Search This Blog

Tuesday, February 5, 2013

MSUVA; STARS v CAMEROON NI MECHI KUBWA KWA KILA TIMU



 Kitendo cha kuifunga timu ya taifa ya Cameroon, kesho siyo tu kitaipaisha Tanzania katika ' renki' za FIFA baadae, Mwezi huu bali kitakuwa ni ' malipo' ya kichapo cha mabao 2-1 ambacho, Stars ilikipata miaka mitatu iliyopita kutoka kwa ' Indomitable lions' jijini, Younde. Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuwavaa, Morocco katika mchezo wa kufuzu kwa fainali zijazo za kombe la dunia nchini, Brazil, Stars kesho  itaipata fursa nzuri ya kujiandaa kwa kucheza timu ya taifa ya Cameroon katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.
" Ni mechi tafu, tumejiandaa kukabiliana nao" anasema kiungo wa pembeni wa timu hiyo, Saimon Msuva alipokuwa akizungumza na mwandishi, Baraka Mbolembole siku ya jumatatu.
 " Hata wao wamejiandaa vizuri na watapata maandalizi mazuri. Tunatakiwa kupambana wote kwa pamoja kama wachezaji na kuona kitakachotokea" anaongeza, " Umoja wetu upo juu na tunadhamira ya kupambana ili tujiweke katika mazingira mazuri ya kuwakabili, Morocco mana ni mechi kubwa hivyo maandalizi yanatakiwa kwani ndiyo yatakayotubeba".
Cameroon ambayo ilianza kutua nchini kwa mafungu, huku fungu la mwisho likiwa limetua leo nchini,   itaongozwa na mshambulia wa zamani wa Barcelona ya Hispania na Inter Milan ya Italia, ambaye ni nahodha wa kikosi hicho, Samuel Eto'o, kiungo wa Barcelona, Alex Song, mlinzi wa Tottenham ya England, Benoit Assou Ekkoto na wengine kadhaa wanaofanya vizuri katika ligi kubwa za Ulaya.
 " Kucheza dhidi ya mchezaji kama, Ekkoto kutanifanya kujiamini zaidi, ni vizuri kucheza dhidi ya wachezaji wakubwa ni vizuri kwa mchezaji kijana' anasema, Msuva ambaye ametokea kuaminiwa sana na kocha , Kim Poulsen. " Juhudi zangu zimenifanya kufika mahali hapa( Stars). Kila kitu ni mazoezi na nimekuwa nikizingati mazoezi na kufuata maelekezo ya makocha wangu" anasema, Msuva anayeichezea klabu ya Yanga.
Stars iliifunga timu ya Taifa ya Zambia mwishoni mwa mwezi disemba mwaka jana katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki na ikapoteza katika mchezo dhidi ya Ethiopia, mapema januari mwaka huu, lakini michezo yote hiyo ilikuwa nje ya kalenda ya FIFA, sasa wataikabili, Cameroon katika mchezo huo unaopigwa katika kalenda ya FIFA. Kuna wakati imekuwa ikicheza mpira mzuri na mara nyingine hucheza soka bovu na wachezaji kuonekana kushindwa kufuata maelekezo ya mfumo unaokuwa unatumiwa.
" Ni kazi ya kocha" anasema, Msuva, akizungumzia mifumo inayotumiwa na Kim Poulsen. " Wachezaji wengi wa Kitanzania tumezoea kucheza mfumo wa 4-4-2. Mimi naweza kusema nakuwa huru kucheza katika mfumo wa aina yoyote, lakini ule wa 4-4-2 umekuwa rahisi kwa wachezaji wengi wa Kitanzania" anasema, Msuva ambaye anapocheza huwa anakimbia huku akitazama sana chini.
 " Kila kitu kina mwisho wake. Nitabadilika tu, kwani hata mtoto mchanga anapozaliwa hatembei, anaanza kutambaa na kisha ndiyo anaanza kutembea, naamini tatizo hilo litakwisha tu". Wachezaji kama Shaaban Nditi na Athuman Idd ni wa muda mrefu katika timu hiyo na hata kiumri wamesogea lakini wameendelea kuitwa kikosini na kocha, Kim. " Hakuna tatizo lolote kwenye timu hii ( Stars) Wachezaji wazoefu kama Chuji na Nditti wamekuwa wakitoa maelekezo kwa wachezaji vijana waliopo kama mimi na tumekuwa na mawazo yanayofanana

. Tatizo ni kwamba kwenye kikosi chetu ( Stars) kuna wachezaji wengi sana wachanga ambao wanahitaji kupewa uzoefu kutoka kwa wazoefu kama, Chuji na Nditti na hata nahodha, Juma Kaseja. Ni changamoto kubwa kwetu sisi makinda tunapokuwa benchi ama uwanjani, tumekuwa tukijufunza mengi kutoka kwao kwani wao tayari wameshacheza michezo mingi mikubwa na kizuri kwetu wamekuwa wakitusapoti na kutupa maelekezo mara kwa mara, pale tunapokosea wamekuwa wakituelekeza cha kufanya na pale tunapofanya vizuri wamekuwa wakitutia moyo zaidi" anasema, Msuva ambaye sasa ameingia katika changamoto kubwa ya kuwania nafasi na Hamis Mcha Hamis.
 " Majukumu yetu yapo palepale, tunatakiwa kuhakikisha kazi ya kocha wetu inakuwa rahisi, kocha ana mawazo yake na kila mtu anapambana aidha kuilinda namba yake kwenye kikosi au yule asiye na nafasi atapambana kuhakikisha anaipata" . Safu ya ulinzi ya Stars imekuwa ikilegalega na kuruhusu mabao.  " Siyo kweli kuwa wa kulaumiwa ni mabeki tunatakiwa kucheza kama timu" alisema, Msuva na kuongeza
" Ulinzi ni kazi ya kila mtu uwanjani, kuanzia kwa Samatta hadi kwa Yondan, na tunatakiwa kulinda kama timu. Wakati mwingine tunatakiwa kusimama na kuhakikisha hatumwachii mtu mmoja majukumu ya timu akiyafanya mwenyewe" anasema mshambuliaji huyo wa vinara wa ligi kuu Tanzania Bara. Msuva alifanya vizuri katika michuano ya Challenge Cup huku nchini Uganda mwishoni mwa mwaka jana.
" Hivi sasa nimeanza kupata uzoefu wa kutosha. Naamini naweza kumaliza kazi niliyoianza". Akizungumzia tukio la " kushikana uchawi" klabuni kwake, Yanga ambalo lilitangazwa na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, Msuva anasema
" Ni kweli hilo lilitokea lakini mimi sikulifuatilia. Ilikuwa mazoezini mara ghafla tukaona hali ya kushikana na kurushiana maneno, sikufuatilia sana na sijui kilichotokea baada ya hapo tukaona kwenye magazeti kesho yake. Inawezekana ikawa kweli au isiwe kweli kwani kila mtu ana imani yake mwenyewe" anasema na kuongeza kuwa “ Nimetulia na klabu yangu na wala sifuatilii mambo hayo ( imani za kishirikina).

No comments:

Post a Comment