Search This Blog

Wednesday, June 13, 2012

EURO 2012: UJERUMANI VS UHOLANZI - WAPINZANI WA JADI WA KIHISTORIA NANI KUCHEKA LEO.

Wakati timu ya taifa ya Ujerumani au the Die Menschaff ikiwa imetulia kambini ikisubiri jukumu lililoko mbele ambalo kuwakabili wapinzani wao wa miaka mingi Uholanza, wapinzani wao hao  wamekuwa wakipambana wenyewe kwa wenyewe kama walivyozoea .
Vichwa vya habari vya magazeti ya michezo nchini Uholanzi kuelekea kwenye mchezo huu vimepambwa na kauli mbaya za Rafael Van Der Vart ambaye amekuwa mwepesi kusema yaliyo moyoni mwake dhidi ya kocha Bert Van Marwick, Klaas Jan Huntelaar naye hajabaki nyuma huku wengine kina Nigel De Jong na Wesley Sneijder wakihusika kwenye utata uliokizunguka kikosi cha Oranje .
Upande wa pili wajerumani wameshikama wote wakitambua mtihani ulioko mbele na wamekuwa wakiifikiria timu kwanza kabla ya kufikiria jinsi ambavyo baadhi wamekuwa wakiwekwa benchi na wengine wakicheza.
Hii ndio tofauti ya kwanza ambayo inaweza kuamua mchezo huu wa watani hawa wa jadi kwa miaka mingi.
Kila mmoja akiingia uwanjani na ajenda yake tofauti lakini wote wawili wana agenda ya kufanya vizuri na kuchukua pointi zote tatu huku Uholanzi wakionekana kuzihitaji pointi hizo pengine kuliko Ujerumani .
Ukiingia kwenye idara ya ufundi kujaribu kupata ufumbuzi wa kipigo walichopata Uholanzi toka kwa Denmark utagundua yafautayo, kimsingi kabisa Uholanzi hawakupaswa kupanga mfumo ambao uliwajumuisha viungo wakabaji wawili ambao ni De Jong na Van Bommel. Mfumo huu uliwafanya Uholanzi kukosa ubunifu wa ziada kwenye idara ya ushambuliaji. Tatizo lingine ambalo limeonekana ni kutomjumuisha Klaas Jan Huntelaar . Robin Van Persie alipangwa kwenye sehemu ya ushambuliaji wa kati, hakuna anayeweza kusema kuwa Van Persie si mchezaji mzuri, la hasha lakini kwenye mfumo wa uholanzi sio mara nyingi amekuwa akipangwa kama mtu ambaye anaongoza mstari kwenye ushambuliaji na hapa ndio unagundua tatizo. Ibrahim Affelay hajacheza sehemu kubwa ya msimu huu na kwenye nafasi yake angeweza kupangwa Van Persie halafu Affelay akasubiri kuleta impact kama Supersub huku Huntelaar akicheza kama mshambuliaji wa kati .
 Mchezo dhidi ya Ujerumani hauna budi kushudia mabadiliko haya endapo Uholanzi watataka kuweka hai matumaini yake ya kusonga mbele.
Ujerumani kwa upande wao sio kwamba walicheza vizuri kwa kustahili alama za asilimia mia moja kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya Ureno, kulikuwa na matatizo sehemu kadhaa, Lukas Podolski alikuwa na matatizo hasa kwenye jinsi ya kuipenya ngome ya Ureno na kwenye umaliziaji pia  kama ilivyokuwa kwa Thomas Mueller. Kilichowapa ufanisi mkubwa wajerumani ni juhudi za wachezaji hawa hasa pale ambapo mambo yalionekana kuwaelekea kombo , walifanya kazi kwa juhudi kubwa na matokeo yake yalikuwa ushindi wa bao moja dhdi ya timu nzuri na ngumu ya Ureno.
Ujerumani wanaweza kufanya mabadiliko endapo watataka kumaliza mchezo mapema, kuna wachezaji kama Andre Schurrie na Marco Reus ambao wanaweza kuingia kwenye nafasi za kina Podolski na Mueller japo hakuna ulazima wa haraka wa kushuhudia mabadiliko haya .
Tatizo kubwa la Uholanzi siku ya jumamosi lilikuwa umaliziaji . Takwimu zinaonyesha kuwa Uholanzi kwenye mechi dhidi ya Denmark walipiga mashuti 22 ambayo hayakulenga lango. Hii ndio idadi kubwa ya mashuti yaliyopotea mwelekeo kuliko timu yoyote ya taifa au klabu yoyote ile kwenye ligi zote kubwa  barani ulaya. Na hapa ndio panaweza kuhitaji mabadiliko. Pamoja na kwenye ushambuliaji mabadiliko mengine yanaweza kuonekana kwenye safu ya Ulinzi ambako Joris Mathijsen amepona na huenda akaingia kwenye nafasi ya Ron Vlaar, hata hivyo mabadiliko ambayo Kocha Van Marwick anapaswa kufikiria kuyafanya ni yale ya kupunguza kiungo mkabaji mmoja na kuongeza kiungo mbunifu kama Rafael Van Der Vart hasa ukizingatia mchezo wa kwanza wa Ujerumani ambapo wajerumani walikuwa wanapitika kiwepesi jambo ambalo linaweza kumpa Bert mawazo kwamba staili ya mchezo ya wajerumani ya kutegemea sana mashambulizi ya counter itakuwa nzuri akiwa na kiungo wa ziada kama Van Der Vart.
Mchezo kati ya Uholanzi na Ujerumani kihistoria ni mchezo ambao utazifanya timu zote ziwe na morali ya ziada kumkabili mpinzani wake. Mara nyingi Ujerumani wamekuwa wakiwanyanyasa wadachi , mazingira ya michezo ya kwanza ya timu hizi yanawafanya wadachi kuwa na sababu ya ziada ya kushinda kwani kitu chochote pungufu ya pointi tatu kitamaanisha kuwa Uholanzi itakuwa ianchungulia kaburi.

No comments:

Post a Comment