Wakati Patrick Viera anapiga penalti ya mwisho pale kwenye uwanja wa Millenium katika jiji la Cardiff na kumfunga golikipa wa Manchester United wa wakati huo, Bw Roy Carroll kisha kusherehekea ubingwa wa kombe la FA wa mwaka 2005, hakuna aliyewaza kwamba Arsenal itakaa zaidi ya miaka 7 bila kushinda kombe lolote kubwa lakini leo hii kuna mashabiki wa Arsenal wanaoamini kwamba timu yao ya msimu huu inaweza isishinde kombe lolote msimu huu pia. Mimi naamini Arsenal msimu huu ina nafasi walau ya kufika fainali kama si kushinda kombe la ligi maarufu kama Capital One Cup.
Arsenal imeondoka kabisa kwenye vichwa vya watu wengi, wadau wa soka kwamba ni timu inayoweza kushinda ligi kuu ya Uingereza hasa kwa kipindi hiki. Hii haimaanishi kwamba Arsenal si timu bora au tishio Uingereza, hapana, kinachomaanishwa hapa ni kwamba Arsenal ya sasa haina nguvu ya kuhimili vishindo vya ligi kuu na mwisho wa msimu iibuke bingwa wa ligi kuu ya Uingereza kama ilivyoshinda mara ya mwisho katika msimu wa 2003/2004, kitu ambacho kwa kiasi fulani kinasanifu ukweli halisi wa mambo. Arsenal ya hivi sasa ni timu ambayo inajikita zaidi kwenye makombe mengine mbali na ligi kuu kutokana na mfumo wa hayo makombe ulivyo, mfumo wa mtoano. Pamoja na kujikita kwenye makombe hayo (FA, Ligi ya mabingwa ya Ulaya ie UEFA CL na Capital One Cup) bado imekuwa haifanyi vizuri sana pia kwa sababu hata huko haijashinda hata moja kwa kipindi hiki cha miaka inayokaribia 8.
Sasa wakati wengi tukiona Arsenal haina nafasi ya kushinda ligi kuu ya Uingereza, kuna mashabiki baadhi wa Arsenal ambao hao dua zao za kuiombea timu yao ziko tofauti kabisa na matarajio ya wengi, wao wanaombea mafanikio mahasimu wao wakubwa zaidi, Tottenham Hotspur au Spurs. Unajua kwa nini wanaiombea mafanikio Spurs? Endelea kufuatana nami.
Hizi timu za Arsenal na Tottenham, uhasama wao umekuwa ni wa muda mrefu sana, siku moja nitakuja hapa kuuelezea huu uhasama wao tu, chanzo na kwa nini unadumu hadi leo hii. Pamoja na uhasama huu kudumu kwa muda mrefu bado Arsenal imeendelea kuwa timu bora mbele ya Spurs kwa kipindi kirefu sasa.Tangu ligi ya Uingereza imekuwa ligi kuu, Tottenham Hotspur imewahi kumaliza juu ya Arsenal mara moja tu katika msimu wa 1994/95 wakati Spurs ilipokuwa ya saba na Arsenal ya 12. Hiki ndio kitu kinachowasukuma mashabiki hawa wa Arsenal waombee Spurs ishike nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya Uingereza wakiamini timu hiyo haitakaa imalize juu yao tena na kama Spurs ikiwa ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingereza basi Arsenal itakuwa ya kwanza. Mtu mwingine unaweza kuona kama hawa mashabiki wa Arsenal aidha wanafanya mchezo wa kuigiza au labda haya ni maneno yao ya kuikashifu Spurs lakini kumbe wao wanamaanisha wanachokisema.
Pamoja na kuwa ligi kuu ya Uingereza bado ni ‘mbichi’ na bingwa hawezi kutajwa kipindi hiki, hili halinizuii kuwashauri mashabiki wa aina hii wa Arsenal kutokuwa na ndoto za kufikirika za aina hii badala yake washangilie kuwafunga Tottenham Hotspur goli 5 na Andre-Villas Boas goli 5 (wakati akiwa na Chelsea) wote kwa ujumla wao mara mbili mfululizo. Chakufanya, wamwambie kocha wa timu yao Bw Arsene Wenger ajikite zaidi katika kununua wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu na hasa wachezaji ambao tayari wameshaonekana kuwa bora (established players) kama Arteta, hapo kwa hakika watakuwa na timu bora ambayo haitangoja mpaka Spurs iwe ya pili ndipo yenyewe iwe ya kwanza.
Nakushukuru kwa kusoma makala hii mpaka hapa. Tuonane tena wakati mwingine.
Imeandaliwa na PodoBest
Twitter: @iPodoBest
hahaha safi
ReplyDelete