Shaffih Dauda na Mbwiga mwenye kapero tukiwa na timu ya vijana wa Kijiji cha Ngukumo iitwayo Chui |
Kwa takribani wiki mbili sasa nipo kwenye tour ya tamasha la Fiesta linalofanyika hapa nchini katika mikoa kadhaa. Wikiendi iliyopita nilikuwa upande wa kanda ya ziwa ya Tanzania na wiki hii nipo na timu nzima ya maandalizi ya Fiesta kwenye kanda ya kati ambapo tamasha hilo litachukua nafasi mwishoni mwa wiki hii mkoa wa Tabora na Singida.
Jana Jumatatu nikiwa na baadhi ya wafanyakazi wenzangu wa Clouds ambao tupo kwenye timu ya maandalizi ya Fiesta, tulikuwa safarini kutoka jijini Mwanza tukielekea Tabora ambapo tamasha la Fiesta litachukua nafasi wikiendi hii. Tukiwa njiani tukapita kwenye kijiji cha Ngukumo, kata ya Kiniziwa, Tarafa ya Puge wilaya ya Nzega ambapo tukiwa barabarani pembeni yetu tukaona vijana wanacheza soka - kiukweli ilibidi nisimamishe gari na kuanza kuangalia vijana wale wanalivyolisakata kabumbu. Kwa jicho la haraka haraka nikaona vijana wale walikuwa na vipaji sana na endapo wangepata nafasi ya kuendelezwa ingekuwa stori nyingine.
Mimi na Mbwiga tukiwa na timu ya watoto tuliowakuta wakicheza soka na kuvutiwa nao |
Tukawapa msaada wa Tshirt |
Baada ya kuona wanacheza huku vitumbo wazi ilibidi tuwape msaada wa T-shirt za mmoja wa wadhamini wa Fiesta kampuni ya mafuta ya Gapco. |
"Nadhani kila mtu anajua dhamira ya ukweli na ya dhati aliyonayo Raisi wetu Jakaya Kikwete juu ya kusaidia michezo, lakini anakwamishwa sana na viongozi wa chini waliokaa kuangalia tu matumbo yao na kupitisha siku ziende aje tumpe kura tena. Hapa pia nazungumzia viongozi wa soka pia kuanzia ngazi ya Taifa, mkoa mpaka wilaya yetu ya Nzega. Kwa kweli hakuna lolote wanalofanya kuweza kuhakikisha vijana tunapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyetu - kwa mfano hapa Nzega ni aghalabu sana kuona kuna mashindano yameandaliwa na chama cha wilaya, mashindano ambayo yangesaidia kuweza kuvionyesha vipaji vyetu na labda tungepata bahati ya kuchukuliwa timu kubwa za mkoa na hatimaye kuonekana kwingineko hivyo kuweza kutimiza ndoto zetu. Viongozi kiukweli wa Tabora nzima wamelala na ndio maana haishangazi kuona hatuna timu kwenye ligi ya Tanzania kwa miaka mingi sana sasa," anasema Zahoro kwa uchungu.
"Nakumbuka zamani hapa wilaya ya Nzega tulikuwa na timu yetu ambayo ilikuwa inafanya vizuri sana ilikuwa inaitwa AMKA - timu ilikuwa inaenda vizuri na mpaka nakumbuka ilianza kutoa wachezaji kwenye timu kubwa kama Said John aliyeenda Milambo, lakini mwishowe ikafa kwa sababu ya uongozi.
"Wengine sie tulikuwa tunapotea kutokana na makundi lakini kutokana na kutumia muda mwingi katika kufanya mazoezi tunakuwa hatuna muda kufanya maovu. Siku hizi ukiachana na kufanya shughuli zetu za kilimo cha mahindi michezo imekuwa mwokozi wetu lakini kwa namna hii sidhani kama hali itaendelea kuwa ilivyo sasa. Kuna baadhi yetu tunaanza kuwa wakubwa na tunataka kuwa na maisha yetu binafsi na kuisadia familia zetu, kwa bahati mbaya elimu zetu sio kubwa kihivyo tulichagua soka kama ajira yetu lakini hatuoni mwanga mbele. Tunaomba Shaffih upeleke kilio chetu kwa wafanya maamuzi wasing'ang'anie tu kukaa kwenye maofisi Dar es Salaam, watoke waje vijijini pia kuna watu wana vipaji vikubwa ambavyo vinaweza kulisadia taifa kupata maendeleo ya soka. Kuna wengine hapa hapa ni wadogo sana na bado wapo shule - serikali iwaandalie mfumo wa kujenga shule ambazo zitakuwa zinatoa mafunzo ya soka na kwa hili naamini ndani ya miaka kadhaa tutaona namna litakavyoleta manufaa kwa taifa." - Alimaliza Zahoro Mohamed ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 18, anacheza nafasi ya kiungo cha kukaba.
No comments:
Post a Comment