Search This Blog

Monday, July 9, 2012

KAYUNI THUBUTU KUMTOA KIFUNGONI MWASAMAKI....


 
Na Kenneth Mwaisabula
TUNAKUTANA tena katika kona hii, baada ya matoleo mawili yaliyopita kuwaletea yaliyojiri katika mkoa ya Mbeya na Tabora katika enzi hizo.
Nakiri, nimepata mwitikio mkubwa kiasi kwamba, baadhi ya wakazi wa mkoa wa Tabora wenye umri uliokwenda kidogo, walitokwa na machozi kwa niliyowakumbusha.
Nimepata mialiko mingi tu kutoka Kigoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi na Mtwara.
Nami nasema Inshaala, nikipata mfadhili na nafasi, nitafika huko. Lakini, leo naomba niibuke na kitu kingine kabisa.
Wakati nikiwa na umri mdogo, muda mwingi nilikuwa nazungumza na marehemu bibi yangu mzaa baba; alikuwa akinipa hadithi nyingi za zamani.
Aliwahi kunitajia watu walivyokuwa wakipewa majina ya utani kutokana na jinsi walivyokuwa wakiishi.
Mfano, kuna mtu alikuwa akiitwa ‘Sikafunje’ mwingine aliitwa ‘Sondamuno’ na mwingine ‘Kotoka.’ Majina yote yana maana kwa wale ndugu zangu wa mkoa wa Mbeya watakuwa wanayafahamu vizuri sana.
Lakini, leo nitajikita katika jina moja tu la ‘Kotoka.’ Katika kijiji cha Lusungo, wilaya ya Rungwe, alikozaliwa Kalagesye au Kanakansungumwelu, palikuwa na mtu aliyeitwa Andongolile.
Huyo alikuwa na matatizo kidogo ya akili, lakini akiwa hana matatizo na mtu mwingine.
Pamoja na hali yake hiyo, hakuwa mgomvi; alikuwa akiamka asubuhi na kwenda zake shambani kulima kama ilivyo kwa maisha ya wengine kijijini pale.
Lakini, akiwa shambani hakuwa akiondoka hadi mtu amwendee na kumweleza basi imetosha, vinginevyo angeshinda kutwa nzima akilima hata kukesha.
Hivyo, alihitaji mtu wa kumkumbusha kwa kumweleza ‘Ugwe Andongolile Kotoka.’ Yaani, ewe Andongolile maliza kazi na ondoka.
Akirudi nyumbani, kama kawaida angekwenda mtoni kuoga kabla ya kupata kifungua kinywa.
Hata kule mtoni, ilikuwa vivyo hivyo, hadi atokee mtu amwambie Kotoka, ndipo arudi kutoka Mtoni.
Kwa mantiki hiyo, huyo Andongolile kila shughuli aliyokuwa akiifanya, alikuwa hawezi kuiacha hadi alipoambiwa basi.
Ndio maana, namwambia Kayuni ‘Kotoka’ Mwasamaki afanye kazi ya ukocha kwa manufaa ya nchi.
Nimeanza kumfahamu Kocha Eugene Mwasamaki mwaka 1998, wakati huo akiifundisha Mbozi ya Mbeya.
Nilikutana naye katika michuano ya Ligi Daraja la Pili iliyofanyika mjini Tanga.
Alikuwa ni aina ya makocha wa kuigwa miongoni mwetu katika michuano ile.
Aidha, niliwahi kushiriki naye mafunzo ya juu ya ukocha chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), yaliyofanyika mwaka huo jijini Dar es Salaam.
Washiriki wengine katika mafunzo yale, alikuwa Sunday Kayuni, Dk. Mshindo Msolwa, Juma Matokeo, Abdallah Kibaden, Juma Pondamali, Madaraka Bendera, Iddy Kipingu.
Wakufunzi wetu alikuwa Stanley Fumo kutoka nchini Lesotho.
Ndio maana nasema, Sunday Kayuni ‘Kotoka’ amwache huru Mwasamaki atoe mchango wake kwa taifa.
Nasema hivi kutokana na ukweli kuwa hakuna kocha ndani ya nchi hii asiyetambua uwezo wa Mwasamaki.
Aidha hakuna mchezaji aliyecheza michuano ya Airtel, Copa Coca Cola au U-20 asiyemfahamu Mwasamaki.
Pamoja na yote hayo, hapewi hata usaidizi wa timu yoyote kati ya hizo, jamani kwangu naona kama dhuluma kwa Mwasamaki.
Ni mtu mwenye uwezo wa kuweza kumpatia hata nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inayoshikiliwa na Kayuni.
Mwasamaki amekuwa akifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na makocha wote wa kigeni, kuanzia Marcus Tinocco na wegineo.
Hata hivyo, inapofika suala la kupewa timu na hasa za taifa, iwe ile ya wakubwa, U-17, U-20 au Twiga Stars, Mwasamaki anawekwa benchi.
Ndiyo maana nasema Sunday “Kotoka” mwangalie Mwasamaki rudisha moyo nyuma kwani wewe ni mtu wa dini, sahau yaliyopita weka utaifa mbele.
Nikirudi miaka minne iliyopita wakati wa kampeni za uchaguzi wa Chama cha Makocha wa Soka Tanzania (Tafca), kulikuwa na kambi mbili tofauti.
Bahati mbaya, mwenyekiti wa wakati ule ambaye ndiye Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, alikuwa kambi tofauti na Katibu wake, Mwasamaki.
Lakini, mwisho wa siku katibu yule alishinda tena kwa kishindo.
Tatizo lilianzia hapo kwa mheshimiwa yule kuweka nongwa ambayo inaendelea kufanya kazi hadi leo.
Ndiyo maana, nimeamua kuiga ile hadithi niliyowahi kusimuliwa na bibi yangu kuhusu Andongolile aliyekuwa akifanya kitu mpaka aambiwe acha.
Kayuni mwache huru Mwasamaki (kotoka); umembana sana Mwasamaki, pengine mtu huyu anaponzwa na hulka yake ya ukimya.
Mwasamaki, leo ndiye aliyekuwa mpiganaji mzuri wa michezo ya ASPIRE inayounganisha vijana wa chini ya miaka 17 wa Tanzania, Rwanda, Kenya na Uganda.
Ni michuano inayofanyika kila mwaka mjini Nairobi, hivyo wachezaji wengi kupita kwenye mikono yake hadi kufika Qatar.
Leo hii, kurugenzi ya ufundi chini ya Sunday Kayuni, imemtupa mbali Mwasamaki na kumchukua Salum Madadi na Katibu Msaidizi wa Tafca, Bundala.
Hivi, Mwasamaki amefanya nini hadi kutendewa hivi, haijulikani huku tukishuhudia tu mkurugenzi huyo akipeta.
Ndio maana mmoja wa watu wanaoguswa na jambo hili, leo nafungua kinywa na kusema, Kayuni inatosha.
Nasema kwa Mwasamaki inatosha endelea kuwabania wengine kama Mwaisabula na Mtoro Alli ambao licha ya kuwa na vigezo vyote vya elimu ya kidato cha nne na Chuo Kikuu (Mtoro), lakini wanaambiwa leseni mtazisikia kwenye bomba.
Lakini, Kayuni kumbuka kila chenye mwanzo, kina mwisho wake, hivyo tumia enzi yako, lakini yaja zamu ya wengine wakiwemo unaowabania.
Naandika makala hii nikitambua fika kuwa wengi hawapendi kuambiwa ukweli, basi nakitonesha kidonda kile ambacho miaka minne iliyopita niliwahi kukigusa.
Niliandika kuhusu makocha walio viogozi kwenye utawala wa soka, lakini wakishindwa kutekeleza waliyokuwa wakiyapigania kabla ya madaraka.
Waliniita kwenye kikao kujadili hilo, lakini nashukuru ujumbe waliupata akiwemo Kinanda Zacharia.
Hata hivyo, wakaishia kusema, haikuwa vema kumhoji mwandishi wa makala, bali kufanyia kazi dosari zilizokuwa zimegusiwa.
Napata shida kuandika makala hii kwa jinsi ninavyoufahamu upole wa Mwasamaki, pia asiyependa makuu, hivyo atakaposoma makala hii, huenda naye atashtuka.
Naamini hataishia hapo, huenda akaungana na yule mbaya wake kunichunia kwa kuamua kuuweka bayana ukweli wa mambo.
Hata hivyo, nasema liwalo na liwe lakini imefika wakati sasa Kayuni atambue anavyofanya kwa mtu huyo sio haki.
Umefika wakati, jambo hili likemewe kwa nguvu zote, sidhani kama Rais wa TFF, Leodger Chilla Tenga na wasaidizi wake akiwemo Mtemi Ramadhani, Msafiri Mgoi, Iddi Mshangama, hawajui jambo hilo.
Kwa kuwa Tenga ni msomi na muelewa basi na wewe tusaidie kumwambia mheshimiwa huyo ‘Kotoka’ tayari muda wake umefika amwache afanye kazi.
Aidha, msiachane mwezi Desemba kwa chuki badala ya udugu, hasa kwa kuzingatia wote mnatoka sehemu moja.
Wiki ijayo nitawaletea makala ya makocha kisa cha nyumbu 400 kunyanyaswa na Simba mmoja.
Namna chama cha makocha kilivyoanzishwa na malengo yake yalikuwaje na yakoje sasa.
Tukutane wiki ijayo, lakini nasema Kayuni ‘Kotoka’

No comments:

Post a Comment