Yanga na Mtibwa Sugar zinapambana kesho (Februari 2 mwaka huu) katika moja ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha ndiye atakayechezesha mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani wakati Yanga ikiongoza ligi hiyo, wapinzani wao Mtibwa Sugar katika mechi iliyopita walilala mbele ya Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa ligi kwa sasa.
Polisi Morogoro itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro wakati Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ruvu Shooting inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa.
Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi mbili. Simba itaumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Tanzania Prisons ikiikabili Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
VILLA SQUAD, MORO UNITED UWANJANI FDL
Villa Squad na Moro United zinaumana kesho (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza mzunguko wa lala salama.
Kundi A litakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Mechi nyingine ya Kundi B itakuwa Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani. Kundi C ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
No comments:
Post a Comment