Catenaccio ni mfumo wa ukabaji wa soka ambao umejizolea umaarufu sana kwa jinsi ulivyofanya kazi kwa ufanisi.
Catenaccio ni neno la kitaliano lenya maana ya BOLT ambayo inafananishwa na dhana ya kubana mlango kwa kutumia bolt pasipo kuruhusu upenyo wowote ule.
Pamoja na ukweli kuwa neno hilo ni la kitaliano, makazi au mizizi yake halisi yako nchini Uswisi ambapo dhana hii ilianzishwa na Karl Rappan. Huu ulikuwa ni mfumo ambao watu wanaopenda burudani ya soka waliupinga kwa jinsi ulivyokuwa ukifanya michezo ionekane hovyo.
Rappan alianzisha mfumo huu akiwa na timu ambayo ilikuwa na wachezaji ‘semi professional’, ambapo mfumo wa Catenaccio uliwapa nafasi ya kushindana na wachezaji wenye nguvu na uwezo mkubwa kuliko vijana wa Rappan.
Catennacio mwanzoni ulitumika kwa timu ndogo ndogo kwa lengo la kuzikera timu kubwa pale wakati timu hizo zilipokutana, ambapo timu hizo ndogo zingefunga mwanya wa kuelekea langoni mwao kwa malengo ya kujihami na hivyo kuzinyima timu hizo ushindi mwepesi.
Helenio Hererra |
MWANZO WAKE
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Rappan ndiye aliyeanzisha mfumo huu au dhana ya Catenaccio ambayo Wafaransa walikuwa wakiiita Verrou. Mwanzo wa mfumo huu ni kitendo cha beki wake wa kati kupitwa kwa kasi na mshambuliaji wa timu pinzani na timu ya Rappan ikafungwa bao la kizembe. Kuanzia hapo, Rappan akabuni mfumo huu wa kukaba wa Catenaccio.
Kuondokana na mabeki kupitwa kizembe, Rappan aliamua kuchezesha beki wa ziada nyuma ya mabeki, jukumu la mtu huyu lilikuwa kumzuia mshambuliaji ambaye tayari amewapita mabeki. Hivi ndivyo jinsi nafasi ya ‘Libero’ ilivyozaliwa, na kwa hivyo mfumo wa Verrou au Bolt ya mlango kwa Wafaransa ikazaliwa.
Rappan aliamini kuwa, kuna njia mbili za kucheza mpira. KWANZA, unawapanga wacheza 11 wenye uwezo binafsi na wangekufanyia kazi kwa ufasaha, ufanisi na burudani pia.
PILI, chukua wachezaji 11 wa kawaida halafu wafundishe au wapike jinsi ya kucheza katika mfumo ulioeleweka miongoni mwao. Mfumo wa ushindi ambao lengo lake ni kutumia uwezo mdogo walionao kwa pamoja huku kila mtu akichangia kidogo alichonacho.
Rappan alifanikiwa kwenye hili la pili akiwa na timu ya watu wasio wachezaji kwa asilimia mia moja kwenye timu yake ya kwanza kufundisha ya Servette ambako alitwaa mataji mawili ya ligi . Baada ya hapo Rappan alitwaa mataji matano ya ligi na saba akiwa na Grasshoppers.
MFUMO
MFUMO W-M |
Mfumo wa Verrou au Catenaccio ulitumika kwa kuendeleza mfumo wa 2-3-5 ambapo lengo kuu lilikuwa kuhakikisha safu ya ulinzi inafanya kazi kwa nguvu. Wing Halfs ambao walikuwa wanacheza kwenye mfumo wa 2-3-5, walirudishwa nyuma na kuongeza ukuta wa mabeki ambao ulifikia idadi ya watu wanne.
Hata hivyo, mmoja wa mabeki wa kati alirudishwa kucheza katikati ya mabeki wenzie na kipa, hivyo kujenga kuta mbili za ulinzi. Katika kuleta uwiano kwenye safu ya kiungo, washambuliaji wa ndani walisogezwa pembeni zaidi kama ilivyokuwa kwenye mfumo wa W-M.
Beki wa kati ambaye alirejeshwa nyuma kucheza katikati ya mabeki wenzie na kipa, alikuwa akifahamika kama ‘VEROULLER’ au Libero. Kazi yake kubwa ilikuwa kuhakikisha mabeki hawapitwi na pia kucheza mipira mirefu iliyokuwa inachezwa na kuelekezwa nyuma au juu ya mstari wa mabeki.
Katika ‘scenario’ nyingine, Libero alimkaba mshambuliaji wa timu pinzani na hivyo kuua shambulizi. Mfumo huu ulifanya kazi vizuri sana kwa Rappan na ndio maana alipata mafanikio makubwa nchini Uswisi.
KUKUA KWAKE
Pamoja na kiwango kikubwa cha mafanikio ndani ya Uswisi, mfumo huu haukufahamika sana sehemu nyingine duniani. Bara la Ulaya liliuona kwa mara ya kwanza wakati Rappan alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Uswisi.
Mafanikio yake kwenye ngazi ya klabu yalimfanya apewe kazi ya kuifundisha timu ya taifa mwaka 1937 huku timu ikiwa inajiandaa kwa Kombe la Dunia 1938. Kwenye michuano hiyo, Uswisi ilikuwa inaonekana ndio timu dhaifu kuliko zote.
Rappan alitumia mfumo wake wa Verrou na alipata mafanikio kiasi chake. Kabla ya michuano kuanza, England ilifungwa na Uswisi kwenye mechi ya kirafiki. Kwenye michuano yenyewe, Uswisi iliifunga Ujerumani kabla ya kukubali kichapo mbele ya Hungary.
Mafanikio haya yalikuwa ishara tosha ya bara la Ulaya kufahamu nini maana ya Catenaccio au Verrou. Makocha wa Ulaya hasa Italia walianza kuupenda mfumo huu. Gipo Viani na Nereo Rocco ndiyo walikuwa wa kwanza kuutumia Italia.
No comments:
Post a Comment