Kipindi cha usajili ni kipindi ambacho mashabiki wa soka ulimwenguni kote huwa na presha kubwa ya kutaka makocha wa timu wanazoshabikia zisajili wachezaji fulani au ziwaache wachezaji fulani, baada ya hapo dirisha la usajili linapofungwa mashabiki hukaa na kuanza kutafakari kilichofanywa na timu zao au kilichofanywa na timu nyingine kwenye usajil.
Ifuatayo ni orodha ya wachezaji 10 waliosajliwa na kutengeneza vichwa vya habari kwa tetesi mbalimbali za usajili.
10. Oscar
Roman Abramovich aliamua kufanya biashara mapema akiwalipa Santos paundi milioni 25 kabla ya michuano ya olimpiki huku akiwaacha wachezaji wengine wakiwazingua waandishi kwa tetesi mbalimbali.
Uwezo wake ulishadhiirika kwenye michuano ya olimpiki akiichezea Brazil na anaingia kwenye kikosi cha Chelsea akiwa ana mzigo wa matarajio kwa mashabiki.
9. Shinji Kagawa
Wakati Sir Alex Fergusson alipoonekana kwenye uwanja wa Olympic huko Ujerumani akifuatilia mchezo wa DFB Pokal kati ya Borrusia Dortmund na Bayern Munich wengi tayari walifahamu nini kinafuatia, siku tatu baada ya hapo Shinji alifichua kuwa yuko mbioni kukamilisha usajili kwenda Man United na baada ya hapo haikuwa siri tena.
Akiwa amecheza Dortmund misimu miwili huku aking'aa kwenye misimu yote Kagawa anaingia United akiwa na jukumu la kurithi nafasi inayotegemea kuachwa wazi na Paul Scholes, tofauti ya Bundesliga na EPL inaweza kuwa changamoto kubwa kwake lakini hakuna shaka juu ya ubora anayoongeza kwenye kikosi cha mashetani wekundu.
8. Santi Cazorla
Tayari Arsenal ilishawasajili Lukas Podolski na Olivier Giroud wakiwa wanajiandaa kumkosa Robin Van Persie ambaye tangu mapema alishasema anataka kuondoka.
Ghafla baada ya kuondoka kwa RVP, Alex Song naye akaondoka na hapo Wenger aliona haja ya kumsajili Sani Cazorla, mchezaji ambaye matatizo ya kiuchumi ya Malaga yalifaya tetesi za usajili wake kuwa kweli .
7. Mousa Dembele.
Kila lilipotajwa jina la Luka Modric la Mousa Dembele halikuwa mbali, kama utakumbuka wakati usajili wa Modric kwenda Madrid unaonekana kuelekea kufeli Dembele alitajwa kutazamwa na Madrid kama mbadala na pale Modric alipoenda Madrid Dembele alikwenda Tottenham kuziba pengo lake akitokea Fulham masaa kadhaa kabla ya dirisha kufungwa.
6. Clinton Dempsey.
Moja ya sababu za Fulham kufanya vizuri kwenye misimu ya hivi karibuni ni jina la kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Marekani Clint Dempsey.
Wakati kocha mpya wa Liverpool Brendan Rogers anaingia Anfield alimtaja Dempsey kama mmoja wa watu anaowahitaji, bahati mbaya paundi milioni moja iliwashinda Liverpool na ofa ya paundi milioni sita toka kwa Tottenham ilitosha kusajili mchezaji mwingine toka Fulham baada ya Dembele.
4. Alex Song & Jordi Alba
Jordi Alba alijijengea jina kama beki wa kushoto wapili kwa ubora nyuma ya Ashley Cole na usajili wake uligubikwa na tetesi za kwenda Man United na kurudi kwenye klabu alikoanzia soka Barcelona.
