Search This Blog

Thursday, May 17, 2012

YANGA KWAZIDI KUCHAFUKA: MINZIRO NAIDAI YANGA MSHAHARA WA MIEZI MINNE

Kocha  msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro amesema hataifundisha timu hiyo inayojiandaa kutetea taji la michuano ya Kombe la Kagame kama uongozi wa klabu hiyo hautamlipa malimbizo yake ya mishahara ya miezi minne.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Minziro alisema hajalipwa mishahara tangu mwezi Februari na juhudi zake za kudai hazionyeshi matumaini kutokana na kutopata jibu la kuridhisha.
Minziro alisema majibu anayopata ni ya kukatisha tamaa na pamoja na uongozi kutangaza kuwa atasimamia mazoezi kwa ajili ya kombe la Kagame.
Kocha huyo, alisema pamoja na mapenzi makubwa aliyonayo kwenye klabu hiyo, hatakuwa tayari kuendelea kufanya kazi katika mazingira magumu ya kutolipwa mshahara.“Uzalendo umenishinda, binadamu wa kawaida hawezi kuishi maisha ya bila mshahara na hakuna matarajio ya kupata fedha hizo kutokana na hali halisi ya klabu hiyo,” alisema Minziro.
Alisema kuwa alipata matumaini ya kulipwa fedha zao mara baada ya mechi ya Zamalek, lakini wakapewa hadithi na baadaye akaambiwa atalipwa baada ya mchezo dhidi ya Simba, lakini mpaka sasa hajalipwa.
“Hali hii ni ya muda mrefu, benchi lote la ufundi tunadai mishahara ya miezi mitatu. Kukosekana pesa kwa wakati kumechangia kwa kiasi kikubwa kushusha morali ya wachezaji na hata sisi wenyewe,” alisema.
Alisema pia anashangaa kuona tangu ligi ilipomalizika hakuna kikao chochote cha kufanya tathmini kilichofanyika ikiwemo maandalizi ya usajili wakati yeye sasa ndiye Mkuu wa Benchi la Ufundi.
Kocha huyo alisema mbali na mishahara yake ya miezi minne, pia anadai posho za mechi 15 na kuweka wazi kwamba kila mechi hulipwa Sh. 100,000.
Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na kusema ni masuala binafsi ya makocha hao.

No comments:

Post a Comment