SHIRIKISHO
la Kimaifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeahirisha uchaguzi wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mkanganyiko uliojitokeza
katika mchakato wa uchaguzi huo.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo
mchana (Februari 19 mwaka huu), Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema FIFA
imetuma barua ikiagiza mchakato wa uchaguzi usimame baada ya kupata
malalamiko.
Amesema kutokana na mkanganyiko huo, FIFA katika barua yake ya leo (Februari 19 mwaka huu- imeambatanishwa)
imeagiza mkutano wa uchaguzi wa TFF ambao awali ulipangwa kufanyika
Februari 24 mwaka huu uahirishwe hadi hapo itakapotuma ujumbe wake
nchini.
Ujumbe
huo wa FIFA unatarajiwa kufika nchini katikati ya mwezi ujao (Machi)
ambapo utafanya tathimini ya hali hivyo, kutuma ripoti yake katika
shirikisho hilo na baadaye kutoa mwongozo wa nini kifanyike.
Rais
Tenga amewaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa usumbufu
uliojitokeza kutokana na uamuzi huo wa FIFA, hivyo kwa sasa hakutakuwa
tena na mkutano huo mpaka hapo watakapopewa taarifa nyingi.
Amesema
TFF inakaribisha kwa mikono miwili uamuzi huo wa FIFA kwa sababu ni
chombo ambacho cha juu kimpira duniani, na hatua hiyo ina lengo la
kuhakikisha kuwa kila mhusika katika mchakato huo wa uchaguzi anapata
haki yake.
“Nia
yetu ni kuona watu wanatendewa haki, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli.
Hivyo wahusika (waathirika) wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja
zao ili FIFA wakifika wawasikilize, wapate maelezo ya kina kuhusu
utaratibu na malalamiko yaliyotolewa,” alisema Tenga.
Rais
Tenga amesema timu hiyo ya FIFA itakapofika yenyewe ndiyo itakayopanga
izungumze na nani kwa wakati gani, hivyo ni vizuri waathirika na vyombo
vyote vilivyohusika na mchakato wa uchaguzi wakajiandaa.
Amesema
ilikuwa ni muhimu suala hili likatatuliwa katika ngazi ya FIFA kwa
lengo la kuhakikisha uchaguzi utakapofanyika TFF inaendelea kuwa chombo
kimoja badala ya kurudi katika migogoro iliyokuwepo huko nyuma.
“Nataka
tubakie kama tulivyokuwa. Malumbano yaishe. Pangeni hoja, wakija hao
waheshimiwa (FIFA) muwaambie. FIFA ni chombo cha juu, nafurahi
wamekubali kuingia katika hili, kwani wana shughuli nyingi wangeweza
kukataa,” amesema.
Kuhusu
fursa ya kufanya marejeo (review) kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
inayoongozwa na Idd Mtiginjola ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga
amesema kwa vile hicho ndicho chombo cha mwisho nchini katika masuala ya
uchaguzi alishauriwa kuwa kingeweza kufanya review.
“Kwa
vile hakuna chombo kingine, nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya review.
Katika utaratibu wa kutoa haki, uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa
sababu. Nilidhani hilo linawezekana, kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo.
Kwa hili uamuzi wa Mtiginjola ni sahihi,” amesema Rais Tenga.
Kamati
ya Mtiginjola iliyokutana jana (Februari 18 mwaka huu) ilitupa maombi
ya review yaliyowasilishwa mbele yake na waombaji uongozi watano kwa
vile hakuna kipengele chochote kwenye Katiba ya TFF na Kanuni za
Uchaguzi kinachotoa fursa hiyo.
Waombaji
hao walikuwa Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na
Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa
Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wengine
ni walioomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao
kwenye mabano; Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi
(Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).
No comments:
Post a Comment