Search This Blog

Monday, December 24, 2012

TAARIFA KUTOKA TFF!

MTIGINJOLA KUONGOZA KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Idd Mtiginjola kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF iliyoundwa kutokana na marekebisho ya Katiba yaliyofanyika hivi karibuni.

Mtiginjola ambaye ni Wakili wa kujitegemea ataongoza kamati hiyo yenye wajumbe watano ambayo sasa itakuwa chombo cha mwisho kusikiliza rufani zinazotokana na uchaguzi wa TFF, na wanachama wa TFF ambao hawatakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Kabla ya uteuzi huo, Mtiginjola alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana. Nafasi yake katika kamati hiyo na ile ya mjumbe mwingine Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Shabani Semlangwa aliyefariki dunia Julai mwaka huu zitajazwa hivi karibuni.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambayo vinara wake (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti) wanatakiwa kitaaluma kuwa wanasheria ni Francis Kabwe. Kabwe ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wajumbe wengine walioteuliwa na Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake cha jana (Desemba 23 mwaka huu) ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.

Wengine ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.



MECHI YA STARS, CHIPOLOPOLO YAINGIZA MIL 109/-
Pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zambia (Chipolopolo) lililochezwa juzi (Desemba 22 mwaka huu) limeingiza sh. 109,197,000.

Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 17,383 waliokata tiketi kushuhudia mechi kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 16,657,169.49, maandalizi ya mchezo sh. 55,339,510, tiketi sh. 5,803,900, ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000, Wachina (technical support) sh. 2,000,000, umeme sh. 300,000 na maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000.

Nyingine ni bonasi kwa Taifa Stars sh. 13,826,313, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 2,504,022, asilimia 10 ya uwanja sh. 1,252,011, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 626,005 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 8,138,070.

Mapato ya mechi nyingine za Taifa Stars ilizocheza nyumbani mwaka huu yalikuwa Taifa Stars vs Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC (Leopards) iliyofanyika Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sh. 32,229,000. Taifa Stars vs Msumbiji (Mambas) iliyochezwa Februari 29 mwaka huu sh. 64,714,000.

Taifa Stars vs Malawi (The Flames) iliyochezwa Mei 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. 40,980,000. Taifa Stars vs Gambia (The Scorpions) iliyochezwa Juni 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zilipatikana sh. 124,038,000 na Taifa Stars vs Kenya (Harambee Stars) iliyofanyika Novemba 14 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza iliingiza sh. milioni 45.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment