Search This Blog

Tuesday, September 25, 2012

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA

. UNAPENDWA NA KUOGOPWA NA WATU WENGI DUNIANI
. UKO HATARINI KUPOTEZA ASILI YAKE KABISA

Na Onesmo Ngowi
 Masumbiwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi.
 Japokuwa katika maisha ya kawaida watu wengi hupigana kwa sababu mbalimbali kama vile kuwa na hasira, kujilinda au kuwaonea tu wengine kwa sababu mbalimbali lakini kwa kawaida ni watu wachache sana walio tayari kujiingiza katika kuucheza mchezo huu.
 Kama tulivyokwisha ona kwenye makala zilizotangulia, ngumi ni mchezo ambao ulianza wakati wanadamu walipoanza tu kukunja ngumi na kurushina kama mchezo. Mchezo wa ngumi upo wa aina mbalimbali.
 Japokuwa kumbukumbu nyingi zinaonyesha kwamba chimbuko haswa la mchezo huu linakubalika kuwa ni nchi za kusini mwa Ulaya hususan Uyunani (leo Ugiriki) na Urumi (Italia ya leo) lakini kuna mataifa au dola nyingine nyingi zilizokuwa na aina yao ya michezo iliyofanana na ngumi.  Wanazuoni wa maswala ya michezo wanaifananisha michezo yote ya kupigana iwe ni kwa kutumia mikono na miguu au kutumia silaha za aina mbalimbali na mchezo wa ngumi.
 Aidha mchezo wa ngumi ni kati ya michezo inayojenga ushupavu wa wachezaji na kuwafanya washujaa wa jamii. Wachezaji wa ngumi mara nyingi ni watu wanaoonekana kama mashujaa kutokana na ujasiri wanaoonyesha katika mchezo wenyewe. 
 Wakati wa utawala wa Marcus Aurelius, mtawala shupavu wa iliyokuwa dola ya Roma (Italia ya leo) na aliyepata mafanikio makubwa ya kuipanua dola ya Warumi (Italia) toka ukanda wa bahari ya Mediterania hadi jangwa la barafu la Siberia huko Urusi, mashujaa wengi wa michezo walichuana kwenye mashindano yaliyofanyika Coliseum (uwanja mkubwa uliokuwa umejengwa katika jiji la Roma). 
 Mashujaa hawa ni pamoja na wapiganaji ngumi na wengine walioshiriki kwenye michezo yenye hatari na kujijengea umaarufu mkubwa kwenye jamii ya Warumi. Dola ya Warumi ilikuwa na nguvu sana katika bara la Ulaya na ilienea hadi kaskazini mwa bara la Afrika. Hivyo utamaduni wao hususan michezo iliyochezwa baada ya ushindi wa vita ulienea kwenye himaya yao yote.
 Kwa mfano katika dola ya Manchuria (China ya leo) iliyotawala kutoka Uchina na nchi nyingi za mashariki ya kusini mwa Asia ngumi zilijulikana kama Kung-Fu ambazo japokuwa kuchezwa kwa ngumi hizi huchanganywa na mateke.
 Maaskari wengi walitakiwa wawe wamejifunza kupigana Kung Fu na waujue mchezo wenyewe kwa kiwango kikubwa. Kwao Kung Fu ilikuwa ni aina nyingine ya silaha na walizitumia ipasavyo kwenye kukabiliana na maadui kwenye vita.  Baada ya ushindi wa vita walikusanyika katika viwanja vikubwa na kucheza michezo hii kama isahara ya kusheherekea ushindi wao.
 Dola ya Kijapani iliyotawala nchi nyingi za Asia ikiwa ni mpinzani mkubwa wa dola ya Manchuria katika karne ya 12 nayo ilikuwa na mchezo wa ngumi uliojulikana kama Karate. Mashujaa wengi wa Kijapani walitakiwa wawe na ujasiri wa hali ya juu wa kupigana Karate.
 Kwao Karate ilikuwa sio mchezo tu bali ni ufundi wa kumshinda adui kwenye vita. Ushindani mkubwa kati ya Wachina na Wajapani uliifanya michezo ya Karate na Kung Fu kupata umaarufu mkubwa sana. Kila upande uliuona mchezo wake kama bora kuliko mwingine.
 Katika miaka ya karibuni watawa wengi katika ukanda huu wanaojulikana kama Monks (monki) waiijifunza Karate na Kung Fu kwa kiwango cha juu ili kujilinda na Maharamia waliokuwa wanawavamia na kuiba mali zao.
 Mtawala Genghis Khan wa dola ya Mongolia (Mongol Empire) ambayo ilitawala kuanzia Mongolia yenyewe hadi Persia (Irani), Babilon (Iraki) na baadhi ya nchi za Balkan (Ulaya ya Kati) aliwachagua wapiganaji wake kwa ustadi na uangalifu mkubwa. Kwa kutumia wapiganaji waliosheheni kila aina ya ushupavu aliweza kushinda majeshi mengi na kuwa kati ya watawala walioogopewa sana wakati wa enzi yake.
 Dola ya Otoman ya Kituruki iliyotawala katika karne ya 19 ilitumia mchezo ulioulikana sana na wengi kama Mieleka ukichanganya na utumiaji wa farasi. Mara nyingi wachezaji wa mchezo huu walifariki kutokana na ugumu wa mchezo wenyewe na watanzamaji walisisimka sana kuona damu ikimwagika. Kwao huu ulikuwa ndio ushujaa tosha.
 Nazo dola za Mafarao wa Misri zilikuwa na aina yao ya michezo iliochezwa haswa na watumwa kwa minajili ya kuwafurahisha Mafarao na familia zao hata katika kujitetea au kushambulia maaduni! Kwa dhati kabisa mchezo wa ngumi ulivyojulikana na Wanafalsafa wa zamani katika ukanda wa Mediterania katika dola nilizotaja hapo juu ulikuwa ni mojawapo ya vipimo vya ujasiri wa mtu.
 Sio vibaya watanzania wakaelewa kuwa ngumi ni mchezo wa zamani sana kuchezwa hata kabla nchi yetu haijatawaliwa na wakoloni katika karne ya 19. Michezo hii iliyochezwa katika viwanja vikubwa vyenye mikusanyiko mikubwa ya watu (Coliseum) huko Roma na (Arena) huko Athina, iliyokuwa katika hekalu kubwa la ufalme wa Wayunani (Ugiriki) la Akropolis.
 Viwanja hivi vilikuwa ndio mwanzo wa ulingo wa kisasa kwani japokuwa ulingo wa kisasa ni wa mraba lakini mwanzo wake ni Arena ya mduara.
Mwandishi wa makala haya ni: Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC). E-mail: ibfafrica@yahoo.cm

No comments:

Post a Comment