Search This Blog
Thursday, July 26, 2012
BAADA YA KELELE ZA WADAU: CECAFA SASA KUHAMISHIA KAGAME CUP MWEZI JANUARY
MICHUANO ya Kombe la Kagame mwakani inatarajiwa kufanyika mapema mwezi Januari ili kuziandaa timu za Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya kombe la klabu bingwa na mashindano ya koombe la Shirikisho la Soka Afrika CAF.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye alisema wameamua hivyo baada ya kuona mapungufu makubwa katika timu za Ukanda wake hivyo mashindano ya mwaka huu yakimalizika Jumamosi Cecafa itakaa na viongozi wa vyama vya soka vya nchi husika na kuzungumza nao kuangalia namna ya kuweka mfumo mpya wa ratiba ya ligi zao.
"Tutakaa na viongozi wa vyama vya soka vya Ukanda wetu kuangalia jinsi ya kuendesha ligi katika nchi za Ukanda wetu ili zisipishane kama ilivyo sasa, mfumo wa ligi uwe mmoja na mashindano haya yawe kwa ajili ya kuzisaidia timu zifanye vizuri kwenye mashindano ya CAF,"alisema Musonye.
Kauli ya Musonye imekuja baada ya Ethiopia kuyatolea nje mashindano haya ya Kagame kutokana na Ligi Kuu ya nchi hiyo inayoendelea, wakati Tanzania imemaliza Ligi tangu mwezi Mei kitendo ambacho kinazipa wakati mgumu timu za Yanga, Azam na Simba.
Hata hivyo tayari makocha mbali mbali wamekuwa wakipigia kelele michuano hiyo kuwa haina tija kwa timu zinazoshiriki kwa kuwa inafanyika kukiwa hakuna michuano yoyote ya kimatafa mbeleni kitu ambacho kinazifanya timu za Ukanda wa Cecafa kuonyesha kiwango kibovu inapofika michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) tofauti na timu zilizopo Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Cosafa).
Kocha wa Mafunzo, Hamed Moroco alikaririwa akisema, "Ninachokiona ni kwamba tunacheza Kagame hivi sasa na mashindano yakimalizika kunakuwa na nini? Nini malengo ya mashindano haya?...Sawa, mashindano yamefanyika na baada ya hapo kuna miezi mitano hadi sita kufikia Februari mwakani tunapoanza michuano ya Caf kwa klabu, hii sioni kama ina tija sana."
Hata hivyo Musonye jana aliiambia gazeti la Mwananchi kuwa kufanya vibaya kwa timu za Ukanda huu katika mashindano ya Afrika wasilaumiwe Cecafa kwani klabu zenyewe zimeshindwa kuandaa timu zao na ndio maana zimekuwa zikiboronga kwenye mashindano mbalimbali.
"Mashindano yetu kama hayasaidii na mnayafananisha na bonanza mbona hayo mashindano mazuri ya Caf klabu za Ukanda huu hazifiki popote?, Cecafa hatuendeshi klabu, hatufanyi usajili kwenye klabu, viongozi wenyewe wa klabu wameshindwa kuandaa timu zao sasa Cecafa tufanyaje? timu kubwa tu inacheza ligi kuu inapigwa bao tano umeona wapi hii?,"alihoji Musonye.
"Badala ya kuandaa timu zifanye vizuri kwenye michuano ya kimataifa wao wanaona sifa kushinda ubingwa wa ligi, kombe la Muungano ikifika michuano ya Caf wanafungwa hawafiki hata hatua ya makundi wanarudi nyumbani wanakaa kaa tu hapa,"alisema Musonye.
Hata hivyo Musonye alisikitika kuondoka mapema kwa timu za Simba, URA, Atletico na Tusker na kudai kuwa alikuwa akizipa nafasi kubwa ya kufika mbali katika mashindano hayo ambayo yamedhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
"Hizi timu zimeingia kwenye mashindano kwa mazoea, hazikufanya maandalizi ya kutosha, nazipongeza timu zilizobaki zitaleta ushindani mkubwa kwa kuwa zimeonyesha kiwango kizuri katika mashindano haya, hakuna upendeleo wowote tunaofanya Cecafa kama ni kupendelea basi ningependelea timu ya nchi yangu Tusker,"alisema Musonye.
Alisema,"nasikia watu wanasema nazipendelea Simba na Yanga, haya Simba hiyo imeondoka naipendelea na nini eti kwa sababu ya posho, posho gani Simba imeondoka sasa kila timu itashinda kwa uwezo wake hakuna upendeleo wowote."
Mwananchi.co.tz
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
cecafa wanazingua au alie upload picha hii mbona ni ya kikombe kimeandikwa sport club villa tena walikuwa mabingwa 2003,kimewekwa taifa mechi ya fainal kati ya simba na yanga,ss kwa nn isito villa wakati wao c mabingwa?
ReplyDelete