizia programu yake ya mazoezi kabla ya kuwavaa Azam nyumbani kwao.
Jumbe alisema kikosi chao kipo safi
kwa asilimia zote kwani mpaka sasa hakuna mchezaji ambaye yupo hatarini kuukosa
mchezo huo.
“Tunaenda kupambana na Azam fc ambao
wametoka kushinda ugenini kombe la shirikisho dhidi ya Barrack Young Controller
II ya Liberia, hii imewapa morali kubwa, lakini tutapambana kufa na kupona ili
kupata ushindi wa ugenini”. Jumbe alisema.
Katibu huyo wa Prisons aliongeza
kuwa, kikosi chake kimekaa maeneo ya Ukongo kwa zaidi ya wiki moja kikitokea
mjini Arusha ambako kilifungwa 1-0 na wapiga kwata wenzao JKT Oljoro, mchezo wa
ligi kuu.
Jumbe alisema wakiwa Ukonga wamecheza
mechi za kujipima uwezo na African Lyon na kuwafunga 1-0, wakacheza na timu ya
wizara ya ndani na kutoka nayo sare ya 2-2 na wakashuka dimbani dhidi Ukonga
united.
“Tunakumbuka mchezo wa mzunguko wa
kwanza tukiwa nyumbani Sokonne, tulilazimisha suluhu na Azam Fc, lakini safari
hii tunahitaji kuwadhihirishia watanzania kuwa uwezo wa kuwafunga tunao”. Jumbe
alitamba.
Akizungumzia suala la mchezaji wao wa
zamani, David Mwantika, anayekipiga Azam kwa sasa kuukosa mchezo huo kutokana na kuoneshwa kadi
nyekundu mchezo uliopita dhidi ya Polisi Moro uliomalizika kwa sare ya 1-1,
alisema ni nafasi nzuri kwao kwani nyota huyo anawafahamu sana washambuliaji
wao.
Wakati huo huo Azam fc imeingia kambini
rasmi leo hii baada ya nyota wake kurejea wakitokea kuitumikia timu ya taifa
hapo jana dhidi ya simba ya Milima ya Atlas, timu ya taifa ya Morroco na
kushinda 3-1.
Akizungumza leo Afisa habari wa Azam
fc, Jafar Idd Maganga amesema wanamshukuru mungu kwani mpaka leo hii hawana
mchezaji majeruhi baada ya mlinzi wao Hajji Nuhu kupona.
Maganga alisema wanatarajia mchezo huo kuwa wa vuta ni kuvute , lakini
wanajiandaa vizuri kuhakikisha wanashinda na kujiweka vizuri katika mbio za
kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2012/2013.
Msemaji huyo amesema mechi mbili watakazo cheza dhid ya Prisons kesho kutwa na Ruvu shooting mwishoni mwa wiki zitawasaidia kujiweka sawa kabla ya mechi ya marudiano na Barrack Young Controller II ya Liberia katika Kombe la Shirikisho aprili 6 mwaka huu ndani ya uwanja wa taifa.
Azam fc wapo katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi wakiwa na pointi
37 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 48 huku Mnyama simba akiwa nafasi ya tatu
na pointi zake 34.
Prisons wapo nafasi ya kumi wakiwa na pointi 20 kibindoni na wanapambana
kuukwepa mkasi wa kurejea ligi daraja la kwanza kwa kuzipisha timu mpya tatu,
Mbeya city ya Mbeya, Rhino Rangers ya Tabora pamoja na Ashant United
zilizopanda kucheza ligi kuu msimu ujao.
Kabla ya mchezo huo wa keshokutwa , Azam fc walicheza na Barrack fc ya
Liberia na kuishindi 2-1 , wakati Prisons wametokea Arusha walipofungwa 1-0 na
maafande wenzao wa JKT Oljoro.
No comments:
Post a Comment