Search This Blog
Tuesday, January 15, 2013
ATHUMANI KILAMBO: KOCHA ALIYEIPA MAFANIKIO MAKUBWA PAN AFRICAN, MPISHI WA AKINA SUNDAY MANARA
AMEKUWA AKIPIGANIA MAISHA YAKE KUTOKANA NA KENSA YA KOO KWA MIAKA MWILI SASA
ANAWAOMBA WATANZANIA, WANAMICHEZO WAMSAIDIE
DESTURI na Maadili ya Mtanzania ni kusaidiana katika Raha na Matatizo, ni
kawaida kusikia watu wakijitokeza kwa wingi kusaidia Mwenzao anapopatwa na
Matatizo, hiyo ndiyo desturi yetu watanzania, au sio jamani?
Moyo huu wa kusaidiana tumeuona katika kipindi cha kuugua kwa Msanii
Sajuki, sasa Marehemu Mungu ailaze Roho yake mahali pema peponi, watu bila
kujali tabaka, itikadi za kidini, au vyama vyao walijitokeza kusaidia pale
walipohitajika, ahsanteni sana Watanzania.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na Taarifa za kuhuzunisha zinazomhusu
aliwahi kuwa kocha na mwanzilishi a Timu ya Pan African ya Mbeya,
namzungumzia mmoja kati ya wanamichezo waliwahi kuiletea nchii sifa katika
medani ya soka kabla ya kuiwezesha Pan African kuchukua ubingwa a ligi
Tanzania Bara (1982), wakati huo ikifahamika kama ligi daraja la kwanza.
Mzee Athumani Kilambo, inaripotiwa kwamba kwa sasa yuko katika hali mbaya
akipigania maisha yake kutokana na ugonjwa wa saratani ya koo ambao umekuwa
ukimtesa kwa kipindi cha miaka miwili sasa.
Mzee Kilambo, ambaye kwa kulitaja Jina Lake, naamini kila mwanamichezo
aliyepata kushuhudia shughuli yake kipindi akiwa mchezaji na baadaye kocha
aliyeipa mafanikio makubwa timu ya Pan African, ataguswa kwa kusikia shujaa
huyu aliyepigania soka letu, sasa hivi anapigania maisha yake bila msaada
wowote kutoka kwa wadau wa michezo wa nchi hii.
MTANZANIA hivi karibuni ilifika katika Hospitali ya Ocean Road alikolazwa
Mzee Kilambo na kufanya mazungumzo, ambapo miongoni mwa mambo mengi
aliyoyazungumza Kilambo, Kocha huyo wa Zamani wa Pan African aliwaomba
Watanzania, Mashabiki wake, wanamichezo kumsaidia kupata fedha za
kugharamia matibabu ya Maradhi yanayo msumbuwa.
Mzee Kilambo baada ya kuruhusiwa hospitalini hapo, anasema Maradhi ya
Saratani ya Koo ambayo yamekuwa yakimsumbua ka miaka miwili yanahitaji
fedha nyingi kutibiwa ikiwa ni pamoja upasuaji, yamekuwa yakimsumbua kwa
kipindi cha miaka miwili sasa.
“Nasumbuliwa na Kensa ya Koo kwa Takribani miaka miwili sasa, nimekuwa
nikija hapa Ocean Road mara kwa mara kwa ajili ya kupoza makali tu,
zinahitajika fedha za kunitibu,” anasema Kilambo.
Mzee Kilambo kwa kupitia gazeti hili na makala haya anawaomba wadau na
wanamichezo kujitokeza kwa wingi kumsaidia hasa katika kipindi hiki kigumu,
kumchangia kwa hali na mali ili aweze kutibiwa ugonjwa huu unaohatarisha
maisha yake.
Pamoja na kuumwa kwake, Mzee Athumani Kilambo pia hakusita kuzungumzia timu
yake aliyoipenda na kuitumikia kwa nguvu zake zote, akiwa ni mmoja wa
waanzilishi wa Pan African, anasema wakati Pan African inaanzishwa mwaka
1976, lengo lilikuwa ni kuanzisha kikundi au chama cha kusaidiana katika
kipindi cha matatizo, swala la Klabu lilikuja baadae.
“Wakati Pan African tunaianzisha mnamo mwaka 1976, lengo letu lilikuwa ni
kufanya kitu ambacho kingetuezesha kusaidiana wakati wa Matatizo, wazo la
kuanzishwa kwa Klabu lilikuja baadae,” anasema Kilambo.
Anasema wakati huo umoja wao ulikuwa na nguvu sana kiasi kwamba wakati wa
matatizo na Raha, walishirikiana pamoja na ilikuwa ni vigumu kusikia kuna
makundi.
“Wakati ule umoja wetu ulikuwa na nguvu mno, ilikuwa ni kawaida kuona
tunashirikiana katika kila hali kiasi kwamba wakati wa matatizo na raha
tulikua sote, sasa naaomba wadau wa michezo hasa wachezaji wa zamani wa Pan
African kukumbuka enzi zetu kwa kunisaidia kuondokana na haya maradhi,
anasema Kilambo.
Mzee Kilambo anawakumbuka baadhi ya waanzilishi wengine wa Pan African
ambao anawataja kuwa ni, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF) Dkt. Ramadhani Dau, Marehemu Sam Dee, Mzee Ally Abbas, Shiraz
Sharrif, Mzee Paul Sozigwa, Dkt. William Ugundo na wengineo wengi.
Nafahamu kuwa Marehemu huwa hadaiwi na kwa muktadha huo, wote waliotangulia
sina la kuwazungumzia zaidi ya kuwaombea Mungu awalaze mahali pema peponi,
Lakini ndugu zangu wote tulio hai hususan marafiki zake na waanzilishi
wenzake, huu ndio muda wa kudhihirisha udugu wetu.
Huu ndio muda wa kumuonesha ndugu yetu, Mzee Athumani Kilambo na
mwanamichezo mwenzetu, kuwa tunaujali na kuuthamini mchango ake katika
maendeleo ya soka letu, na zaidi huu ndio muda a kudhihirisha utu wetu na
sio kusubiri hadi yatokee yakutokea, Mungu aepushie mbali.
Kilambo pia anaendelea kuwakumbuka wachezaji waanzilishi wa Pan African,
waliochangia timu hiyo kupata umaarufu, baadhi yao wamo, Omary Kapera,
Adolf Richard, Jellah Mtagwa, Mohammed Mkweche, Sunday Manara, Kitwana
Manara, Kassimu Manara na Marehemu Muhaji Mukhi.
Ifahamike kamba lengo la kutaja hayo majina hapo juu haina maana ya kutaka
kumhukumu mtu, lengo ni kuwaonesha watu aina ya mtu tunayemzungumzia ni
nani na mmchango ake katika soka letu, naamini ni wengi tu wanawafahamu
akina Manara, lengo hapa ni kutoa hamasa kwa wadau ili mwisho wa siku sote
tushiriki kumsaidia shujaa huyu.
Athumani Kilambo, ameifanyia makubwa taifa letu na soka letu, amefanya
mambo mengi makubwa ambayo nikiyataja sitoweza kuyamaliza leo, kwa ufupi
Watanzania huu ni Muda wa kurudisha fadhila, huu ni muda wa wanamichezo
kuonesha uwanamichezo wetu.
Kwa maoni na Ushauri
www.kijiwechetu.blogspot.com
fadhiliathumani85@gmail.com
0756038214/0654724337
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment