DAKTARI wa Yanga, Nassoro Matuzya amethibitisha kuwa Frank Domayo yupo fiti kuikabili Mtibwa Sugar kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jambo ambalo linamaanisha kuwa atasimama katika nafasi ya kiungo akishirikiana na Athuman Iddi 'Chuji'.
Domayo alishindwa kucheza pambano la kwanza dhidi ya Prisons ya Mbeya wikiendi iliyopita katika dakika za mwisho kutokana na kuugua ghafla akiwa tayari amepangwa kwenye kikosi cha wachezaji 11 watakaoanza mchezo huo. Yanga ilishinda mabao 3-1.
Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alilazimika kufanya mabadiliko na kumpanga Nurdin Bakari badala ya Domayo.
Hata hivyo, Nurdin aliimudu vizuri nafasi ya kiungo akishirikiana na Athuman Iddi 'Chuji' kuwalisha mipira mastraika Jerry Tegete na Mrundi Didier Kavumbagu.
Pia, Nurdin alitoa pasi ya bao la tatu, lililozamishwa na Jerry Tegete kama ilivyokuwa kwa Chuji aliyepiga pasi ndefu kwa Simon Msuva aliyepiga krosi iliyofungwa na Tegete aliyepachika mabao mawili na jingine likifungwa na Mbuyu Twite kwa shuti kali.
Matuzya aliiambia tovuti hii kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama jijini Dar es Salaam kuwa hali ya Domayo kwa sasa imeimarika kwa asilimia kubwa isipokuwa uamuzi unabaki kwa kocha kumchezesha.
"Vipimo vilionyesha kuwa Domayo ana malaria," alisema Matuzya aliyerithi mikoba ya Juma Sufian aliyetupiwa virago na uongozi.
Kwa upande wake, kocha Brandts amefurahishwa kurejea kwa kiungo huyo, kwani anaamini ni mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga hasa wakati huu wakiwa kwenye harakati za kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Nafikiri Domayo ni mchezaji muhimu kwetu. Kila mtu analijua hilo. Mchango wake unahitajika sana, hasa kipindi hiki tukiwa kwenye mbio za kuwania taji la ligi," alisisitiza.
No comments:
Post a Comment