*Apata balaa jingine, Wasauz wamkatia rufaa
*Yanga yapita, azuiwa kucheza nane bora Afrika
Na Saleh Ally
WIKI ILIYOPITA, tuliishia wachezaji wa Yanga akiwamo Bakari Malima wakiwa wameomba mechi yao ya marudiano dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda ichezwe mjini MWanza kwa lengo la kukimbia presha kubwa ya mashabiki jijini Dar es Salaam. Uongozi ukakubali na maandalizi yakaanza. Endelea.
TULIENDELEA na maandalizi siku kadhaa tukiwa jijini Dar es Salaam, baada ya hapo tukafunga safari kwenda Mwanza kwa ajili ya kuweka kambi huku tukiisubiri mechi dhidi ya Rayon Sports.
Wachezaji tulijua ugumu wa Wanyarwanda lakini tulipania kushinda na kuweka rekodi ya kuifikisha Yanga kwenye hatua ya Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mashabiki wengi wa soka walifunga safari kutoka Dar es Salaam kuja Mwanza kutuunga mkono.
Siku ya mechi, kama ambavyo tulitarajia, ilikuwa ni ngumu na wapinzani wetu walionekana walikuwa wamejiandaa vilivyo kushinda ugenini na kusonga mbele. Walijitahidi wakapata bao lakini nasi tulifunga bao zuri lililopachikwa kimiani na mshambuliaji wetu, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.
Mechi iliisha kwa sare ya bao 1-1, maana yake Yanga tulikuwa tumefanikiwa kuvuka hadi hatua ya Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati huo tulikuwa tunasema Klabu Bingwa Afrika. Sherehe zilianzia pale CCM Kirumba hadi sehemu mbalimbali za mji wa Mwanza.
Sherehe hizo zilikuwa ni za aina yake, kwani ziliendelea jijini Dar es Salaam na sehemu nyingine nchini. Tulikuwa tumeweka rekodi mpya kwa Yanga. Binafsi nilijisikia vizuri kwa kuwa nilikuwa nimetimiza malengo ya kuilipa Yanga mazuri kwa kuwa viongozi walionyesha mapenzi kwangu.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, tulianza mara moja maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo pamoja na mingine iliyokuwa inakabiri Yanga. Kwangu, angalau niliona kama maisha yalianza kwenda vizuri tena, nilianza kuishi kawaida.
Ingawa suala la mahakamani hukumu ilishatolewa na nikaonekana sina hatia, bado wako ambao waliamini kama haikuwa sawa. Hali hiyo iliniumiza sana, kwani kila aliyejaribu kukumbushia alitonesha jeraha nililopata kwa kupata matatizo kwa kitu nisichokijua hata kidogo. Bado niliendelea kumuachia Mungu.
Niliendelea na maisha yangu ya kawaida, mara kadhaa nilikuwa nikiwasiliana na uongozi wa Vaal Professional kuhusiana na suala la kurejea Afrika Kusini. Niliona ningeweza kufanya hivyo kwa kuwa pamoja na kupata matatizo walionyesha ustaarabu kwangu.
Lakini niliona ni vizuri kama ningemaliza jukumu la kupambana kwa ajili ya Yanga kwenye michuano hiyo mikubwa ya Afrika. Maana tayari ratiba ilishatoka na tulipangiwa kuanza mechi dhidi ya Maning Rangars ya Afrika Kusini.
Nilijua ingekuwa ni mechi ngumu kwa kuwa Wasauz wana kila kitu, hivyo lazima wangejiandaa vya kutosha kwa ajili ya mechi hiyo. Lakini binafsi nilikuwa nikifanya mazoezi kuhakikisha nakuwa fiti sawasawa.
Balaa likaibuka tena, Maning Rangers kwa kuwa walikuwa wananijua wakanikatia rufaa kwamba sitakiwi kucheza michuano hiyo kwa kuwa mkataba wangu wa miaka mitatu na Vaal ulikuwa haujamalizika. Nilichanganyikiwa, lakini nikawa na matumaini huenda Shirikisho la Soka Afrika (Caf), litapuuzia.
Ingawa niliingia hofu ya kutoichezea Yanga, lakini niliamua kuweka pamba masikioni na kuendelea na mazoezi kwa nguvu kama vile nilikuwa na uhakika ningeichezea Yanga kwenye michuano hiyo hatua ya nane bora.
Siku chache kabla ya kuivaa Maning Rangers, Yanga ilipokea barua kutoka Chama cha Soka Tanzania (Fat), ilikuwa inatokea Caf. Barua hiyo ilitoa maelekezo kwamba nisingeruhusiwa kucheza, si mechi dhidi ya Wasauz pekee, badala yake zote.
Kwangu ilikuwa ni kama kisu moyoni, niliona maisha yangu yalikuwa yamejaa misukosuko. Ilikuwa kama wamenikumbusha upya matatizo yaliyonipata wakati ninatokea Sauz. Niliamua kwa mara nyingine kumuachia Mwenyezi Mungu.
Nikakaa kando na kuwa mtazamaji, bahati mbaya Yanga haikufanya vizuri katika michuano hiyo, ilitolewa mapema sana. Nilisikia uchungu kwa kuwa niliona huenda kuwepo kwangu kungekuwa msaada kwa kushirikiana na wenzangu na tungeweza kuikoa Yanga. Kukosekana kwangu ni kama kulipunguza nguvu, sikuwa na namna.
Baada ya hapo, niliichezea Yanga kwenye ligi na tulifanikiwa kuwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika nchini Uganda. Nakumbuka sana, hiyo ni mwaka 1999, safari yetu ilikuwa ni ya kubangaiza.
Tulisafiri kwenda Uganda kwa usafiri wa kuungaunga. Nakukumbusha sisi ndiyo tulitwaa ubingwa kwenye michuano hiyo, lakini safari yetu kwenda ilikuwa ni ngumu kupindukia na hakukuwa na posho, lakini wachezaji tukawa tayari kupambana.
Tulisafikirishwa kwa mafungu mawili kwa basi. Awali uongozi ulitaka kuitoa timu lakini sisi tukasema tutacheza. Tuliondoka tukiwa na pea moja tu ya jezi, maandalizi yetu yalikuwa mabovu kuliko timu yoyote iliyoshiriki michuano hiyo.
MALIMA anaongozana na Yanga kwenda Uganda, maandalizi ni mabovu, timu haina fedha lakini mwaka huo wa 1999, Yanga walikuwa mabingwa. Je, ilikuwaje hadi wakafanikiwa huku maisha yao yalikuwa ya kuungaunga? USIKOSE EPISODE-8
No comments:
Post a Comment