Tetesi zakwenda United zilififia haraka kama moto wa jiko la mkaa lililomaliza kupika baada ya beki huyo kusajiliwa na Barcelona akiwa mchezaji wa tatu wa Valencia kuitolea nje United ikiwa ipo tayari kutoa fedha zilizohitajika na Valencia, babu aliwahi kuchukua za uso toka kwa David Villa na David Silva pia.
Alex Song hakutengeneza vichwa vingi vya habari kwa kuwa taarifa yake kwenda Barca ilikuja ghafla na ilikuja baada ya Barca kushindwa kumsajili Javi Martinez ambaye Bilbao walikuwa wakitaka paundi milioni 40.
4. LUKA MODRIC
Dirisha hili la majira ya joto halikuwa na vurugu za usajili zilizozoeleka nchini Hispania , unapotafakari kuwa Madrid na Barca wamesajili wachezaji watatu kati yao unaweza kushangazwa na pengine hii ni ishara kuwa vikosi vyao vimetimia na ndio maana hakuna usajili mkubwa uliofanyika.
Moja ya tetesi ambazo karibu kila siku zilipamba vyombo vya habari ni ile ya Luka Modric, mwanzo aligoma kwenda pre-season, akagoma kufanya mazoezi lakini mwisho wake Spurs na Los Merengues Blancos walikaa kwenye meza moja na Modric akauzwa.
3. Lucas Moura.
Mwanzoni mwa dirisha la usajili magazeti ya Daily Mail, The Mirror, The Sun na mengineyo yaliripoti taarifa za United kutaka kumsajili winga kinda wa Sao Paolo Lucas Moura, baada ya hapo Clip za Youtube zinazomuonyesha dogo huyu akifanya vitu vyake ndani ya uzi wa Sao zilivunja rekodi ya kutazamwa.
Baada ya hapo mbio hizi zikawa ngumu baada ya timu nyingine kuingia, Inter Milan na Madrid walitajwa lakini tetesi zilizidi kuwapa nafasi kubwa United, baadaye mwishoni kabisa wakaingia PSG na mkwanja wa mafuta na hapo ikawa kilio kingine kwa United kwani Lucas alisajiliwa na wafaransa hao wanaofaidi fedha za kiarabu.
2. Robin Van Persie.
Robin tayari alishasema kuwa anataka kuondoka kwenda mahali ambako atatwaa ubingwa. Kauli hii ilizua vita kati ya Man United na Man City huku Juventus nao wakifuatilia kwa karibu hali ilivyoendelea. Tatizo la City lilikuwa mkurugenzi Brian Marwood ambaye alikuwa akitekeleza maelekezo ya mabosi ya kutonunua hovyo na upande wa Juve kifungo cha kutokaa benchi alichokipata Antonio Conte kilimvunja moyo Van Persie na kumfanya awe na chaguo moja tu ambalo ni Man United, biashara iifanyika na RVP akavikwa jezi namba 20 yenye nembo ya Man United.
1. Eden Hazard.
Tetesi za Hazard zilianza katikati ya msimu uliopita. Mwanzoni aliwataja Tottenham kama klabu ambayo angependa kuvaa jezi zake, baada ya hapo alikaribishwa kwenye manchester derby na kisha akapewa tour ya uwanja wa Etihad, baadaye zilitoka taarifa kuwa anatafuta nyumba jijini Manchester na hapo vita ikawa ya United na City, kuelekea mwishoni mwa msimu Hazard alitoa taarifa kuwa angevaa jezi za mabingwa wa ulaya na hapa ndio Chelsea walipoingia huku United nao wakiwa mabingwa wa zamani wa ulaya wakihusishwa lakini kwa mbali.
Mwishoni kabisa akasema atavaa jezi za blue na United wakaondoka , akaja Luis Saha kwenye twitter akitoa taarifa kuwa Hazard atasajiliwa na Chelsea, hakika tetesi za Hazard zilitawala vichwa vya habari kuliko usajili wowote ule.
No comments:
Post a Comment