*Akubali kusaini Jangwani bila kuuliza hata mshahara wake
Na Saleh Ally
WIKI ILIYOPITA, Malima alikuwa anawasili katika mahakama ya Kisutu akiwa mshitakiwa wa madawa ya kulevya. Kwa kuwa taarifa kuhusiana na suala hilo zilikuwa zimeripotiwa kwenye vyombo vya habari, watu walikuwa wengi sana, hali iliyomfanya awe mwoga. Nini kitafuatia? Endelea.
TULITEREMKA pale mahakamani huku idadi kubwa ya watu ikiwa inatusubiri, niliwaona baadhi ya watu niliokuwa nawajua wakiwemo mashabiki wa Yanga. Wengi waliniangalia kwa jicho la huruma.
Suala hilo kwa kiasi kikubwa lilinichanganya sana, niliona kama ni mtu ninayeonewa lakini ilikuwa vigumu kuwaeleza watu kilichokuwa kinaendelea ili wanielewe.
Ukichana na hivyo, nisingeweza kupata nafasi ya kuwaeleza namna mambo yangu yalivyokwenda vibaya. Nilichofanya ni kuangalia chini ili kupunguza uchungu kwa kuwa nilihisi huenda ningemwaga machozi.
Baadhi ya watu wa Yanga walikuwa pale wakipiga kelele kunipa moyo kuwa nisijali kwani kila kitu kitaisha. Walinipa moyo kiasi cha kunifanya niamini kweli Yanga ni nyumbani kwangu, hilo ninaliamini hadi leo.
Tuliingia mahakamani na tukaanza kusomewa mashitaka, hatukutakiwa kuzungumza lolote na baada ya hapo tukaombewa dhamana. Lakini tukaelezwa tusingeruhusiwa kupewa dhamana kutokana na uzito wa jambo lenyewe.
Hali hiyo ilinichanganya zaidi, niliona mambo yanazidi kuwa mabaya. Nilikanganyikiwa hasa baada ya kukosa hata nafasi ya kuwaona ndugu zangu. Nikajua ndiyo mwisho wangu.
Yule dada aliendelea kulia, hali hiyo ilinitia huruma sana kwa kuwa niliona kama mimi ndiyo chanzo cha tatizo. Lakini sikuwa na sababu ya kujilaumu maana sikujua lolote kuhusiana na litakalofuatia na wala sikuwa na nia mbaya kwake.
Wakati tukiwa tunajiandaa kupanda karandinga kwenda Segerea, tuliijiwa na kuambiwa dhamana ilikuwa imepatikana. Sikuamini, pia sikujua nani aliyetusaidia kiasi hicho.
Baada ya kutoka, nikagundua walioniwekea dhamana mimi na yule dada ni viongozi wa Yanga ambao tayari walishaanza kushughulikia suala la wanasheria kwa ajili ya kutusaidia kuendesha kesi yetu kitaalam zaidi.
Nilifanikiwa kutoka, ingawa kwa dhamana angalau niliona kama nilikuwa huru kwa kiasi fulani maana siku hiyo ningelala nyumbani. Kikubwa nilitakiwa kukutana na viongozi wa Yanga kujadili kuhusiana na suala hilo.
Hakika sikuwa na ubishi kwa sababu ya mambo mawili makubwa, moja Yanga ipo kwenye damu yangu na hupaswi kuuliza hata chembe. Pili, nilikuwa kwenye matatizo ambayo yananifanya niwe msikivu kupindukia.
Nilipokutana na viongozi wa Yanga, walinieleza namna ninavyoweza kusalimika, kwamba ni kuacha sheria ifuate mkondo wake. Lakini niwe mkweli kwa wanasheria watakaoniwekea.
Wakanipa sharti moja kuwa wao watanipigania hadi mwisho lakini nilitakiwa kufanya kitu kimoja, kuachana kabisa na mambo ya Afrika Kusini, niisahau timu yangu ya Vaal na kusaini Jangwani.
Wakati huo Yanga ilikuwa imefanikiwa kuvuka na kuingia kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ilihitaji mtu ambaye ni imara kwa ajili ya sehemu ya ulinzi wa kati. Jembe Ulaya likawa chaguo lao.
Sikuwa na sababu ya kubisha, nilikubali haraka sana na nikawaahidi nitafanya mawasiliano na Afrika Kusini na kuwaeleza hali halisi ilivyo ili wasinione ni mbabaishaji.
Unajua wakati ule tumekwenda na Nonda, yeye akasajiliwa na mimi nikakosa kibali, nilikuwa ninawasiliana na mmiliki wa timu hivyo sikupenda kumuangusha maana alifanya juhudi na kunisajili.
Nikakubali kusaini Yanga kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa, kutokana na namna mambo yangu yalivyokuwa mabaya, sikuthubutu kuomba hata senti moja wala kuulizia mshahara wangu utakuwa ni kiasi gani.
Siku ya kusaini, nilizirukia karatasi fasta, nikasaini kwa ajili ya kuichezea Yanga katika michuano hiyo mikubwa huku nikiendelea kupambana na sakata langu ambalo liliendelea kusikika kila sehemu.
Wakati nilipoanza mazoezi Yanga, kila mmoja alitaka kuniona. Mashabiki walijitokeza kwa wingi kutaka kuniona na walikuwa wakinishangaa sana, lakini nilijikausha na kuendelea na shughuli zangu. Nilifanya mazoezi kwa nguvu sana.
Wakati yote yanaendelea, nilijiuliza mara kadhaa ninavyoweza kuzungumza na Wasauz na kuwaeleza kuwa sitarudi kwa kuwa nilishikwa na madawa ya kulevya. Ilinichanganya sana lakini nikaamua kupiga na kuzungumza nao.
MALIMA ameamua kuzungumza na timu yake kuhusiana na kilichomtokea. Je, viongozi wa timu hiyo watamuelewa? Watachukua uamuzi gani wakati yeye tayari ameshasaini kuichezea Yanga huku akiwa na mkataba nao? ITAENDELEA.....
Poa tunasubiri kaka PELLE WA TZ
ReplyDelete