TFF YATOA ITC KWA WACHEZAJI WANNE
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) kwa wachezaji wanne waliokuwa wakichezea timu mbalimbali nchini.
Wachezaji
hao ni Tony Ndolo aliyejiunga na KCC ya Uganda kutoka Toto Africans,
Felix Amech Stanley aliyekwenda Bahla ya Oman kutoka Coastal Union,
Ernest Boakye kutoka Yanga aliyejiunga na Tripoli Athletics Club ya
Lebanon na Derrick Walulya aliyerejea URA ya Uganda kutoka Simba.
15 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TWFA
Wanamichezo
15 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Chama
cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) utakaofanyika mwanzoni
mwa mwezi ujao.
Waliochukua
fomu za kuwania uenyekiti ni Lina Kessy, Isabellah Kapera na Joan
Minja. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imeombwa na Roseleen Kisiwa pekee
wakati Katibu Mkuu ni Amina Karuma na Cecilia Makafu. Macky Mhango pia
ni mwombaji pekee aliyeomba nafasi ya Katibu Msaidizi.
Waombaji
watatu wa nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ni Furaha Francis, Juliet Mndeme na Zena Chande.
Nafasi ya Mhazini nayo ina mwombaji mmoja tu ambaye ni Rose Msamila.
Sophia
Charles, Rahim Maguza, Telephonia Temba na Jasmin Badar Soud wao
wanaomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho kwenye
uchaguzi huo ambao utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya
Ombeni Zavalla.
MKUTANO VODACOM, KLABU ZA LIGI KUU
Klabu
za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom zimekutana jana (Septemba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo
yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba wa
udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa
mdhamini kuangalia uwezekano wa kukiondoa.
Pande
hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila
klabu mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu
katika ligi hiyo.
Klabu
zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African Lyon ambayo
ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo.
MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI TAFCA
Mchakato
wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania
(TAFCA) unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa
wagombea.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan
Mambosasa, fomu kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka
huu, na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka
huu.
Fomu
hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya
fomu kwa waombaji wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu
Mkuu na Katibu Msaidizi ni sh. 200,000.
Nafasi
zilizobaki za Mhazini, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ada ya fomu ni
sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment