Search This Blog

Tuesday, June 5, 2012

Kili Taifa Stars yarejea kutoka Ivory Coast

·        Poulsen asema nguvu zote sasa zimeelekezwa katika mechi ya Gambia
TIMU ya Taifa-Kilimanajro Taifa Stars jana imerejea nyumbani ikitokea Ivory Coast ambako ilicheza mechi yake ya kwanza ya kufuzu kucheza kombe la dunia ambapo ilishindwa na mwenyeji wake kwa magoli mawili bila.

Ndege iliyowabeba wachezaji 23 wakiongozwa na kocha Kim Poulsen, benchi la ufundi, viongozi mbalimbali wa TFF na waandishi wa habari ilitua katika Uwanja wa KImataifa wa Julius Nyerere saa moja na nusu asubuhi ikitokea Nairobi baada ya kuondoka Ivory Coast saa nne za usiku saa za frika Mashariki.

Wachezaji hao walipokewa na viongozi mbalimbali wa TFF akiwemo Katibu Mkuu Angetile Osiah.

Mara baada ya kuwasili Kocha Kim Poulsen alisema baada ya matokeo ya mechi yao na Ivory Coast, sasa hivi timu yake imeelekeza nguvu zote katika mchezo wa Gambia utakaochezwa Jumapili Jijini Dar es Salaam.

“Matokeo hayakuwa mazuri kwetu ila vijana walicheza vizuri na tunatumai tutafanya vizuri katika mechi ijao dhidi ya Gambia,” alisema..

Alipoulizwa kuhusu timu kuchelewa kurudi alisema wamekuwa wakifanya mazoezi nchini Ivory Coast kila siku tangu tmu iondoke Dar es salaam Alhamisi iliyopita.

Huku akiwashukuru wadhamini wapya wa Timu ya taifa, TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager,  Poulsen alisema mapokezi nchini Ivory Coast yalikuwa mazuri na wachezaji walionesha nidhammu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja.

“Tulicheza vizuri lakini wenzetu wana uzoefu na wana kikosi kizuri kwa hivyo wanatuzidi lakini tunajitahidi ili tuweze kucheza vizuri zaidi kila tunapoingia uwanjani.

Naye nahodha wa Timu ya Kilimanjaro Taifa Stars, Juma Kaseja, alisema mechi yao dhidi ya The Elephants ilikuwa ngumu lakini wachezaji walijitahidi kucheza vizuri.

Alisema anaamini watapata matokeo mazuri katika mchezo dhidi ya Gambia utakaopigwa katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili.

Hii ilikuwa ni mechi ya kwanza ya Taifa Stars ya mchujo wa kufuzu kucheza katika mashindano ya kimataifa tangu ipate mdhamini mpya-Kilimanjaro Premium Lager na pia tangu timu hii itangazwe na kocha Poulsen.

Tayari watanzania mbalimbali waishio ndani na nje ya Tanzania wametoa maoni yao kuhusiana na ttimu hii na kwa mujibu wa wengi, timu hii inaonesha matumaini makubwa.

Watu mbalimbali nchini Ivory Coast wakiwemo wachezaji nyota kama Didier Drogba, Solomon Kalou, Yaya Tourre na wengine walistaajabishwa sana na kiwango cha hali ya juu kilichoonesha na Taifa Stars.

No comments:

Post a Comment