Search This Blog

Thursday, January 3, 2013

KUTOKA KUKATALIWA NA VILABU KIBAO ULAYA, MAJERUHI KUMUANDAMA MPAKA KUWA MRITHI WA DIDIER DROGBA CHELSEA - DEMBA BA FUNZO KWA WACHEZAJI WA KITANZANIA

Demba Ba yupo karibuni kutangazwa rasmi na Chelsea kuwa mchezaji mpya wa mabingwa hao wa ulaya, lakini haikuwa njia rahisi kwa kijana huyo ambayo alipata kukataliwa na vilabu vingi vikiwemo Barnsley na Watford wakati akihangaika kwa hali mali kuweza kupata mkataba.

Mshambuliaji huyo wa Senegal, 27, amefunga mabao 29 katika mechi 58 alizoichezea Newcastle na kuwa moja ya washambuliaji wanaovitoa udenda klabu nyingi sana duniani.

Ba alikuwa akikataliwa na timu nyingi tangu alipokuwa kinda akijaribu kuweza kupata mkataba wa soka la kulipwa. Majaribio aliyoyafanya na Lyon na Auxerre mwaka 2004 hakufanikiwa, lakini hakukata tamaa na hatimaye akadandia gari na rafiki zake na wakazamia kwenda huko England kujaribu bahati yake.

Walipofika England wakishuka kutoka kituo cha Folkstone hawakuwa hata na wazo lolote juu ya namna ya kuanza kukamilisha ndoto zao, BA akaishi kwenye hoteli mbalimbali na pia alifikia hatua ya kusihi kwenye vibaraza vya nyumba za rafiki zake aliokuwa akiwasiliana nao alipokuwa akifanya mipango ya kwenda England.

Rafiki mmoja kutoka Ufaransa, Gauthier Diafutua,  alikuwa akiichezea Watford kipindi hicho na akafanikiwa kuishawishi klabu yake kumpa nafasi BA ya kufanya majaribio lakini akaishia kupigwa chini.

Pia akapata bahati ya kupewa nafasi ya kufanya majaribio na Barnsley kwa wiki moja lakini pia akatoswa.

"Nilienda Barnsley na nikakaa kwenye hoteli ya kifahari. Klabu ililipa. Majaribio nilifanya lakini sikufanikiwa. Nilikuwa hotelini kwa wiki lakini likatokea tatizo lingine," Ba alisema kwenye mahojiano ya hivi karibuni.

 "Nilipotaka kuondoka, hoteli ikatuzuia ikisema klabu ililipia fedha za chumba tu na sio chakula, na sikuwa na fedha hivyo ikabidi niwasiliane na wakala mmoja ambaye alisaidia kwa kutuma £500 ikalipwa bill ya chakula, na cha ajabu katika siku zote hizo nilikuwa nashindia maji na crips."

 Ba alienda tena kwenye vilabu tofauti kuomba kufanya majaribio na akatoswa na vilabu kama vile Swansea na Gilligham na hatimaye akaamua kufungasha virago kurudi nchini Ufaransa alipoenda kujiunga na timu ya daraja la nne ya Rouen.

Pale alicheza kama mshambuliaji, lakini mwanzoni alianza kucheza kama kiungo wa ulinzi kabla ya kuamua kwamba afurahii kucheza nafasi hiyo, hivyo akarudi kucheza kama mshambuliaji na akaonyesha kwanini hakuwa anafurahia kucheza kama kiungo mkabaji, alifunga mabao 22 katika mechi 26 kabla ya kuhamia katika timu ya Ubelgiji iitwayo Mouscron. 

Balaa lake la kucheka na nyavu liliendelea na hatimaye akaitwa kwa mara ya kwanza kwenye timu ya taifa ya Senegal, na pia akaivutia klabu ya Hoffenheim, na mwaka 2007 Ba akawa njiani kwenda Ujerumani.

Ba aliendeleza rekodi yake nzuri ya kufunga, na akasaidia sana Hoffenheim kupanda mpaka Bundesliga na katika msimu wake wa kwanza wa Bundesliga akafunga mabao 14. Lakini, baada ya kukamilisha ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa, kitu kingine kikaanza kutishia ndoto yake ya kwenda kucheza nchini England.

Mwaka 2006, Ba alivunjika mguu wake wa kushoto mara mbili, matokeo yake ikahitajika kuwekewa kifaa maalum kwenye mguu ili uweze kukaa sawa. Kifaa hicho kikatolewa mwaka 2009 lakini wakati akifanyiwa upasuaji kuna kiungo kilichopo kwenye goti lake kikapata uharibifu.
Kilikuja kuwa kitu kikubwa kilimchomsumbua sana na kikasababisha afeli vipimo vya afya  na Stuttgart kabla ya uhamisho wake wa kwenda Stoke City mwezi January 2011 pia kushindikana kutokana na sababu hiyo hiyo.
  
Ba akaondoka Hoffenheim baada ya hapo na pamoja na matatizo yake ya majeruhi West Ham wakaamua kumsajili kwa dili la kulipwa kadri unavyocheza na akawa mmoja ya wachezaji waliopigana katika kujaribu timu hiyo isishuke daraja.
Ba akamaliza msimu akiwa mfungaji bora wa wagonga nyundo wa London, akiwa amecheza mechi 12 tu, lakini hakuweza kuinusuru timu hiyo kutoshuka daraja na hatimaye akawa amepata nafasi ya kujiunga na Newcastle kwa mkataba wa miaka 3.

Tangu wakati huo, rekodi ya Ba inaongea yenyewe. Alimaliza msimu ulioisha akiwa mfungaji bora wa klabu hiyo na msimu huu mpaka sasa ameshatupia mabao 13, akifunga karibu nusu ya mabao yote yaliyofungwa na Newcastle msimu huu.


Tishio la majeuhi pia lilishindwa kumuandama, kwani mshambuliaji huyo amekosa mechi 17 tu katika miaka 7 iliyopita.

Chelsea ambao wamekuwa katika msako wa kumtafuta mrithi wa Didier Drogba hatimaye sasa wwamefanikiwa kupata mchezaji ambaye ana sifa kama za Nahodha wa Ivory Coast.

Mapitio ambayo ameyapitia mshambuliaji huyu wa kisenagali ni funzo tosha kwa wachezaji wa kitanzania ambao wamekuwa nandoto za kutaka kucheza ulaya lakini wamekuwa wepesi wa kukata tamaa. Ba alikuwa na nia ya dhati ya kutaka kufanikisha ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa hasa katika ligi kuu ya England ndio maana alifanikiwa. Hakujali kwenda kucheza vilabu vidogo vya chini barani ulaya kwani alijua nini anatafuta, tofauti na wachezaji wetu hapa ambao wanataka wakitoka tu kwenye timu zetu za Kulwa na Doto waende moja kwa moja Old Trafford. Nidhamu, juhudi na kutokukata tamaa ndio njia sahihi iliyomfanya Demba Ba kuwa hapa alipo sasa - na ikiwa kama ambavyo watu wengi tunaamini, basi safari ya msenegali huyu haitakuwa imeishia hapa, kwani kiwango chake kitapanda maradufu na kucheka na nyavu itakuwa sio swali tena akicheza na watu wenye viwango vya dunia kama akina Mata, Hazard, Oscar.

No comments:

Post a Comment