Kibaden akiwa baadhi ya wachezaji wa Simba |
Na Baraka Mpenja
Wakata miwa wa Kaitaba, Kagera sugar,
wametamba kuwaadabisha mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara, wekundu wa
Msimbazi Simba kwenye mchezo wa ligi kuu unaotarajiwa kupigwa keshokutwa katika
dimba la kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka
Kaitaba, Kocha mkuu wa kagera sugar, Abdallah King Kibaden “Mputa” amesema
maandalizi yanakwenda vizuri na mpaka sasa hakuna majeruhi yeyote.
Kibaden alisema alama tatu za mchezo
huo zinahitajika sana, hivyo anawaeleza wachezaji wake kuwakabili Simba kwa tahadhari
kubwa kutokana na hali halisi ya Simba kwa sasa.
“Nimefarijika sana kusikia Simba
wamefanya maamuzi ya kuwaamini vijana wao wadogo kucheza mechi zilizosalia,
binafsi nawafahamu sana vijana hawa, nimekaa nao na kuwafundisha pale Simba,
ninachokifanya sasa ni kuandaa mbinu za kuwaburuza”. Kibaden alisema.
Mchezaji huyo wa zamani wa taifa
stars , simba na kocha wa klabu hiyo,
aliongeza kuwa kwa sasa klabu yake inahitaji kujiweka nafasi nzuri katika
msimamo wa ligi, hivyo kila mechi ndani ya uwanja wake wa nyumbani ni lazima
jitihada zifanyike kupata alama tatu muhimu.
Kibaden alisisitiza kuwa mechi ya
ngwe ya kwanza wakicheza uwanja wa taifa Dar es Salaam waliwabana wapinzani wao
na kulazimisha sare ya 2-2, na sasa ni nafasi yao kujaribu bahati yao wakiwa
mbele ya mashabiki wao mjini Bukoba.
“Nimewajenga wachezaji wangu
kisaikolojia, kwa sasa nipo hatua za mwisho kupata kikosi cha vita mbele ya Simba,
vijana wananielewa vizuri na wapo katika morali ya hali ya juu”. Kibaden
alisema.
Akizungumzia hali ya hewa ya Kaitaba,
Kibaden alisema kuna mvua za hapa na pale, lakini wachezaji wake wamezoea na hadhani
kama itaathiri mchezo wa kesho kutwa.
Kwa upande wa wapinzani wa kagera
sugar katika mchezo wa keshokutwa, wekundu wa Msimbazi Simba, leo wachezaji
watano kati ya sita waliokuwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania taifa
stars kilichoshuka dimbani jana na Morroco na kuwafunga 3-1 wameondoka kuungana
na wenzao mjini Bukoba.
Afisa habari wa klabu ya simba Ezekiel
Kamwaga, alisema wachezaji hao ni mlinda Mlango namba moja wa stars na nahodha,
Juma Kaseja, mabeki Masoud Nassor “Cholo”, Shomary Kapombe na viungo ni Amri
Athman Kiemba na Mrisho Khalfan Ngassa “Anko”.
Kamwaga alisema Mwinyi Kazimoto
ameaachwa kwani hayupo kwenye mipango ya Kocha Mfaransa Patrick Liewig
akisaidiwa na Jamhuri Kihwelu Julio na Mganda Moses Basena.
Wachezaji wa Simba SC ambao
hawakuwamo Katika kikosi chaTaifa Stars,
wapo Bukoba tangu jana kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi Kuu.
Aidha, Kamwaga alisema wachezaji
wengine wawili waliokuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, The Cranes
kilichopepetana na Liberia jana, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde nao
wataungana na timu wakitokea uganda moja kwa moja Bukoba.
Wekundu wa Msimbazi wanaoonekana kuweka rehani
ubingwa wao walioutwaa msimu uliopita kwani wanazidiwa pointi 14 na wapinzani
wao wa jadi, ambao ni vinara, klabu ya Yanga inayoongoza kwa pointi 48.
Simba wanapigana kufa na kupona kupata angalau nafasi ya pili kwa kuwapiku
waoka mikate wa Azam Fc ambao wapo
katika nafasi hiyo kwa pointi zake 37. Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 34.
No comments:
Post a Comment