Manchester City walianza msimu wake kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Chelsea wiki iliyopita. Kitu cha kukumbukwa kwenye mchezo huu ukiachilia mbali kadi nyekundu ya Ivanovic yalikuwa majaribio ya Roberto Mancini kuchezesha watu watatu nyuma badala ya mfumo uliozoeleka wa kuchezesha mabeki wanne.
Kuchezesha watu watatu si jambo geni sana kwa City . Mara kadhaa Mancini alijaribu kuchezesha watu watatu mara kadhaa kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita kwenye baadhi ya michezo. Kipya katika mfumo huu hata hivyo ni ukweli kwamba anaanza mechi akitumia mfumo huu kinyume na msimu uliopita ambapo alikuwa akitumia mfumo huu kumaliza mechi.
Kwanini mabadiliko haya.
Moja ya shida ambazo Man City ilizipata msimu uliopita ilikuwa kukosa mashambulizi toka pembezoni mwa uwanja. David Silva na Samir Nasri si wachezaji ambao wanacheza vyema wakiwa pembeni ,wote ni viungo ambao hucheza vizuri zaidi wakiwa wanapitia katikati ya uwanja badala ya pembeni , kucheza kwa wachezaji hawa katikati mwa uwanja kuliwanyima wachezaji wanaotumia nafasi kubwa uwanjani kama Tevez na Yaya Toure kwa kuwa kama ilivyo kwa Silva na Nasri nao hupenda kucheza katikati.
Tatizo hili lilipatiwa ufumbuzi kwa muda msimu uliopita wakati alipocheza mtu kama Adam Johnson ambaye angetanua uwanja na kuipa timu balance iliyohitajika . Ila shida moja ni kwamba Mancini hana imani na Adam kiasi cha kumchezesha kila mara hivyo bado hali hii iliendelea kuwa tatizo.
Mancini alikuwa na ufumbuzi wa aina yake kwenye suala hili hasa kwenye mchezo muhimu wa ugenini kuelekea mwishoni mwa ligi dhidi ya Newcastle United. Huku mechi ikiwa inaelekea kuwa 0-0 kuelekea kipindi cha pili , Mancini alimuingiza Nigel De Jong kwenye nafasi ya Samir Nasri na kumsogeza mbele Yaya Toure . Katika akili ya mtu wa kawaida haya yalikuwa mabadiliko ya kujihami zaidi lakini mabadiliko haya yalimpa Toure nafasi ya kupanda na kusaidia mashambulizi. Baada ya hapa Toure alifunga mabao mawili yaliyoipa City ushindi wa mabao 2-0.
Kuchezesha mabeki watatu moja kwa moja kutaipa City nafasi zaidi ya kushambulia hata kama itamaanisha baadhi watalazimika kushuka kusaidia ulinzi. Na zaidi ya hapa Mancini anajaribu kuipa City mtazamo mbadala .
Inavyofanya kazi.
Mfumo wa City wa 3-4-1-2 unashuhudia walinzi watatu wakiwa wanalindwa na viungo wawili wakabaji mbele yao, wachezaji wawili wa pembeni na washambuliaji watatu.
Wakati timu ikimiliki mpira wachezaji wa Pembeni wanakuwa kama mabeki wa kushoto na wa kulia , wakijaza nafasi inayoachwa wazi na washambuliaji wa pembeni wakiwa wamepanda . Kwenye kipindi cha pili, City walichezesha mabeki wa pembeni ambao ni Clichy na Zabaleta kama mabeki wa kati wanaocheza pembeni . Beki anayecheza kati anacheza chni zaidi kati ya mabeki watatu.
Wakati timu ikiwa na mpira mfumo wa ulinzi wachezaji wanaocheza nyuma wanasaidia kumiliki mpira na kupoza presha lakini inafanya hali ya ukabaji kuwa ngumu na madhara yake ni kuifanya timu kuwa wazi sana na inaweza kufungika rahisi kwenye mashambulizi ya ghafla.
Kitu muhimu kwenye mfumo wa 3-5-2 ni wachezaji wanaocheza pembeni. Wanapaswa kutimiza majukumu ya mawinga na mabeki huku wakitanua uwanja wakati wa mashambulizi na kulazimika kukimbia kukaba wakati mpira ukipotea.
Wakati jukumu la beki wa pembeni ambaye anashambulia linapokuwa lazima kuliko lile la winga anayecheza mbele yake mara nyingi mabeki wa pembeni katika mifumo ya kisasa wanacheza kwa kutumia nafasi kubwa iliyoko mbele yao na mara nyingi hulazimika kukata na kuingia ndani.
Sababu kubwa ya beki anayecheza pembeni ya kuwafanya washambulie zaidi ni kwamba kwa mfumo wa sasa hakuna mchezaji maalum wa kukabana na beki wa pembeni .
Mwisho.
Majaribio ya Mancini ya kutumia mfumo wa 3-4-1-2 unaonyesha ishara ya kuleta vita ya kusisimua ya kimbinu wakati City ikiwa inacheza na timu nyingine hasa kwenye ligi ya mabingwa. Kama itakuwa inatumika kama mpango mbadala wa kiulinzi au mfumo wa kushambulia kwa kushtukiza tutapata majibu wakati michuano hii ikianza na mfumo huu utakapotumika, itakuwa tofauti na kile tulichozoea kukiona na kingine cha msingi ni jinsi mfumo huu utakavyofanya kazi dhidi ya timu kubwa kwenye ligi ya England.
kaka shaffih mfumo huo ndio uliompa mafanikio Pandelli na Italia yake katika UERO 2012
ReplyDelete